MARA nyingi utasikia mchezaji wa kandanda kafunga hat-trick, yaani mabao matatu katika mchezo, lakini mashabiki wengi na hata baadhi ya waandishi wa habari za michezo hawajui asili ya hili neno hat-trick.
Mara nyingi waandishi na wachambuzi wa michezo nchini huzungumzia mchezaji kufunga ‘hat-trick’ katika kandanda na hawaendi mbali zaidi.
Tafsiri fupi inayotolewa ni kwamba hat-trick ni hupatikana pale mchezaji akitingisha nyavu mara tatu katika mchezo mmoja.
Nataka nikiri neno ‘hat-trick’ lilinipa shaka kwa muda mrefu wakati nilipokuwa naandika habari za michezo kam mashindano ya Kombe la Sunlight (baadaye Kombe la Taifa), Kombe la Gossage (sasa Chalenji) na mashindano mengine ya soka.
Hii inatokana na tafsiri tofauti zilizotolewa na waandishi wa michezo waliobobea, mashirika ya soka ya kimataifa ya michezo na wataalamu wa mchzo wa kandanda.
Wachambuzi wa kandanda wengi hupenda kueleza kuwa hili neon lilibuniwa katka nchi zao na ninakumbuka utata uliozuka juu ya ‘hat trick’ katika mkutano uliofanyika chumba cha habari cha Tanganyika Standard (sasa Daily News) katika barabara ya Maktaba, jijini Dar es Salaam mwaka 1967.
Mhariri wetu, Ken Ridley (Muingereza) alituuliza nini maana ya hat-trick. Tulikuwa watu kama 30 katika mkutano, nusu yake wazungu kutoka Uingereza, Ireland, New Zealand na Australia.
Miongoni mwao tulikuwepo waandishi wa michezo kama watano wa michezo wa hili gazeti. Pamoja na mimi walikuwepo Hadji Konde, mwandishi wa kujitegemea Chris Ndakaba na John Gardener (wote marehemu).
Kila mmoja alitoa tafsiri yake na hatimaye tulikubaliana hakuna aliyeelewa maana halisi ya neno hili na historia yake, isipokuwa tulilitumia tu kila alipotokea mchezaji kufunga mabao matatu.
Kila nilipokwenda kwenye mashindano ya kimataifa katika nchi za Kiafrka, Ulaya, Mexico na kwengineko niliwauliza waandishi wa michezo waliobobea maana ya ‘hat trick’. Kila mmoja alinipa maelezo tofauti, kama nilivyoona katika kile kikao cha ofisini.
Mnamo mwanzo wa miaka ya 2000 nilijitahidi kumaliza kiu yangu ya kuelewa maana na historia ya neno hili na nilichobaini kupitia niliyoelezewa kwa mdomo, niliposoma kwenye vitabu, niliyokuta katika mitandano na njia nyingine ni utata, hasa juu ya asili na tafsiri ya ‘hat trick’.
Wapo wanaoeleza chanzo chake ni katika mpira wa magongo kwenye uwanja wa barafu, lakini wapo wanaong’angania kuwa ilitokana na mchezo wa kriketi.
Lipo kundi linalosema chanzo chake ni katika kandanda na wengine wanadai ni kutokana na mchezo wa mpira wa kikapu.
Kila upande unayo maelezo ya kuvutia yenye tarehe na maelezo mengi kutaka kuthibitisha msimamo wao.
Hata hivyo, kwa muhtasari wengi wanasema, kama inavyoelezwa katika kitabu kiitwacho Cricketers Annual kilichoandikwa mwaka 1877 na James Lilly kuwa chanzo chake kilitokana na siku moja kwa mchezaji kuchukuwa wiketi sita kwa kurusha mipira saba.
Lakini miaka 10 kabla ya hapo neno hili ‘hat trick’ (maana yake kwa Kiswahili cha neno kwa neno ni ujanja wa kofia aina ya heti) kuelezea vitimbi alivyofanya mchawi kwa kuitupa kofia yake alipokuwa akishangilia goli.
Falsafa nyingine ni kuwa matumizi yake yalianza katika kriketi na baadaye kupokewa katika rugby na mpira wa magongo.
Kwa wanaodai matumizi yake yalianza katika kriketi wanasema neno hili lilianza kutumika mwaka 1858 kutokana na mchezaji aitwaye Stephenson alipopewa zawadi ya kofia kwa kuwatoa wachezaji watatu, mmoja baada ya mwingine kwa kuwarushia mipira mitatu na kila mmoja kugonga vile vijiti vitatu.
Stephenson alikuwa anaichezea Uingereza ilipokutana na timu ya Hallan katika Uwanja wa Hyde Park.
Wengine wanadai ilitokana na mchezo wa mpira wa magongo kwenye barafu ilipokuwa kawaida (hailezwi wakati wenyewe) kule Amerika ya Kaskazini kuona mashabiki wanavua kofia na kuzirusha uwanjani mchezaji alipofunga mabao matatu.
Vile vile yapo maelezo kuwa mfanyabiashara wa duka la kuuza kofia katika mji wa Toronto, Canada, alikuwa na kawaida katika miaka ya 1940 kumzawadia kofia mchezaji aliyefunga mabao matatu katika mchezo mmoja.
Hadithi nyengine ni ya klabu moja ya Canada ya kiwanda cha kutengenezea kofia ilipogawa kofia kwa mashabiki katika mwaka 1946 kila alipotokea mchezaji wake kufunga mabao matatu.
Vile vile upo utatanishi wa ‘hat-trick’ inapatikana vipi. Wapo wanaosema mabao yote matatu katika soka au mpira wa magongo lazima yafungwe katika kipindi kimoja, cha kwanza au cha pili na sio mawili kipindi kimoja na kipindi chengine au katika muda wa nyongeza.
Katika kriketi wengine wanasema hat-trick hupatikana katika mzunguko mmoja wa kurusha mipira sita na wengine katika mchezo mzima, uwe wa siku moja au tatu.
Katika kandanda ndio upo mkorogo. Wapo wanaosema ‘hat trick’ hupatikana kwa mchezaji kufunga mabao matatu mfululizo bila ya wapinzani kupata bao kabla hajafunga hayo mabao matatu, mfano wa hili ni kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga. Harry Kane kuna mechi amefunga hat-trick msimu uliopita, lakini ikaelezwa kwa kanuni zao hazikuwa hat-trick kwa vile mabao yake hayakufuatana mfululizo baada ya wachezaji wengine kufunga kabla hajayakamilisha mabao yote matatu.
Lakini wapo wanaodai bora tu mtu afunge mabao matatu ndani ya muda wote wa mchezo hiyo inakuwa ni hat-trick, ikiwa ni pamoja na muda wa nyongeza (extra time) au panapokuwepo mpira wa adhabu. Hili bao la mpira wa adhabu lina utata kwa kuwa wapo wanaosema linahesabika na wengine wanaosisitiza kuwa halistahiki kuhesabiwa katika kukamilisha hat-trick.
Huu mvutano katika kandanda unakwenda mbali zaidi. Lipo kundi linalosema hizi hat-trick zipo za dhahabu, fedha na shaba.
Hii ya shaba wanasema ni ya mabao matatu yaliyofungwakwa njia yoyote ile, iwe yote kwa mguu au kwa kichwa. Ile ya fedha ni mchezaji anapopata magoli mawili kwa mguu wa kulia au kushoto na moja kwa kichwa.
‘Hat trick’ ya dhahabu ni ya mchezaji kufunga bao moja kwa mguu wa kulia, jingine mguu wa kushoto na jingine kwa kichwa. Wapo walioliza je, itakuwaje kama limefungwa kwa tumbo au kifua?
Katika sakata hii ninakumbuka sokomoko alilozusha Sir Alf Ramsey mwaka 1969 ambaye alikuwa kocha wa kikosi cha Uingereza kilichobeba Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na ya pekee kwenye Uwanja wa Wembley, London, mwaka 1966.
Ramsey aliuliza: “Jee kama mchezaji atafunga bao moja kwa mguu, la pili kwa kichwa na la tatu kwa kifua itakuwa ‘hat-trick’ ya almasi?
Wapo pia waliouliza panapotokea mabao yote matatu kufungwa haraka haraka kama alivyofanya Alex Torr wa England katika Ligi ya Jumapili ya nchi hiyo kwa kutumia sekunde 70 itakuwa hat-trick ya aina gani?
Torr aliichezea timu ya Ross County ilipokutana na Narin County Novemba 28, 1964.
Uholanzi inahesabu mchezaji kupata hat-trick kama amefunga mabao yote matatu katika nusu moja ya mchezo. Bao la tatu linalofungwa Ujerumani katika muda wa nyongeza huhesabiwa, tofauti na ilivyo katika nchi nyingi za Ulaya.
Ni kawaida katika nchi nyingi mchezaji anayefunga mabao matatu katika mchezo mmoja kukabidhiwa mpira uliotumika kuuchukua nyumbani kama kumbukumbu yake.
Katika miaka ya karibuni zimekuwepo hat-trick nyingi, lakini zipo zilizohesabika kuwa za kiufundi na kutolewa mfano kama uwezo mkubwa wa wachezaji waliopata mafanikio hayo.
Miongoni mwao ni ya Syndey Leourex wa timu ya taifa ya wanawake ya Marekani wakati walipoifunga Mexico 7-0 mwezi Januari, 2013.
Dada huyu alifunga bao la kwanza kwa kichwa, la pili kwa mguu wa kulia na la tatu kwa mguu wa kushoto. Alifunga mabao yote matatu katika dakika 19 za kipindi cha kwanza.
Karibu na mpira kumalizika aliongeza bao la nne na kusema hakutaka liingie katika hesabu kwa vile alikuwa anafanya mazoezi.
Lakini kama unamtafuta mwamba wa kufunga mabao matatu katika mhezo mmoja katika siku za hivi karibuni Cristiano Ronaldo anaibuka kidedea.
Akiwa na klabu ya Real Madrid alifunga ‘hat-trick’ yake ya 19 katika Ligi ya Hispania walipocheza na klabu ya Getafe karibu miaka minane iliyopita. Bao moja lilikuwa kwa mguu wa kulia, jingine kwa mguu wa kushoto na moja kwa kichwa.
Naye Edinson Cavani wa Uruguay alifunga mabao matatu, kila mguu bao moja na jingine kwa kichwa timu akiwa na klabu ya Napoli ilipoicharaza AS Roma 4-1 katika Ligi Kuu ya Italia.
Kwa wachezaji wa Kiafrika wanaocheza Ulaya, mafanikio ya Ayegbeni Yakubu wa Nigeria katika mwaka 2007 hayasahauliki.
Mshambuliaji huyu wa Nigeria alikuwa anaichezea Everton ilipopambana na West Ham wakati ndio kwanza amehamishwa kutoka Middlesbrough. Aliyafunga mbao hayo kwa mguu wa kulia, kushoto na kichwa.
Baadaye alisema alitamani sheria ingeliruhusu kufunga bao kwa mkono.
Zipo simulizi nyingi za kuvutia juu ya hiki kinachoitwa hat-trick. Miongoni mwao ni:
– Pedro Zurita wa Argentina (alizaliwa tarehe 3, Novemba 1997) anahesabika kuwa mmoja wa mabingwa wa hat-trick.
Akiwa na klabu ya Larbatata ameweka historia ya kufunga zaidi ya mabao 1,000 na kuwa na hat-trick zaidi ya 50.
Mchezaji anayehasabika kufunga hat-trick kwa mwendo wa kasi zaidi ni Tommy Ross wa Uingereza ambaye alifariki miaka mitano iliyopita akiwa na miaka 71.
Jina lake limeingia katika kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness kutokana na kufunga mabao matatu katika kipindi cha sekunde 90 (dakika moja na nusu) wakati akiwa na miaka 18 alipokuwa akichezea jimbo la Ross lilipokutana na jimbo la Nairn katika mwaka 1964 katika mashindano ya majimbo kule Uingereza.
Ross baadaye alichezea klabu mbalimbali za England, vikiwemo Peterborough United, Wigan Athletic, Newcastle na York City na Brora Rangers ya Scotland. Katika miaka ya 1990 alikuwa mwalimu wa kandanda wa klabu mbalimbali na aliwahi pia kuwa ofisa wa kutafuta vijana wadogo wenye vipaji kwa klabu ya Tottenham Hotspur.
– Mchezaji aliyezusha gumzo la aina yake katika siku za hivi karibuni ni mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero kwa kufunga mabao matano Manchester City ilipoichapa Newcastle 6-1 katika ligi ya mwaka 2015.
Timu yake ikiwa imepachikwa bao moja mapema Sergio ambaye ni raia wa Argentina alichacharuka na kufunga mabao matano katika kipindi cha dakika 20 na kushangiliwa kwa nderemo na vifijo uwanja mzima.
Hii ni pamoja na mabao matatu mfululizo. Aguero akaungana na Andy Cole, Alan Shearer, Jermain Defoe na Dimitar England.
– Katika ligi ya Bundesliga ya Ujerumani, Robert Lewandowski wa Bayern Munich alifanya walipokutana na Wolfsburg. Akiwa amekaa katika ubao wa wachezaji wa akiba aliingizwa katika kipndi cha pili na ulipoanza mchezo tu alihangaika kila pembe ya uwanja kama kuku tembe aliyekuwa anataka kutaga.
Katika kipindi cha dakika 9 alifunga mabao matano, kati ya hayo matatu ya kwanza katika muda wa dakika nne.
Wachambuzi wa mchezo waliuliza: Hali ingekuwaje kama angekuwemo katika kikosi tangu mwanzo wa mchezo maana boli lilimkubali ile mbaya siku hiyo!
– Mchezaji mwengine aliyefanya makubwa katika suala hili ni Jimmy O’Connor wa Uingereza alipokuwa akichezea klabu ya Scotland ya Shelburne ilipopambana na Bohemians katika ligi ya Scotland mwaka 1967.
Alifunga mabao matatu katika kipndi cha dakika sekunde 13.
– Eduardo Maglioni wa Agentina alipoichezea klabu ya Independiente ilipokutana na Gimnasia La Plata, katika mwaka 1973 alifunga hat trick kwa dakika 1 na sekunde 51.
– Magnus Arvidsson wa Sweden alipoichezea klabu ya Hassleholms ilipokutana na Landskrona mwaka 1995 alifunga mabao matatu katika muda wa dakika 1 na sekunde 29.
– Alex Torr wa Uingereza wakati alipochezea Rawson Spring ilipokutana na klabu ya Winn Gardens mwaka 2013 alifunga hat trick katika kipindi cha dakika 1 na sekunde 39.
– Katika mashindano ya kimataifa Geoff Hurst wa England ndiye mchezaji pekee aliyejipatia hat-trick katika mechji ya fainali ya Kombe la Dunia 1966 ambapo England ilibeba kombe baada ya kuifunga Ujerumani Magharibi 4-2 katika mchezo wa fainali.
Kwa vyovyote vile hat trick itaendelea kuwa mada muhimu katika mchezo wa kandanda kwa miaka mingi ijayo.