Rais Samia kusafiri kwa SGR Dar-Dodoma kesho

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan kesho Alhamisi, Agosti 1, 2024 atazindua treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kwa kupanda kutoka jijini Dar es Salaam hadi Dodoma.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkoa wa Dodoma leo Jumatano Julai 31, 2024, imesema Rais Samia atasafiri kwa treni hiyo kwa kilometa zaidi 444 kama ishara ya uzinduzi.

Jana Jumanne, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema reli hiyo itasaidia katika kukuza biashara, utalii na mapato ya Mkoa wa Dodoma.

“Hii ni fursa kubwa ya kutangaza mazao yanayopatikana Mkoa wa Dodoma. Kuwepo kwa treni hii ambayo kwa muda mfupi itaanza kusafirisha mazao ni fursa kubwa kwetu,” amesema.

Amesema kutakuwa na fursa ya kibiashara kutokana na mizigo mikubwa ikiwemo makontena itakayosafirishwa kwa njia ya SGR, itashushwa katika bandari kavu iliyopo Ihumwa jijini Dodoma na kisha kusafirishwa kwenda katika maeneo mengine ndani na nje ya nchi.

“Tumejipanga Agosti Mosi 2024, kesho sisi kwetu itakuwa ni siku ya pekee ambapo mheshimiwa Rais Samia anakwenda kuzindua rasmi treni hii ya mwendo kasi, pamoja na reli ya mwendo kasi, tutakuwa zaidi ya watu 30,000 hapa kumpongeza Rais Samia kwa ujenzi wa reli hii,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya ameagiza madereva wote kujisajili katika kituo chao ili kuepuka ugomvi unaoweza kujitokeza kwa kigezo cha watu kuvamia kituoni.

“Taratibu mtakazowekeana mzifuate, mheshimiane…la pili acheni ulevi, Serikali ilikuwa imeondoa viroba lakini kuna vipombe vingine vimekuja mnatembea navyo achaneni na hizo pombe kwanza zina madhara,” amesema.

Kamanda Mallya amewataka madereva hao kuacha tabia ya kuwaibia abiria mizigo yao wanaowasafirisha.

“Yaani mama wa watu ametoka Dar es Salaam kuhenyeka amekuja na begi lake la mizigo, nguo zake za kuuza, unamtelekeza na unaondoka na mzigo ni dhambi. Acheni kuibia abiria,” amesema.

Amewataka pia kufuata sheria za usalama wa barabarani kwa kuwa hakuna mtu aliyejuu ya sheria.

Mmoja wa madereva bodaboda, Elias Antony amesema tangu kuanza kwa safari za treni hiyo Julai 25, 2024 amesema awali walikuwa wakipata Sh20,000 lakini kwa sasa hivi suala la kuondoka na Sh40,000 kwa siku sio shida tena.

“Tunamshukuru Mungu hata mapato ya biashara yanakuwa kidogo mazuri tofauti na mara ya kwanza katika kijiwe chetu. Ujio wa treni hii umekuja kutubusti kidogo kabla hata kufunga hesabu za mabosi wetu ilikuwa ni mtihani,” amesema.

Amewataka waendesha bodaboda na bajaji kuheshimu shughuli wanazozifanya.

Katibu wa Kijiwe cha Bodaboda cha Chamdumi SGR, Simon Kawawa amesema jumla ya madereva 180 wa bodaboda na bajaji wamejiandikisha kwenye kituo hicho na kwamba waliokamilisha taratibu zinazotakiwa wako 123.

“Kwa wale wanaofahamika wanatakiwa kutoa hela ya kiingilio ambayo ni Sh70,000 lakini waliotoka mbali na maeneo haya wanatakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa mwenyekiti wa serikali anakoishi. Hii ni kuweka kumbukumbu za watu wetu na kufahamu,” amesema.

Amesema kwa bodaboda aliye na namba ya kadi ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) inakuwa ni vyema zaidi.

Kawawa amesema utaratibu huo utawasaidia inapotokea changamoto kufahamika ni nani aliyekutwa na tatizo na wapi pakumpata.

Kuhusu udhibiti wa nidhamu, Kawawa amesema wameweka utaratibu kuwa itapojulikana mtu ametumia kilevi hataruhusiwa kufanya kazi hadi hapo kilevi kitakapoisha huku wanaotumia lugha chafu wakifutia usajili katika kijiwe hicho.

Related Posts