KAMA ulikuwa unajua kuwa mchezaji wa kike akibeba ujauzito na kujifungua kiwango chake kinashuka uwanjani basi sio kweli ni wewe mwenyewe tu juhudi zako mazoezini.
Hilo analithibitisha Golikipa wa Baobab Queens, Jeanne Pauline Umuhoza (33), raia wa Rwanda ambaye baada ya kupata mtoto alirudi kiwanjani na kukiwasha kama ilivyo awali.
“Wengine wanakuwa wavivu ti lakini kama unazingatia mazoezi ya Kocha mbona unarudi taratibu kwenye hali yako ya kawaida na unakuwa bora kama ulivyo mwanzo,” anasema kipa huyo ambaye aliwahi kuichezea Simba Queens mwaka 2020.
Pauline anasema mtoto wake alimzaa mwaka 2009 na wala haikumpa shida kwani akienda uwanjani anakwenda akiwaachia benchi la ufundi.
“Kwanza mimi sikupanga kuwa na mtoto lakini ilitokea nikapata ujauzito na nashukuru sikupata tabu, nikienda uwanjani nilikuwa nawaachia makocha wakae nae,” anasema na kuongeza
“Kuna muda kama naona muda umeenda sana na mwanangu hajanyonya naomba mwamuzi dakika kadhaa namnyonyesha kisha namrudisha naendelea kucheza,”
“Na huwezi kuamini watu wanasema mtoto wa kike akizaa na kurudi uwanjani kiwango kinashuka mimi kwangu ilikuwa tofauti kwani sikuona mabadiliko yoyote ukizingatia mazoezi kila kitu kinarudi fresh.”
Kipa huyo anasema ameona matunda ya kuwa na mtoto kwani anajivunia yeye na hajutii.
“Naweza kumtuma mwanangu kaninunulie kitu fulani lakini kama nisingekuwa na mtoto ingekuwaje, nampenda sana na natamani kuzaa tena mwingine lakini kama ningeulizwa jinsia gani basi ni mwanamke,” anasema mchezaji huyo ambaye kwa asilimia kubwa soka ndio lilimuendeshea maisha yake hususani kusomesha mtoto wake
Kipa huyo alicheza Baobab kwa misimu mitatu alipojiunga nao mwaka 2021 akitokea Simba Queens ambako alichukua ubingwa wa ligi.
“Baobab waliniona nikiwa Simba ambako msimu wa 2020 tulichukua ubingwa hivyo ikawa njia rahisi ya kusajiliwa, nikacheza misimu miwili na huu mmoja nilikuwa nje nikiuguza majeraha ya goti,” anasema na kuongeza
“Ligi ya Tanzania naifahamu vyema kwani kabla ya Simba na Baobab niliichezea Kigoma Sisters mwaka 2019/20 kwahiyo nimehudumu WPL misimu mitano sasa,”
Pauline anasema alianza kucheza ligi msimu wa 2006 akicheza timu mbalimbali za Rwanda wakati huo akicheza beki wa kati na sio golikipa.
“Nilicheza ligi Rwanda nikaitumikia pia APR, nikatoka na kuchezea timu za Burundi ambapo nilikutana na Joelle Bukuru, Asha Djafar (Simba Queens), Uganda na Congo.”
Baobab Queens ni miongoni mwa timu mbili zilizoshuka daraja msimu uliopita kwa idadi kubwa ya mabao ya kufungwa ikiruhusu 45 na kipa huyo anaeleza sababu zilizoishusha timu hiyo.
Anasema sababu mojawapo ya timu kufanya vizuri ni kutokana na utimamu, hali nzuri ya wachezaji, mawasiliano mazuri kati ya viongozi na wachezaji lakini pia malipo mazuri.
Anaongeza kuwa hawakuwa na msimu mzuri wa ligi kwani kwenye mechi 18 timu hiyo imeshinda mitatu, sare nne na kupoteza mechi 11.
“Tunaweza kusema ligi ya wanawake inakuwa lakini bado kuna vitu ni changamoto ambavyo vinaididimiza ligi hiyo mfano timu hizi ndogo hata posho inakuwa shida hata chakula nacho changamoto hivyo wachezaji hawawezi kucheza na njaa,” anasema
Kwa Simba,Yanga, JKT au Fountain Gate Princess anasema ni taasisi ambazo zinajitegemea hata kama hazina mdhamini ndio maana wanapafomu vizuri.
Hadi ligi inaisha mwezi uliopita, Mwanaspoti linafahamu kuna baadhi ya wachezaji hawakulipwa mishahara zaidi ya miezi mitatu.
Kipa huyo anasema bado anaidai klabu hiyo mshahara wa miezi mitatu lakini kama ilivyo kwa wachezaji wengine walipatiwa fedha ya usafiri wa kurudi makwao.
“Mimi pia nilikumbana na changamoto hiyo, na hadi leo tangu tukae kambini kuanzia Septemba mwaka jana hadi June unakuta miezi mitatu minne hujapewa mshahara wako na hapo familia inakutegemea wengine tuna watoto wanahitaji kuhudumiwa,”
“N tulijaribu kuzungumza na mwenye timu lakini haikufua dafu, mimi kwa upande wangu nikaona bora nirudi zangu Dar nikafanye mambo yangu mengine,” anasema
Kipa huyo anasema baada ya soka kuzingua kwa sasa anajishughulisha na mambo ya kuhudumu hotelini lakini kama timu zitamfuata anaweza kurudi tena uwanjani.
“Kwenye maisha yangu napenda soka na uhudumu wa hotelini ingawa sikusomea lakini napenda sana, kwa sasa nimeona nikae pembeni kidogo na soka nitafute pesa,”
“Lakini kama kuna timu zityatokea na kuweka mpunga wa maana narudi uwanjani bado umri unaruhusu kucheza ingawa hata nikiacha kucheza nimepanga kusomea ukocha baadae nije kufundisha.”
Anasema akiwa Congo mwaka 2013/14 aliwahi kuitwa jina la Kaseja akiwa uwanjani mashabiki wakimfananisha na kipa wa zamani wa Yanga na Simba, Juma Kaseja.
“Nilianza kumfuatilia Kaseja kabla hata sijaja Tanzania baada ya watu kunifananisha nae na tangu hapo nikaanza kumshabikia na kumkubali alikuwa kipa mzuri sana,” anasema na kuongeza
“Alipomaliza muda wa kucheza nikaanza kumfuatilia Aishi Manula wakati ule alikuwa na kiwango bora na sijui kwanini sasa hivi hachezi ilihali Tanzania kuna uhaba sana wa kipa ya aina yake.”
Pamoja na watu kuzungumza kuhusu umri kuwatupa mkono kiungo mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama na mchezaji wa zamani wa Simba, Saido Ntibazonkiza kwake nduio wachezaji bora wa muda wote.
“Walikuja wakina Haruna Niyonzima, Mukoko Tonombe walikuwa bora sana lakini kwangu napenda aina ya uchezaji ya Chama na Saidoo wanajua nini timu inataka na kwa wakati mgumu inawapatia matokeo,”
MASTRAIKA HAWA WALIMKOSHA
Anasema aina ya uchezaji wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, Meddie Kagere ambaye anaitumikia Namungo na Jean Baleke wa Yanga ni mastraika ambao wangempa shida langoni.
“Kwenye timu ukiwa na wachezaji hao unaweza kutolewa mchezoni kabisa kutokana na kasi yao, nguvu na ujuzi wa kuliona lango hivyo ni washambuliaji ninaowakubali sana,”
Nje na changamoto alizopitia mchezaji huyo ikiwemo kula mlo mmoja kwa siku lakini kwa kiasi fulani amepata mafanikio ikiwemo kuendesha maisha yake.
“Kama nisingepata mafanikio kwa miaka yote hiyo nisingeendelea kufanya kitu ambacho hakina faida, kwahiyo kiasi fulani nimepata mafanikio ikiwemo kumsomesha mwanangu kwa pesa ya soka na kuendesha maisha, kupanga chumba changu mwenyewe ingawa sijafanikiwa kujenga lakini nipo kwenye mchakato huo.” anasema
Anasema amecheza Ligi nchi mbalimbali Afrika Mashariki lakini Tanzania kuna utofauti kwanza maslahi, muitiko wa mashabiki wanaokuja uwanjani kushabikia timu zao hususani Simba na Yanga.
“Miaka mitano ijayo, WPL itakuja kuwa ligi tishio kama timu zingine zitaendeshwa kama vigogo wanne wa soka la wanawake Tanzania, matunda yanaonekana hata kwa mauzo ya wachezaji tu,” anasema na kuongeza
“Sasa hivi Tanzania imetoa wachezaji sita wanaocheza soka la kulipwa nje na wanapata nafasi ya kucheza, Aisha Masaka (Brighton), Clara Luvanga (Al Nassr), Enekia Lunyamila, Opah Clement, Diana Msewa na wengine ambao wamekuwa msaada kwenye timu zao.”
Anasema si kila mchezaji anakuwa na tabia za kujiweka kiume kuanzia mavazi hadi miondoko kwani yeye yupo tofauti na anaamini mwanamke atabaki kuwa hivyo hata iweje.
“Najua kuishi na kila aina ya watu kwa hiyo binafsi nimeweza kuepuka mtego huo na kuna muda nakaa nawashauri wadogo zangu acheni hivi fanya hivi na wapo wanaelewa,” anasema na kuongeza
“Ukiingia ndani kwangu pia utaona kuanzia mavazi kila nguo ambaye mtoto wa kike anayo mimi navaa, magauni, vitenge, suruali za kike hadi kupika niko vizuri na niko kwenye mahusiano na mtu ambaye anapenda ninachokifanya.”