Mfuko wa Wakfu wa Benjamin Mkapa watanuka

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF), Dk Adeline Kimambo amesema Mfuko wa Wakfu (Endowment Fund) wa taasisi hiyo umetanuka kutoka Sh1 bilioni mwaka 2022 hadi kufikia Sh2.3 bilioni mwaka 2024.

Dk Kimambo amesema hayo leo Jumatano, Julai 31, 2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya tatu ya kumbukizi ya hayati Benjamin Mkapa, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Julai mwaka 2021 Rais (Samia Suluhu Hassan) ulituzindulia rasmi mfuko wa wakfu wakati tunaadhimisha kumbukumbu ya hayati Mkapa, ikiwa ni dhana ya kuendelea kujizatiti na kuongeza nguvu za uendelevu wa ndani.  Napenda kuwataarifu kwamba, mfuko huu umeongezeka kutoka Sh1 bilioni mwaka 2022, hadi kufikia Sh2.3 bilioni Juni 2024,” amesema.

Dk Kimambo amesema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na juhudi za msarifu, bodi ya wadhamini na menejimenti ya BMF, akishukuru kwa mchango wa awali uliotolewa na Serikali wa Sh100 milioni kwenye mfuko huo.

Amesema wamesimamia utekelezaji wa mpango mkakati wa tatu wa taasisi hiyo wa miaka mitano, kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2024, uliogharimu Sh156 bilioni.

“Tunafarijika kuona tumefanikiwa kutekeleza mpango mkakati huu kwa takribani Sh157 bilioni, ambayo ni sawa na asilimia 101 kwa miaka mitano, hivyo kuwafikia wanufaika takribani milioni 11 Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro amesema katika kumbukizi ya kiongozi huyo inayofanyika kwa mara tatu, wamezindua mkakati wa taasisi unaoanza mwaka 2024 mpaka 2030.

Amesema wakati wanaandaa mkakati huo, bodi ilijiuliza suala gani ambalo hayati Mkapa angetaka kushawishiwa kufanya katika mpango ujao, hivyo waliona kuna ulazima wa kuhusisha mkakati wa nguvu kazi ya afya.

“Ndiyo sababu kumbukizi ya mwaka huu tunazungumzia rasilimali watu. Programu ya kuandaa wataalamu wa afya na kujenga nyumba za wataalamu ilikuwa miongoni mwa programu za awali, kinachotutia moyo ni jitihada za Serikali kuchukua hatua,” amesema.

Dk Ellen amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo miaka 18 iliyopita, wataalamu wa afya 1,150 wamesomeshwa.

“Taasisi imeweza kutoa ajira takriban 13,000 katika sekta ya afya ambayo inajumuisha wataalamu wa afya wajulikano Mkapa Fellows takribani 7,000 na wahudumu ngazi ya jamii 6,000,” amesema.

Amesema wametekeleza miradi ya majaribio ya wataalamu wa afya ngazi ya jamii na matokeo yake yalichangia Serikali kuchukua hatua ya kuajiri watoa huduma ngazi ya jamii.

Akisoma risala kwa niaba ya familia ya Mkapa, William Erio amemshukuru Rais Samia kwa kuwapo mara tatu mfululizo katika kumbukizi hiyo.

“Familia inatambua kuwa mwaka jana haikuwa na shughuli kama hii lakini kwa upendo ulio nao hukutaka mwaka uishe hivihivi, ulizuru kaburi lake Lupaso kutoa heshima, pia tunashukuru kwa jinsi unavyoendelea kumtunza mjane wa Mkapa na jinsi unavyoangalia familia kwa ujumla, tukiwemo sisi vijana wake kama unavyoona bado mama yake anang’ara na kupendeza hili ni jukumu lako,” amesema.

Erio pia amemshukuru Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuwa msarifu na kuilea Taasisi ya Benjamin Mkapa inayoendeleza maono ya muasisi huyo.

“Asante kwa upendo wako ulitwambia mwaka 2021 pale Mlimani City, huna hakika kama unaweza kuvaa viatu vyake, lakini tuliyoyasikia leo na tunayoendelea kuyasikia ni wazi kuwa si tu utaweza kuvivaa lakini viatu hivi vitakubana, tunakushkuru sana kama familia,” amesema.

Akizungumzia hilo, Rais Samia amesema ubunifu wa BMF umeilazimisha Serikali kutengeneza kada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Amesema Serikali imeanzisha kada hiyo mpya katika utumishi wa umma kwa kuajiri watumishi hao 137,000.

Related Posts