KONA YA MALOTO: Siku 3,074 za Kinana CCM na panda, shuka zake

Aprili Mosi, 2022, Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara. Nilifanikiwa kuzungumza na Kinana muda mfupi baada ya uchaguzi huo na nikamuuliza swali, kwa nini ameamua kugombea tena nafasi hiyo. Alinijibu kwa kifupi: “Nimeombwa kumsaidia mama.”

Ni kipindi ambacho Rais Samia Suluhu Hassan, alikuwa akitimiza mwaka mmoja madarakani. Akiwa ndiyo kwanza amechaguliwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa CCM. Awali, alichaguliwa katika mazingira maalum, kujaza nafasi ya mtangulizi wake, Dk John Magufuli.

Namkumbuka Kinana baada ya kuwa Makamu Mwenyekiti CCM. Sura yake ilijenga bashasha na matumaini. Aliamini Rais Samia alikuwa katikati ya vita nzito ya kimadaraka kwa sababu anuwai. Alijenga matumaini kwamba uwepo wake CCM, ungemsaidia Rais Samia kushinda kila vita.

Sisahau, muda mfupi baada ya kuwa Makamu Mwenyekiti, Kinana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Nafasi ambayo Kinana aliitumia kujenga mwafaka wa kisiasa baina ya CCM, vyama vya upinzani na dola. Kinana alikuwa mstari wa mbele kutafsiri maono ya maridhiano ya Rais Samia.

Kupitia Kinana, siasa za nchi zilipata nuru. Halafu, Rais Samia alitangaza “R4”, kama falsafa mama ya kujenga na kuimarisha siasa Tanzania. “R” ya kwanza ni Reconciliation (Maridhiano), ya pili ni Reform (Mabadiliko), tatu ni Resilience (Ustahimilivu na unyumbulifu), nne, Rebuilding (ujenzi mpya).

Ungemwona Kinana kwenye ziara za mikoani zilizotambulishwa kuwa za “kukiimarisha chama.”

Haikushangaza kwa sababu Kinana alipata kuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa miaka sita. Kipindi hicho, alidhihirisha kwamba yeye si mtu wa ofisini, bali mtindo wake ni wa kwenda “field”. Mtindo huo, kwa kiasi kikubwa ndiyo uliinusuru CCM na Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Sasa, Kinana aliporejea CCM kama Makamu Mwenyekiti, alipoanza kuingia field kuimarisha chama, ilikuwa wazi kwamba aliendelea na mtindo wake uleule.

Lakini ghafla Mkataba wa Usirikiano wa Serikali (IGA), baina ya Tanzania na Dubai, kwa ajili ya kuendesha na kuendeleza bandari za Tanzania, ukafanya nchi ifunikwe na fununu.

Moja ya fununu ilimhusu Kinana, kwamba alikuwa mmoja wa wapingaji wa ujio wa kampuni ya DP World kutoka Dubai, kuja kuendesha na kuiendeleza Bandari ya Dar es Salaam. Fununu hizo zilidai Kinana alikuwa na masilahi na mazingira ya Bandari ya Dar es Salaam, kabla ya DP World. Hakuna ushahidi uliotolewa, isipokuwa ilihojiwa: “Mbona Kinana yupo kimya, hatetei mkataba?”

Kinana alitoka, alifanya ziara akiongoza viongozi wengine mbalimbali. Ujumbe wa Kinana ulibeba hoja mbili kuu ambazo alizizungumza yeye mwenyewe. Kwanza, Kinana alisherehesha msimamo wa Serikali wa kuingia ubia na DP World ili kuongeza ufanisi wa bandari.

Pili, Kinana alizungumza kwa msisitizo: “Mimi nataka niwahakikishie Watanzania, hakuna namna, na nawasihi msiamini kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekula kiapo, eti atafanya jambo ambalo halina masilahi na nchi yake, haiwezi kutokea.”

Japo haikutosha kufuta kila kilichosemwa nyakati za fununu, lakini kwa kila mwenye afya timamu ya akili, ilimtosha kuelewa kwamba fununu za Kinana kuwa nyuma ya upingaji wa mkataba wa IGA na ujio wa DP World, hazikuwa na ujazo wowote kwenye kipimo cha ukweli.

Hata hivyo, taratibu mtindo wa Kinana kwenda field ulipungua. Ni kweli, nafasi ya Makamu Mwenyekiti CCM siyo ya utendaji, lakini kila aliyemfahamu au kumzoea Kinana wa field, aliona mabadiliko makubwa na bila shaka alishangazwa.

Julai 29, 2014, taarifa iliyosainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, ilieleza kuwa Kinana alijiuzulu Umakamu Mwenyekiti CCM, halafu Rais Samia, aliridhia kuachia kwake ngazi. Taarifa hiyo imesema, Rais Samia amekubali Kinana kuondoka kwa sababu alipomwomba awe Makamu Mwenyekiti, waliahidiana iwe kwa muda mfupi.

Baada ya waraka wa Makalla kuhusu Kinana kujiuzulu, mitandaoni ilisambaza picha yenye kumwonyesha Kinana katikati ya wanasiasa, January Makamba na Nape Nnauye. Ni picha waliyopigwa mwaka 2015, wakitembea kwa miguu kumsindikiza Magufuli kwenda ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuchukua fomu ya kugombea urais.

Ni picha yenye ujumbe usiopaswa kupuuzwa. Julai 21, 2024, ilitolewa taarifa ya Ikulu kuwa Rais Samia alitengua uteuzi wa January (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Nape (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), hivyo kuondolewa Baraza la Mawaziri. Baada ya kishindo cha wiki moja na siku moja, inatoka taarifa kwamba Rais Samia ameridhia barua ya Kinana kujiuzulu.

Inakumbusha; Machi 23, 2017, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape, aliondolewa kwenye nafasi waziri. Iliaminika sababu ya Nape kung’olewa ni msimamo wake wa kufuatilia na kutaka haki itendeke juu ya tukio la uvamizi kwenye kituo cha Clouds TV.

Machi 17, 2017, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alidaiwa kuvamia kituo cha Clouds TV na kulazimisha kurushwa hewani maudhui yaliyokataliwa na waandaaji wa kipindi cha Shilawadu pamoja na wamiliki wa kituo. Tukio hilo lilitikisa mno lakini Magufuli akiwa Rais, alitoa msimamo kuwa Makonda aachwe afanye kazi.

Kitendo cha kuvuliwa uwaziri Nape, kiliibua minong’ono kuwa Kinana alikasirishwa na uamuzi huo, hivyo akaamua kususa. Yapo maneno yalinong’onwa kwamba Kinana alikuwa ameachia ngazi na kwamba alikuwa haingii kabisa kwenye ofisi yake ya Katibu Mkuu CCM. Ikavumishwa pia kuwa hakuwa akijulikana alipo.

Magufuli akiwa Rais, vilevile Mwenyekiti wa CCM, alilazimika kutoa ufafanuzi kuwa Kinana alikuwa nje ya nchi kwa matibabu kwa ruhusa aliyompa. Pamoja na kufafanua hilo la Kinana kutoonekana, bado haikuwezekana kutuliza minong’ono.

Hatimaye, Mei 28, 2018, Kinana, aliandika barua ya kujiuzulu ukatibu mkuu wa CCM. Magufuli aliridhia kuondoka kwake. Akasema Kinana alishaomba sana kuondoka, yeye akawa anamlazimisha. Kisha, Aprili Mosi, 2022, Kinana alirejea kwenye chama, akiwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.

Piga hesabu. Kutoka Mei 28, 2018 mpaka Aprili Mosi, 2022 ni miaka mitatu, miezi 10 na siku nne. Yaani siku 1,404. Huo ndiyo muda ambao Kinana alikuwa nje ya CCM. Halafu, kutoka Aprili Mosi, 2022 hadi Agosti 29, 2024, ni miaka miwili na miezi mitano kasoro siku mbili (siku 882). Huo ni muda wa Kinana aliotumikia Umakamu Mwenyekiti CCM, Tanzania Bara.

Miaka sita ambayo Kinana alitumikia Ukatibu Mkuu CCM, inaleta jumla siku 2,192. Endapo utajumlisha na siku 882 za Umakamu Mwenyekiti CCM, utapata jumla ya siku 3,074 za Kinana, kukihudumia chama chake katika nafasi za juu kabisa.

Julai 2016, kuelekea mkutano mkuu maalum wa CCM uliomchagua Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama, Kinana alijitokeza na kutangaza kusudio lake la kuachia ngazi. Alisema hata nafasi yenyewe aliishika kwa ombi la wazee, ila hayakuwa mapenzi yake.

Wakati wa mkutano mkuu, Rais Magufuli aliikataa barua ya Kinana na kumtaka aendelee kushika nafasi ya katibu mkuu.

Kinana alipokuwa akielezea alivyoafikia uamuzi wa kuendelea na nafasi hiyo, alisema alipokea kijiti cha ukatibu mkuu kutoka kwa mtangulizi wake, Wilson Mukama baada ya kuombwa mara nyingi na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Kwa maneno yake mwenyewe, alisema: “Niliona si heshima kumkatalia Rais wa nchi.” Kauli hiyo inadhihirisha kuwa hata Rais Magufuli alipoikataa barua yake ya kuomba kuachia ngazi, alikubali kwa sababu aliyemkatalia kujiuzulu ni Rais.

Kikwete pia alipata kuelezea safari ya kumshawishi Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM, kwamba kila mara alipomwomba alikataa. Kabla ya Yusuf Makamba kuwa katibu mkuu, alipeleka ombi kwa Kinana akakataa. Mwaka 2012 baada ya Mukama, Kikwete alisema alimwambia Kinana kuwa safari hii hakuwa na namna zaidi ya kukubali ili kukiokoa chama.

Hivyo basi, suala kwamba Kinana hakuwa akitaka awe Katibu Mkuu CCM halibishaniwi. Maana limezungumzwa mara kadhaa na yeye mwenyewe, kisha Kikwete alilitolea ufafanuzi mzuri. Huo ni uthibitisho tosha kuwa majukumu aliyopewa kwa imani kubwa kuwa angeyaweza, yeye hakuyataka.

Kurejea alipokubali kuwa Katibu Mkuu haikutokana na ushawishi wa Kikwete peke yake, kwa kuwa Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na wa tatu, Benjamin Mkapa, waliungana kumshawishi na kumshinikiza akubali.

Kisha tena, alikubali kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa kuombwa na Rais Samia, vilevile kwa ushawishi wa wazee wengine wa chama, akiwemo Dk Kikwete.

Hiyo inatoa tafsiri kwamba Kinana ana kitu kikubwa ambacho wengi hukiona. Huombwa kukisaidia chama katika nyakati ngumu, halafu huondoka kwa kujiuzulu.

Kinana; hata Rais Mwinyi alipokuwa madarakani, alipata kumwomba Kinana awe Katibu Mkuu CCM. Kipindi hicho Kinana akiwa Waziri wa Ulinzi. Hata hivyo, Kinana alimwangukia Rais Mwinyi asimpe nafasi hiyo kwa sababu alikuwa bado kijana. Mzee Mwinyi alimwelewa.

Inaleta mantiki kuwa Kinana ni hazina ya CCM, inayotumainiwa mno kipindi chama kinapopitia nyakati ngumu. Hukubali pale ambapo huona hana budi kukubali. Huitenda kazi yake, halafu yeye mwenyewe kuomba kuondoka.

Mwaka 2018, kipindi Kinana alipoachia Ukatibu Mkuu CCM, ilikuwa wazi hakuwa mwenye furaha chini ya Magufuli. Hata hivyo, wakati wa sasa, maswali ni mengi yanayozuka, kutokana na jinsi alivyoingia kwa matumaini makubwa, lakini ameondoka ghafla.

Kilichomkwaza ni January na Nape kuenguliwa kama inavyonong’onwa mitandaoni? Inawezekanaje? Taarifa ya January na Nape kutenguliwa uwaziri ilitoka Julai 21, 2024. Siku iliyofuata, Julai 22, 2024, Kinana alikuwepo ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, akifanya kazi kama vile hakikutokea kitu.

Je, ndani ya Kinana kulikuwa na kitu endelevu au kuna vuguvugu la chinichini baina yake na Rais Samia, ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM? Isipuuzwe, baada ya January na Nape kuondolewa uwaziri, wapo watu walisema mitandaoni kuwa Rais Samia aliamua kujitenga na wapinzani wake.

Wasiwasi mkubwa ni urais mwaka 2025. Yanasikika maneno kuwa Kinana na Kikwete, wanamwandaa January kuwa Rais uchaguzi ujao. Kinana na January kwa nyakati tofauti, walishajitokeza hadharani kumuunga mkono Rais Samia kuendelea muhula wa pili. Hata Kikwete, alipata kusema, hakuna wa kumzidi Samia 2025, labda mambo yaharibike sana.

Je, kama ni wasiwasi wa urais 2025, unatokea wapi? Au mambo ndiyo yameshaharibika sana kama alivyosema Kikwete? Zipo taarifa kwamba ndani ya CCM kuna uchonganishi mkubwa, lakini shabaha ni kuwaondolea baadhi ya watu nguvu kuelekea Uchaguzi Mkuu 2030. Wanawachonganisha na Rais Samia ili awapige rungu, wadhoofike mapema. Ikifika 2030 wawe hoi.

Related Posts