Feitoto afunguka madini aliyopewa na kocha Wydad Rhulan

KIUNGO Mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema alikuwa na wakati mzuri na kocha wa Wydad Casablanca, Rhulani Mokwena ambaye amempa mbinu za kuendelea kuwa bora.

Kiungo huyo amesema amepata nafasi ya kuzungumza na kocha huyo muda mchache baada ya timu yake kupokea kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Wydad Casablanca.

“Mara baada ya mchezo kocha Mokwena aliniita na kunipongeza kwa kuniambia licha ya timu kupoteza nilikuwa na mchezo mzuri na amekuwa akinifuatiliaekutokana na kuvutiwa na aina ya uchezaji wangu” alisema na kuongeza:

“Kaniambia mimi ni mchezaji mzuri na umri wangu unaniruhusu kuendelea kuwa bora kama ntazingatia alichoniambia nikifanye na ananiona mbali kutokana na kuwa na mwendelezo mzuri wa ubora.” 

Fei Toto alisema kocha amemwambia ubora alionao sasa na nidhamu yake ya uchezaji anazidi kuwa mchezaji mkubwa na anamuona mbali sana na kwa sasa akiambiwa ataje kiungo bora wa Tanzania anaecheza Ligi Kuu Bara atamtaja yeye.

“Ameniambia mimi ni mchezaji ambaye nina uwezo wa kutengeneza mashambulizi, kukaba na naweza kutumika nafasi nyingi uwanjani kulingana na kocha atataka kunitumia kulingana na wapinzani huku akiniambia siyo mwoga wa kufanya maamuzi,” alisema.

Akizungumzia maandalizi ya msimu kwa ujumla pamoja na mchezo walioupoteza kwa idadi kubwa ya mabao, alisema maandalizi yanakwenda vizuri na mchezo wao na Wydad Casablanca ulikuwa mzuri kwao na umetoa nafasi kwa kocha kusawazisha makosa yaliyoonekana.

“Mchezo wetu na Wydad ulikuwa mzuri na wa ushindani kuna mengi tumejifunza licha ya kupoteza na naamini kipimo kizuri ni kukosea ili urekebishe makosa kabla ya mashindano, naamini kocha kaona tulipokosea anafania kazi makosa kabla ya kuanza mechi za mashindano,” alisema.

Wakati huohuo, Kocha msaidizi wa Azam FC, Bruno Ferry amesema licha ya kupoteza mchezo wa mwisho wa kirafiki kwa kuchapwa mabao 4-1 na Wydad Casablanca, lakini ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na viwango vya wachezaji wa timu hiyo.

“Kupoteza kwetu hakujatuathiri kwa sababu lengo ni kutengeneza kikosi imara cha ushindani hasa kutokana na wingi wa nyota wapya waliopo kwa sasa. Jambo zuri kama benchi la ufundi tumeridhika na kiwango cha mchezaji mmoja mmoja,” amesema. Ameongeza kuwa kwa kiasi kikubwa kambi imekuwa na manufaa wamepata mechi nzuri.

Related Posts