Kisa migogoro, chaneta yapigwa pini kimataifa

SERIKALI imekipa kibarua Chama cha Mchezo wa Netiboli nchini (Chaneta) kutatua migogoro yao ya ndani sambamba na kufanya uchaguzi mzuri wa wachezaji wa timu ya Taifa kwa kufuata haki.

Ilisema kwa kufanya hivyo, Chaneta itapata nafasi ya kuruhusiwa kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa na kufadhiliwa na serikali, pia itawapatia wadhamini wa kudumu wa kusapoti mchezo huo.

Rai hiyo ilitolewa na Naibu Waziri mwenye dhamana ya michezo, Hamis Mohamed Mwinjuma wakati akifungua mkutano Mkuu wa Chaneta juzi jijini Arusha na kuhudhuriwa na wajumbe 76 kutoka mikoa yote 26 za Tanzania Bara.

Katika mkutano huo, Mwinjuma alisema Netiboli ni moja ya michezo mitano iliyopewa kipaumbele na serikali na inafaa kuwa mchezo namba mbili unaofanya vizuri nchini lakini kutokana na migogoro inayoendelea baina yao na kupakana matope imesababisha mchezo huo kupoteza mvuto kabisa.

“Mchezo huu umeingizwa matopeni kwelikweli na umepoteza mvuto na umaarufu wake na hii imesababisha hata kukosa wadhamini maana hakuna mtu au taasisi anataka kuwekeza fedha zake kwenye vurugu, hivyo basi, nataka moja ya ajenda zenu hapa ninyi viongozi wa juu kuhakikisha mnafanyia kazi hili na mnamaliza migogoro,” alisema Mwinjuma;

“Pia suala lingine linalowaponza ni namna dhaifu ya kuchagua timu yetu ya Taifa ya netiboli na maandalizi hafifu ambayo timu hiyo inapata, hivyo kuanzia sasa hivi tukishindwa kujiridhisha kama timu imechaguliwa kwa haki na kwa jinsi inavyofaa au imefanya maandalizi ya kutosha hatuwezi kuwaruhusu kwenda popote,” alisema Mwinjuma.

Akitoa salamu za shukrani, Makamu Mwenyekiti wa Chaneta, Shyrose Bhanji alisema wamepokea maelekezo ya Naibu waziri na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha mchezo huo unatimiza malengo yake ya kuwakilisha nchi vyema kwenye michuano ya kimataifa.

“Ni kweli yote uliyoyasema na tunaahidi baada ya mkutano huu, utapata mrejesho mzuri na tunakwenda kuanza moja dhidi ya mambo yote na zaidi tunakuahidi tutakwenda kukuletea timu bora na yenye ushindani msimu huu,” alisema Bhanji.

Amesema malengo ya Mkutano huo ni kupitia katiba ili kuiboresha iendane na mahitaji ya netiboli kwa sasa, pia watapitia taarifa za fedha na mpango mkakati wa netiboli.

Mmoja wa wadhamini wa Mkutano huo, Meneja wa Kanda ya Kaskazini kutoka Benki ya NMB, Baraka Ladislaus alisema wamesapoti mkutano huo kiasi cha Sh8 milioni ili kuwasaidia kufanikisha malengo waliojiwekea yatimie.

Related Posts