SIMBA imekamilisha ‘pre-season’ Misri baada ya kuwa huko kwa wiki tatu na leo Jumatano imerejea Dar kumalizia maandalizi ya mwisho kabla ya Simba Day Jumamosi na msimu mpya utakaoanza Agosti 8 kwa kucheza Ngao ya Jamii.
Katika wiki tatu ilizokaa Misri, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Fadlu Davids amekiona kikosi baada ya kucheza mechi tatu za kirafiki na kushinda zote.
Licha ya kupata ushindi katika mechi hizo, lakini kocha huyo hajafurahishwa na namna safu yake ya ushambuliaji ilivyokuwa inapoteza nafasi nyingi za kufunga.
Msala huo umewaangukia wachezaji wa eneo hilo yakiwemo majembe mapya Joshua Mutale na Steven Mukwale.
Simba ilianza kucheza na Canal SC ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0, kisha ikashinda 2-1 dhidi ya Telecom Egypt na kumaliziia dhidi ya Al-Adalah FC kwa ushindi wa mabao 2-1.
Mbali na Mutale na Mukwala, Valentino Mashaka na Freddy Michael nao ni washambuliaji wa timu hiyo inayopambana kurejesha heshima katika ligi baada ya kukosa taji la Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo.
Akizungumzia hali ya kikosi, Fadlu alisema ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha hakipotezi nafasi nyingi kinazotengeneza ili kuweza kushinda kwa idadi kubwa ya mabao na siyo kama ilivyo sasa.
Fadlu alisema ni hatua nzuri aliyopo sasa kwani wachezaji licha ya kukosa nafasi wamekuwa wakikaa kwenye nafasi huku kuwa ndani ya boksi wachezaji wamekuwa wakiingia wengi hivyo wameanza kuingia kwenye mfumo wake.
“Timu imeimarika kila eneo na wachezaji tayari wameanza kuingia kwenye mfumo shida ya kutofunga ni sehemu ndogo ambayo inaweza kuisha kwa muda mfupi kwani wachezaji wamekuwa wakijitega vizuri kwenye nafasi,” alisema.
Akizungumzia kikosi chao, Mutale alisema walikuwa na muda mzuri Misri kujiweka sawa tayari kwa msimu mpya huku akidai kuwa wamejengeka kimwili na kiushindani.
Alisema wamepata utimamu wa mwili vizuri na wapo tayari kwa kushindana huku akifurahia namna wachezaji wenzake walivyo na muunganiko mzuri.
Naye Mukwala alisema walikuwa na maandalizi mazuri na ameona namna wachezaji wenzake walivyokuwa wanapambana kusaka nafasi kikosi cha kwanza.
“Kwa upande wetu kama wachezaji tunafikiri kuna kitu tumeongeza hasa kwenye mechi tatu tulizocheza, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona timu yao Jumamosi katika Simba Day, nawaahidi kuwa watafurahi,” alisema.
Katika mechi tatu walizocheza Simba wakiwa Misri, wamefunga mabao saba na kuruhusu mawili. Wafungaji wao ni Mutale, Mukwala, Mashaka, Ladack Chasambi, Augustine Okejepha na Charles Ahoua aliyepiga mbili