Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeimarisha nguvukazi kwenye sekta ya afya kwa kuongeza taasisi zinazotoa mafunzo ya afya na upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa kada hiyo.
Akizungumza na viongozi, wadau na watumishi walioshiriki ufunguzi wa mkutano wa pili wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika sekta ya afya leo Julai 30, 2024, Waziri Mkuu amesema serikali ya awamu ya sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu zinapatikana kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa.
“Serikali imefanya upanuzi wa taasisi za mafunzo ya afya ili kuongeza idadi ya wahitimu, taasisi hizo ni pamoja na vyuo vya uuguzi, ukunga na utabibu, hivi sasa nchi yetu ina taasisi 182 zikiwemo taasisi 137 zinazomilikiwa na sekta binafsi ni jambo la faraja kuona kuwa katika mwaka 2023/2024 peke yake, vyuo hivyo vimedahili wanafunzi 40,000,” amesema Waziri Mkuu
“Lakini pia, wanafunzi wanaosomea kozi za afya wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100 vilevile, suala la kuendeleza rasilimali watu limeendelea kuwa kipaumbele cha serikali kwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kila mwaka ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa,” ameongeza.
Akielezea kuhusu ajira na upangaji wa watumishi wa kada za afya, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita, watumishi 30,000 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi vikiwemo vya vijijini.
“Baadhi ya watumishi hao ni pamoja na madaktari, wauguzi pamoja na wakunga hii ni hatua kubwa sana ya maendeleo katika utoaji wa huduma za afya nchini,” amesema.