BIL 3 ZIMETOLEWA MATENGENEZO BARABARA ZILIZOATHIRIWA NA EL-NINO MKOANI NJOMBE-ENG RUTH

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kushughulikia Barabara zilizoathiriwa na mafuriko/Mvua za El-Nino kwa mkoa wa Njombe.

Fedha hizo zimetumika kuhakikisha kuwa miundombinu yote ya Barabara iliyoathiriwa na wananchi kushindwa kutoka eneo moja Kwenda jingine inapitika kwa haraka kama ambavyo serikali imekusudia.

Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya miradi ya Barabara inayoendelea na matengenzo mbalimbali Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shaluwa amesema kuwa Maeneo ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoathiriwa na Mvua za El Nino mwezi Januari – Mei, 2024 ni Itoni – Ludewa – Manda Km 211.4; Sehemu ya Lusitu – Mawengi Km 50 (Maporomoko ya Udongo, Gangitoroli Km 62 – Km 64 na Jongojongo Km 82 – Km 85), ambapo kiasi cha shilingi Milioni 350 zimetumika.

Maeneo mengine ni Pamoja na Barabara ya Njombe – Makete Km 107.4 katika Maporomoko ya Udongo eneo la Mang’oto, Barabara ya Ikonda – Lupila – Mlangali Km 78.84 katika eneo lililokatika kwenye barabara na Maporomoko ya Udongo ambapo shilingi Milioni 383 zimetumika.

Pia Milioni 250 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa tuta la Barabara eneo la Ikowo katika Barabara ya Ndulamo – Nkenja – Kitulo I Km 42.28 ambao ujenzi umefikia asilimia 58 kwa gharama ya shilingi Milioni 150, Matengenezo ya eneo lililofurika kwenye Mto Rumakali na Maporomoko ya Udongo eneo la Utanziwa katika Barabara ya Kikondo – Bulongwa – Makete Km 74.2

Mhandisi Ruth amesema kuwa Milioni 359.76 zimetumika kwa ajili ya matengenezo kwenye Barabara ya Nkenja – Ikuwo – Usalimwani Km 42.70, huku Milioni 257.24 zikitumika kwa ajili ya matengenezo kwenye Barabara ya Kitulo II – Matamba – Mfumbi.

Mhandisi Ruth amesema kuwa Pamoja na Barabara hizo pia serikali imetoa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukabiliana na uharibifu wa Barabara uliotokana na mvua za El-Nino katika Barabara ya Mkoa ya Kipengele – Wangama – Kidugala – Mambegu, Pamoja na Milioni 150 zilizotolewa kwa ajili ya Barabara ya Mkoa ya Makoga – Kinenulo – Imalinyi – Mdandu pamoja na Milioni 750 zilizotumika kwa ajili ya Barabara kuu ya Makambako-Lukumburu yenye urefu wa Kilomita 139.5 eneo la Lukumburu.

Meneja huyo amesema kuwa kutokana na Athari hizo za Mvua za El Nino, barabara nyingi zilikuwa zikipitika kwa taabu na hivyo kupelekea kuidhinishiwa fedha kiasi cha shilingi billioni 3 ili kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.

Mhandisi Ruth amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 kwa ujumla Mkoa umepangiwa kiasi cha Shilingi bilioni 11.58 ili kutekeleza kazi za Matengenezo na Shilingi bilioni 3.079 kutekeleza miradi ya maendeleo. Taa zaidi ya 90 zitafungwa katika maeneo mbali mbali ya mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TANROADS.

Related Posts