Mwili wa mwanamke wakutwa ukielea bwawani

Songwe. Mwili wa mwanamke mmoja ambaye hajafahamika, umekutwa ukielea katika Bwawa la Mbimba, linalotumika kwa shughuli za umwagiliaji kando ya Barabara ya Tanzania – Zambia wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe.

Mwili huo umekutwa umeharibika na uliopolewa jana Jumanne Julai 30, 2024 jioni na haijulikani mwili huo kama umetupwa au mtu huyo alitumbukia mwenyewe bwawani humo.

“Baada ya kuuona, wananchi walitoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Songwe ambao walifika na kuuopoa,” amesema Baka Mwangosi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbimba alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusiana na tukio hilo leo Jumatano Julai 31, 2024.

Mwangosi ameliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika eneo hilo kwa kushirikiana na wananchi.

“Hatujui kama huyu mtu alitumbukia mwenyewe kwenye hili bwawa au kuna watu wamemtumbukiza, bado ni kitendawili,” amesema Mwangosi.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Songwe, Joseph Kapange amesema walipokea taarifa hizo jana jioni kutoka kwa wananchi.

Amesema walipofika eneo la tukio, walibaini mwili huo ni wa mwanamke na ulikuwa umeharibika mdomoni.

Hata hivyo, amesema hili ni tukio la pili kutokea katika bwawa hilo, “Mwaka jana pia tuliopoa mwili wa mwanamke mwingine ambaye pia haikujulikana ni mkazi wa wapi na hata wenyeji wa hapa hakuna aliyekuwa anamfahamu.”

Mmoja wa mashuhuda na mkazi wa Mbimba, Joseph Mwazembe amesema tukio hilo limewashtua na linaibua hofu kwa wananchi.

“Mwaka jana pia kuna maiti ya mwanamke ilitolewa kwenye bwawa hili, sasa hii inaleta maswali halafu siyo watu wanaoishi hapa kwa sababu hata huyo wa mwaka jana maiti yake haikutambuliwa na sijui ilizikwa na Serikali au ndugu zake walipatikana hakuna anayejua,” amesema Mwazembe.

Naye Mariam Hamis amesema kuna haja sasa ya wananchi nao kulilinda bwawa hili.

“Hii ni maiti ya pili sasa, Serikali nayo itusaidie kulitazama hili, hatutaki kuona bwawa hili sasa linatumika kama eneo la kutupa miili ya watu,” amesema hamis.

Kapange amesema mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na ametoa wito kwa wananchi ambao wamepotelewa na ndugu kufika hospitalini hapo kuutambua mwili huo kama ni wa ndugu yao.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts