HATIMAYE mashindano ya Mkuu wa Majeshi ‘CDF Cup’ yametamatika juzi Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, huku JKT ikiwa mshindi wa jumla wa mashindano hayo ikitawala kwa kubeba vikombe karibu kila mchezo.
Mashindano hayo ambayo maalumu kwa ajili ya kuadhimisha miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi wa Wanachi Tanzania (JWTZ) yalikuwa kwa siku 10 ambayo ilijumuisha soka, netiboli, mpira wa mikono, wavu, shabaha, ngumi, riadha na kikapu.
JKT imechukua medali ya mshindi wa kikapu wanaume na wanawake, mshindi wa kwanza netiboli wanawake ,mshindi wa tatu mpira wa mikono wanaume na wa kwanza wanawake huku wavu wanawake na wanaume.
Kwa mchezo wa ngumi imekuwa mshindi wa pili huku shabaha wanaume nafasi ya pili na wanawake nafasi ya kwanza, mchezo wa riadha wanaume imebeba nafasi ya pili na wanawake ikikosa na soka ikiwa mshindi wa pili na wa kwanza akiwa Kamandi ya Jeshi la nchi Kavu.
Akizungumza baada ya ugawaji wa tuzo hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya CDF, Brigedia Jenerali Said Khamis Said alisema; “Ni msimu wa sita, yalikuwa na ushindani mkubwa hasa vijana wadogo, nimefarijika kuona viwango vya wachezaji na naamini haya yatakuwa maandalizi mazuri kuelekeza Septemba kwenye majeshi.”