Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kuweka mikakati itakayosaidia kuwabaini wanaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidhi ya watoto ukiwemo utekaji, ili kutokomeza matukio yanayoendelea nchini.
Ushauri huo unatolewa katika kipindi ambacho, kumeripotiwa matukio kadhaa ya madai ya kutekwa na kutoweka kwa watoto nchini.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alikiri kuwepo kwa matukio hayo, akifafanua wingi unaoripotiwa ni tofauti na uhalisia wa idadi yake.
Pia, Waziri Masauni alieleza mikakati ya Serikali ya kukabiliana na vitendo hivyo imefanya maboresho ya mifumo na mikakati ya kuyakabili.
Amesema kinachofanywa sasa ni kuboresha mifumo na taratibu za kukabili vitendo hivyo na sio kutumia mbinu za kale. Ameeleza uboreshaji huo, unahusisha kuja na mbinu mpya na za kisasa zitakazoendana na wakati uliopo.
Leo, Jumatano Julai 31, 2024 mwanazuoni kutoka Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Chris Peter Maina ametoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kisheria watetezi wa haki za watoto na kueleza kinachopaswa kufanyika.
Amesema kuendelea kwa matukio hayo dhidi ya watoto kunaongeza hofu kwa jamii, hivyo mikakati ya kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo itasaidia kuondoa wasiwasi uliopo.
“Watu hawaheshimu sheria, hawalei watoto wao vizuri sasa hivi kuna wimbi la watoto kupotea, wengine wanauawa na kukutwa baadhi ya viungo hawana.
“Serikali ikiweka mikakati ya kuwabaini wahusika wa vitendo hivi itasaidia kuondoa ukatili unaoendelea kufanyika nchini,” amesema.
Tatizo lililopo, amesema watoto hawalindwi, hawapendwi na hawataki kuiheshimu jamii inayowazunguka wakiwemo wazazi au walezi.
Akizungumzia dhamira ya mafunzo hayo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema wanalenga kujenga uwezo katika sheria na mifumo ya ulinzi na utetezi wa haki za binadamu kikanda na kimataifa.
Olengurumwa amesema lengo ni kuboresha hasa kipindi ambacho kuna wimbi la ukatili na ukiukwaji wa haki za watoto.
“Tumeona taarifa za polisi zinasema masuala ya ulawiti, ubakaji yanaongezeka kama kupotea na utekaji, watetezi wa haki za watoto wakipata mafunzo tunaamini kazi ya utetezi itaboreka zaidi hasa kule walipo wengi wao wanatoka shuleni.
“Leo tumewaleta watetezi wanaowatetea watoto kutoka mikoa sita ya Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Mtwara na Lindi,” amesema Olengurumwa.
Amesema taasisi za ustawi wa jamii ndiyo walinzi wa watoto katika ngazi ya Kata, lakini wengi hawaelewi sheria na mifumo hivyo wanatakiwa wajengewe uwezo ili watimize wajibu wao.
Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Mashirika ya Watoto, Ombeni Kimaro amewataka wazazi kuhakikisha wanawapa elimu watoto wao ili inapotokea changamoto ya ukatili watoe taarifa kunakohusika.