Kikwete asimulia alivyomruhusu mkewe kugombea ubunge kishingo upande

Mchinga. Rais wa awamu ya nne nchini Tanzania, Jakaya Kikwete amesimulia namna alivyoshawishiwa na wazee 15 kutoka Jimbo la Mchinga mkoani Lindi, ili amruhusu mkewe, Salma Kikwete agombee ubunge kwenye jimbo hilo mwaka 2020.

Kikwete amesimulia kisa hicho leo Jumatano Julai 31, 2024 wakati wa mkutano mkuu wa Jimbo la Mchinga ambapo mbunge wa jimbo hilo, Mama Salma amesoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika jimbo lake.

Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye amehitimisha ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kushiriki mkutano huo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Kikwete amesema kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020, alifuatwa na wazee 15 kutoka kata zote za Jimbo la Mchinga kumwomba amruhusu mke wake, Mama Salma kugombea ubunge katika jimbo lao.

“Nilikubali kishingo upande nilipofuatwa na wazee 15 kutoka Jimbo la Mchinga. Waliniambia tunataka mkeo aje kugombea ubunge katika jimbo la Mchinga, tumechoka kuongozwa na CUF (Chama cha Wananchi).

“Nikawauliza, mmejipanga? Tusije kwenda kwenye uchaguzi mkanifedhehesha na mkamfedhehesha,” amesema Kikwete na kuelezewa na wazee hao kwamba wamejipanga na wanamhakikishia ushindi.

Basi, amesema aliporudi nyumbani alimweleza mke wake kuhusu ombi la wazee hao, Mama Salma akamwambia atakuwa tayari kama atamuunga mkono kwenye jambo hilo.

“Nilimhakikishia nitamuunga mkono na ninaendelea kumuunga mkono kwa kila shughuli anazofanya, tatizo langu, namkosa kwa muda mrefu,” amesema Kikwete huku wananchi waliohudhuria mkutano huo wakiangua vicheko.

Kikwete amemhakikishia mke wake kwamba ataendelea kumuunga mkono kwenye kazi zake, hivyo aendelee kuchapa kazi ya kuwatumikia wananchi katika jimbo lake la Mchinga na Tanzania kwa ujumla.

“Mke wangu, mbunge wa Mchinga, nakutakia kila la heri kwenye kazi zako. Endelea kufanya kazi zako, mimi nipo, nitaendelea kukuunga mkono,” amesema Rais huyo mstaafu.

Wakati akihitimishwa hotuba yake, Mama Salma amemshukuru kipekee mume wake, Kikwete, kwa msaada mkubwa anaompatika katika kutekeleza majukumu yake ya kibunge.

“Kipekee namshukuru mume wangu, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete. Yeye amekuwa nguzo yangu na mhimili wangu kwenye kazi zangu, nikichoka ananituliza,” amesema Mama Salma huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa jimbo.

Ameongeza: “Namshukuru yeye na watoto wetu na wajukuu wetu, wamekuwa msaada mkubwa kwenye kazi zangu.”

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts