KONA YA MALOTO: Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024 kudhihirisha 4R za Rais Samia

Wananchi hawakuitikia vizuri wito wa kujiandikisha kwenye daftari la mpigakura, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Novemba 2019. Hii inapaswa kujenga tahadhari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Septemba 2024.

Kama swali litakuwa ni kuhoji kwa nini mwitikio ulikuwa mdogo, jibu linatakiwa liwe na macho ya namna uchaguzi hufanyika na mazingira yake. Jicho la kwanza liwe na tafsiri kuhusu uchaguzi. Mmiliki wake ni nani? Jibu ndiyo mwamuzi wa itakavyokuwa Septemba 2024.

Kuna tafsiri mbili. Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, amepata kusema: “Uchaguzi ni mali ya wananchi. Kama wao wenyewe wataamua kukalia moto, waachwe, kwani ni wao wenyewe watakaolazimika kukaa kwa makalio yenye majeraha ya moto.”

Tafsiri ya Lincoln ilikuwa kuwaacha wananchi wenyewe kuamua. Endapo watafanya uchaguzi mbaya na kujiingiza kwenye janga, madhara ya kuchagua vibaya watayapata wenyewe.

Ipo tafsiri ya pili, ya Kiongozi wa Urusi na Soviet kwa miaka 31, Joseph Stalin, aliyesema: “Jukumu la mwananchi ni kupiga kura na kuondoka, suala la nani atatangazwa mshindi, hilo haliwahusu wananchi.”

Stalin alifikisha ujumbe kuwa mwananchi hutumika kama kiini macho cha uchaguzi, lakini wenye mamlaka ya kuamua mshindi ni wanasiasa. Kwamba kura zipigwe, mtu apate idadi kubwa kiasi gani, lakini yupo mtu au kikundi cha watu wachache huamua vinginevyo.

Tafsiri ya Lincoln ni kuwa uchaguzi ni mali ya wananchi na hawapaswi kudhulumiwa. Ina maana kuwa mwananchi mwenyewe anakuwa anajisikia mwamuzi, kwamba kura yake itaamua mabadiliko au kuubakisha utawala unaokuwepo.

Stalin anasema kuwa mwananchi asijidanganye kwamba kura yake itafanya mabadiliko au itaamua chochote. Yeye ni mtumwa tu wa kupanga foleni katika jua kali, lakini atakachokiamua, hakitazingatiwa na wenye mamlaka.

Katika nchi ambayo maneno ya Lincoln yanaheshimika, wananchi wanajiona ndiyo wenye haki ya kuamua, na wanajihisi waamuzi ndani ya nyoyo zao, huwezi kuwapigia kelele kujiandikisha. Muda ukifika watakimbilia vituoni ili wafanye uamuzi.

Uchaguzi ni alama kuu ya matumaini kwa mwananchi baada ya oksijeni. Ikiwa anavuta hewa safi na anao uhakika wa kumwondoa au kumweka madarakani kiongozi wake, angalau hujiona yupo kwenye tabaka la maisha ndani ya mamlaka yake. Na hiyo ndio demokrasia. Wanasiasa wanatakiwa kufahamu fika kuwa kama ambavyo wao hupenda mamlaka ya kuongoza na kuwakilisha, ndivyo na wananchi wanavyohusudu mamlaka ya kuamua nani awe kiongozi wao na yupi asiwe.

Na kwa wanasiasa, halipaswi kuwa ombi, bali lazima. Kuyaacha mamlaka ya kuchagua ndani ya matakwa ya wananchi. Wasisaidiwe, waachwe wenyewe. Kama wataamua kukalia moto, ni wao wataungua. Wakishaungua, watajifunza kutorudia makosa.

Kwa kurejea kusuasua kujiandikisha kwenye daftari la mpigakura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, swali la kujiuliza ni je, nyakati za sasa kupitia uchaguzi ambao umekuwa ukifanyika, hasa uchaguzi mdogo, Tanzania inaheshimu Tafsiri ya Lincoln au inakumbatia maneno ya Stalin?

Mwaka 2019, Rais alikuwa Dk John Magufuli, sasa nchi ipo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Mabadiliko ni makubwa. Mtindo wa uongozi wa Rais Samia, hauna mfanano wowote na ule wa Magufuli.

Hivyo, haitarajiwi matukio ya mwaka 2019, yarejee 2024.

Hata hivyo, lipo kosa la kimsingi linaendelezwa. Ukifanya mapitio ya rasimu za kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024. Rasimu zote vinne. Kanuni ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo na Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa. Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mtaa katika Mamlaka ya Wilaya na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali katika Mamlaka za Miji. Zote hizo, kanuni zinaelekeza kuwa mamlaka ya uchaguzi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Mwaka 2019, yalitokea madhila mengi. Vyama vya upinzani, Chadema na ACT-Wazalendo, vilisusia uchaguzi. Ni baada ya wagombea wao kwa zaidi ya asilimia 95 kuenguliwa kwa sababu mbalimbali. Maeneo mengine, wasimamizi wa uchaguzi walizikimbia ofisi ili wafombea wa upinzani wasifanikiwe kurejesha fomu hadi muda upite. Kitendo cha kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, kuendelea kumtaja Waziri wa Tamisemi, mwanasiasa na mwanachama wa CCM, kuwa msimamizi wa uchaguzi unaokutanisha vyama vingine, vinavyoshindana na chake, dhahiri nchi bado ipo kulekule. Haijabadilika.

Aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally, ambaye ni Karibu Mkuu Kiongozi aliyedumu kwa muda mfupi zaidi katika historia ya Tanzania, alipata kuzungumzia nidhamu ya Watanzania kujiandikisha na kupiga kura. Nukuu hiyo ipo kwenye video ambayo ilipata kusambaa mno mitandaoni. Bashiru anasema: “Kuna wale ambao naweza kuwaita ni wajanja, wapigakura wa Tanzania, ambao wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani kwa sababu wanaona uchaguzi ni kituko, wanaona ni mchezo wa kuigiza, na ndiyo maana leo kupata watu kuhudhuria kwenye kupiga kura imekuwa shida. Kote tunaposhinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40.” Nukuu ya Bashiru inaundwa na mantiki kuwa Watanzania zaidi ya asilimia 60 hawana matumaini na uchaguzi. Hivyo, huwa hawaoni umuhimu wa kujiandikisha wala kupiga kura.

Rasimu za kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, hazishawishi wananchi kuona uchaguzi ni mali yao. Zaidi, haziendi usawa mmoja na falasa ya “R 4”, ambayo ndiyo Rais Samia alieleza ataitumia kuendesha siasa nchini. Umebaki mwezi mmoja, kufikia Septemba ambao ndiyo mwezi wa uchaguzi. Ni mwezi wa kuamua kuwa 2024, Tanzania itafuata mwongozo wa Lincoln au Stalin. Je, “R 4” zitadhihirika. Watanzania wataanza kuamini uchaguzi au wataendelea kuona kituko? Zaidi, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, utadhihirisha sura ya Samia na pale anaposimamia.

Related Posts