NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Mb) amekutana na Balozi wa Canada nchini Tanzania anayemaliza muda wake, Mhe. Kyle Nunas.
Akiongea leo hii katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mhe. Nyongo akiwa na mgeni wake Mhe. Nunas walijadili mambo mbalimbali kuhusu uwekezaji nchini na ushirikiano na watu wa Canada.
“Uhusiano wetu umekuwa wa muda mrefu, zaidi ya miaka 60, na bado tunaendelea kudumisha uhusiano huu kwa kuboresha mazingira mazuri ya uwekezaji kutoka Canada kuja nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uchakataji wa mazao, na mheshimiwa balozi ametuhakikishia kwamba balozi anayekuja ataendeleza na kuboresha yale yaliyokwisha fanywa kwa kuwakaribisha wawekezaji zaidi, hususan katika sekta za miundombinu, habari, nishati safi, na madawa,” alisema Mhe. Nyongo.
Pia, Mhe. Nunas amemshukuru na kumpongeza Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia, kwa kuunda kamati ya kuangalia masuala ya kodi ili kujenga na kudumisha mazingira rafiki ya uwekezaji nchini Tanzania.