Madiwani wawili wa upinzani Mchinga watimkia CCM

Mchinga. Madiwani wawili kutoka Kata za Milola na Rutamba zilizopo katika Jimbo la Mchinga mkoani Lindi, wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuvutiwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na unaofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Madiwani hao ni Hussen Kimbyoko kutoka Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na Athumani Mmaije kutoka ACT Wazalendo ambao walikuwa madiwani pekee kutoka upinzani katika jimbo hilo lenye kata 11.

Madiwani hao pamoja na wengine 60 kutoka upinzani, wamepokewa leo Jumatano Julai 31, 224 kwenye mkutano wa Jimbo la Mchinga ulioandaliwa na mbunge wa jimbo hilo, Salma Kikwete, mgeni rasmi akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Madiwani hao wanajiunga CCM ikiwa ni siku moja imepita tangu aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo 2015-2020 kupitia CUF, Hamidu Bobali ambaye baadaye alijiunga na ACT-Wazalendo kutangaza kuhamia CCM.

Bobali na wanachama wengine zaidi ya 250 walitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara wa Dk Nchimbi uliofanyikia Lindi Mjini.

Katika mkutano huo, Mama Salma amewasilisha taarifa yake ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika jimbo lake huku wakifanikiwa kuzikomboa kata mbili zilizokuwa chini ya upinzani tangu uchaguzi wa mwaka 2020.

Wakizungumza baada ya kupokelewa kwenye chama chao kipya, madiwani hao wamesema hawawezi kusifia maendeleo yanayofanywa na CCM wakiwa kwenye upande wa pili, hivyo wameamua kujiunga na CCM na wamebainisha hawajali kama watakuwa wamepoteza sifa ya uongozi pamoja na maslahi yao.

Aliyekuwa diwani wa Rutamba, Mmaije amesema haoni sababu ya kubaki kwenye chama chake cha awali ikiwa lengo ni kupata maendeleo na yamepatikana.

“Nimehamia CCM kwa sababu ya kufuata maendeleo, kuna kijiji kama cha Michee hapakuwa na shule lakini sasa kuna shule. Rutamba pia hapakuwa na shule na sasa kuna shule. Kwa hiyo, sababu kubwa iliyonifanya nihame ni maendeleo na maendeleo wananchi wangu wameyaona,” amesema Mmaije.

Mbali na shule hizo, amesema zimejengwa zahanati na hata visima vya maji vimepatikana.

“Kwenye chama nilichotoka hakuna pigo bali kuna ajenda za matukio na ndizo zilizonifanya nihame chama kwa sababu ajenda hizo hazina tija,” amesema Mmaije.

Kwa upande wake, aliyekuwa diwani wa Kata ya Milola, Kimbyoko amesema ameamua kuhamia CCM kutokana na kasi ya maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Rais Samia pamoja na ushirikiano alioupata kutoka kwa mbunge wa Mchinga, Mama Salma.

“Tangu kata ya Milola imeanzishwa, hakuna mwaka tumepata maendelea kama mwaka huu, kwa hiyo sababu ya kutoka CUF ni juhudi zinazofanywa na kata yetu imepata maendeleo. Hivyo, kwanini niendelee kukaa kwenye chama tofauti na CCM,”amehoji Kibyoko.

Kimbyoko amesema kwenye kata yake hakuna wanachama wengi wa CUF na kampeni zake zilikuwa zinafanywa usiku na wanaCCM na baada ya kupata walimwambia akae madarakani kwa miaka kama mitatu kisha arudi CCM, jambo ambalo amelifanya leo.

Related Posts