ZRA kukusanya mapato ya ndani Sh845 bilioni za Zanzibar

Unguja. Ili kufikia lengo la kukusanya mapato ya ndani ya Sh845 bilioni, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imeweka mikakati maalumu ya kuhakikisha fedha hizo zinapatikana ikiwamo kuwasajili walipakodi wapya na kutoa elimu kwa wafanyabiashara.

Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo leo Julai 30, 2024, Kamishna wa Walipakodi Wakubwa ZRA, Shaaban Jaffar Jumanne amesema ni lazima kujiwekea mikakati ya kuvuka malengo yaliyowekwa ili kuimarisha ulipaji kodi.

Pia, mkakati mwingine amesema ni kuendelea kusimamia mfumo wa matumizi ya kielektroniki hususani katika utoaji wa risiti kwa kuwa bado hilo ni changamoto kwa wafanyabiashara na wananchi.

“Ni lazima kuwasajili walipakodi wote ambao wapo nje ya wigo ili iwe rahisi kuwafikia,” amesema Shaaban.

Amesema kutokana na mikakati hiyo wanaamini kuwa, lengo la kukusanya kiasi hicho cha fedha mwaka 2024/25 kitafikiwa.

Shaaban amesema ili kuwafikia wanaokwepa kulipa kodi, wameandaa mkakati wa kutoa risiti na kufatilia madeni kila ifikapo mwisho wa mwezi.

Hata hivyo, amesema bado wananchi hawadai risiti wanapofanya ununuzi na wafanyabiashara na hawaandiki bei halisi ya bidhaa wanazouza, hivyo ni muhimu kudai risiti ili iwe uthibitisho bidhaa itakapoleta shida.

Meneja wa kampuni idara ya walipakodi wakubwa ZRA, Khadija Abdallah Suleiman amesema wana mkakati wa kuhakikisha wanafuatilia miradi yote kwa lengo la kuhakikisha hawapotezi mapato ya Serikali.

Pia, amesema wanahakikisha walipakodi wakubwa wanaunganisha mifumo yao na kupata kodi stahiki ili kupunguza mianya ya ukwepaji kodi.

Meneja wa Mkoa wa Mjini Magharibi Kikodi, Suleiman Iddi amesema kikao hicho kinawataka wahakikishe wananchi wanadai risiti na wafanyabiashara watoe risiti ya kielektroniki ili mapato yapatikane.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi namba saba ya mwaka 2009, ukishindwa kutoa risiti moja faini ni Sh2 milioni na kwa mwananchi ambaye hadai risiti faini yake Sh30,000.

Related Posts