SERIKALI KUJENGA KITUO CHA KUREJELEZA TAKA DODOMA – MWANAHARAKATI MZALENDO

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema imejipanga kujenga kituo cha kurejeleza taka za plastiki pamoja na kuhifadhi na kuchambua taka ngumu kwa ajili ya kutumika kama malighafi ya viwanda.

Kituo hicho kitakachojengwa katika Jiji la Dodoma kitasaidia ukusanyaji wa taka kutoka dampo kwa ajili ya kuchakatwa hatua itakayosaidia kulinda mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo wakati akizungumza kwenye kipindi cha ‘Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo’ kinachotayarishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Amesema kuwa si kazi za viwandani pekee ndizo zinazozalisha gesijoto angani lakini pia shughuli mbalimbali za kila siku za mwanadamu ni chanzo cha uzalishaji wa gesijoto hiyo.

“Shughuli zetu za kila siku za nyumbani, ofisi tunatupa taka tunazikusanya na zikichukuliwa kupelekwa dampo zinazalisha gesijoto ambayo ina athari kubwa katika mazingira yetu na hatimaye kutuletea changamoto ya mabadiliko ya tabianchi,“ amesema.

Kutokana na hali hiyo, Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa mwaka 2021 Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mwongozo wa Udhibiti wa Taka Ngumu kuhamsisha taasisi na jamii namna ya kupunguza uzalishaji wa taka.

Ameongeza kuwa Mwongozo huo ulikuja na dhana tatu ambazo ni Punguza (Reduce) matumizi ya bidhaa ambazo huzihitaji kwa muda huo kwasababu ni wazi unapoitumia itakuletea taka na kwenda kwenye mazingira na kuleta athari. Pili kuna bidhaa ambazo zinaweza kutumiwa tena (Reuse) badala ya kutupwa.

Dhana ya tatu Dkt. Kijaji ametaja kuwa ni Rejeleza (Recycle) ambazo zinaweza kutumika tena kwenye viwanda kama malighafi ya kuzalisha bidhaa zingine ili kuhamasisha jamii kulinda mazingira.

Aidha, Dkt. Kijaji amesema Mwongozo huo umeelekeza kila halmashauri iwe na kituo cha kukusanya taka ili zirejelezwe na kwa msingi huo ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo itakayosaidia kuwapatia kipato sanjari na kulinda mazingira.

Pia, amewapongeza mabalozi wa mazingira kwa kujitoa kwao katika shughuli zao za kuhamasisha kulinda na kuhifadhi mazingira katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo upandaji wa miti.

#KonceptTvUpdates

Related Posts

en English sw Swahili