Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue kuwa Mwenyekiti wa Tume Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi nchini humo.
Tume hiyo iliyotangazwa leo Jumatano, Julai 31, 2024 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ina wajumbe wanane waliobobea kwenye nyanja za uchumi akiwemo Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Profesa Mussa Assad.
Wengine ni, Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, Mtaalamu na Mshauri wa Masuala ya Kodi na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Kodi, PwC, David Tarimo.
Aliyekuwa Ofisa Mtendaji MKuu wa Price Water House (PwC), Tanzania, Leonard Mususa, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Aboubakar Mohamed Aboubakar na Mshauri wa Masuala ya Sheria, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar.
Julai 29, 2024, Rais Samia katika Mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) alitangaza uamuzi wa Serikali kuunda kamati ya kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi nchini Tanzania.
Endelea kufuatilia Mwananchi.