Sh425 milioni kuwapatia maji watu 20,036 Hanang

Hanang. Hatimaye wananchi wapatao 20,036 waliokuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji na usafiri wa mazingira wilayani Hanang Mkoa wa Manyara, wanatarajia kuondokana na adha hiyo baada ya mradi wa Sh425 milioni kuzinduliwa wilayani humo.

Mradi huo uliotekelezwa na Shirika la Water Aid kwa ufadhili wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho umehusisha uboreshaji wa huduma za miondombinu ya maji na usafi wa mazingira.

Akizungumza leo Julai 31, 2024 wakati wa halfa ya makabidhiano ya mradi huo katika Kijiji cha Bashang wilayani humo, Mkurugenzi Mkaazi wa shirika hilo, Ana Mzinga, amesema mradi huo ulizinduliwa Septemba 2023 mjini Katesh wilayani humo na sasa umekamilika.

Amesema katika kikao cha wadau kilichozindua mradi huo mchakato wa utekelezaji uliwasilishwa na kilichokuwa kimebaki ni utekelezaji.

“Tunakiri kupata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini na wataalamu katika kutekeleza mradi huu na mpaka sasa umefanikiwa kukamilika kwa asilimia 100 katika miundombinu ya vyoo bora, miundombinu ya usambazaji wa maji safi, miundombinu ya usafi binafsi na usafi wa kitaasisi na uelimishaji wa jamii ya watumiaji wa miundombinu,” amesema.

Mzinga amesema lengo la WaterAid inayofanya kazi na Serikali limefikiwa kupitia mradi huo, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya maji safi na salama, vyoo bora na mazingira salama ya usafi na usafi binafsi.

Meneja Mkurugenzi wa shirika hilo Kanda ya Afrika Mashariki, Leah Kaguara amesema wataendeleza ushirikiano na Serikali kuhakikisha kuwa kila mtu anafikiwa na huduma za maji salama, usafi wa mazingira.

Amesema mradi huo uliokabidhiwa unakwenda sambamba na mkakati wa shirika hilo uliopitishwa mwaka 2022 pamoja na programu za nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania zilizozindua mikakati yao mwaka 2023.

“Huduma katika eneo la Wilaya ya Hanang italeta mabadiliko makubwa kwa lengo la hamasisha usafi wa mazingira (WASH) ili kuboresha afya kwa umma,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almish Hazali ameshukuru kwa mradi huo na kueleza kuwa miundombinu yote iliyopangwa kutekelezwa imekamilika vizuri na ipo tayari kwa matumizi.

Amesema mradi huo utawanufaisha wananchi wakiwemo wanafunzi, wagonjwa katika Kata za Laghanga, Wareta na maeneo ya jirani.

“Tunaomba mwendelee kutuwezesha zaidi katika maeneo mengine yanayohitaji huduma za maji na usafi wa mazingira ili kuunga mkono jitihada za Serikali chini uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Related Posts