SERIKALI IMEIMARISHA NGUVUKAZI SEKTA YA AFYA – MWANAHARAKATI MZALENDO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeimarisha nguvukazi kwenye sekta ya afya kwa kuongeza taasisi zinazotoa mafunzo ya afya na upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa kada hiyo.

“Serikali imefanya upanuzi wa taasisi za mafunzo ya afya ili kuongeza idadi ya wahitimu. Taasisi hizo ni pamoja na vyuo vya uuguzi, ukunga na utabibu. Hivi sasa nchi yetu ina taasisi 182 zikiwemo taasisi 137 zinazomilikiwa na sekta binafsi. Ni jambo la faraja kuona kuwa katika mwaka 2023/2024 peke yake, vyuo hivyo vimedahili wanafunzi 40,000.”

Akizungumza na viongozi, wadau na watumishi walioshiriki ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya  (Jumanne, Julai 30, 2024), Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu zinapatikana kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa.

“Lakini pia, wanafunzi wanaosomea kozi za afya wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100. Vilevile, suala la kuendeleza rasilimali watu limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kila mwaka ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa,” amesema.

Akielezea kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali, Waziri Mkuu amesema Serikali imekwishaimarisha huduma ya afya ya msingi, huduma za afya katika ngazi ya wilaya na sasa inaimarisha huduma hizo kwenye ngazi ya Halmashauri.

“Tumeimarisha huduma za msingi, tumeimarisha hospitali za wilaya na sasa tunajenga hospitali za Halmashauri ili kupunguza umbali kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni. Sasa hivi tunaimarisha pia huduma za rufaa kama vile Benjamin Mkapa na Bugando,” amesema.

Inaweza kuwa picha ya Watu 5, jukwaa na maandishi
Inaweza kuwa picha ya Watu 3, jukwaa na maandishi

Related Posts