Unguja. Ili kuimarisha uhifadhi wa taarifa na utendaji wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imetia saini mkataba wa ujenzi wa kituo cha kuhifadhia kumbukumbu na Kampuni ya Emerging Communication Ltd (Ecom).
Kituo hicho kitajengwa kwa ufadhili wa Mamlaka ya Mapato ya Norway (NTA) ikiwa ni sehemu ya kuijengea uwezo ZRA, huku Sh613.88 milioni zikitarajiwa kugharamia ujenzi huo.
Akizungumza baada ya utiaji saini mkataba huo leo Julai 31, 2024, Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed amesema kituo hicho kitajengwa katika ofisi kuu ya ZRA iliyopo Gombani kisiwani Pemba na kitahudumia ofisi zote za mamlaka hiyo Unguja na Pemba.
Amesema lengo la kituo hicho ni kuimarisha utendaji wa ZRA katika uwekaji na uhifadhi wa kumbukumbu za wadau wake, huku kikitumika pia kama mbadala wa kuhifadhia taarifa za taasisi hiyo iwapo kutatokea hitilafu.
“Iwapo kutatokea majanga mfano wa moto na kuathiri kituo cha kuhifadhia taarifa kilichopo Unguja, ZRA haitaathirika kwani kituo hicho kitaiwezesha kufanya kazi zake kama kawaida kwa kuwa itakuwa rahisi kurejesha taarifa zilizopotea,” amesema.
Kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa, ujenzi unatarajiwa kuanza mara moja na utakamilika ndani ya miezi mitatu tangu tarehe ya kusainiwa kwa mkataba huo.
Amesisitiza ni matarajio ya ZRA kuwa kampuni iliyoshinda zabuni ya kujenga kituo hicho ya Ecom itatekeleza masharti yote ya mkataba ikiwemo kukamilisha kazi kwa wakati na ufanisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Said Buhero amesema wana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika miradi ya aina hiyo, hivyo kazi hiyo ni mwendelezo wa nyingi nzuri walizozifanya.
Amebainisha kuwa ujenzi wa mradi huo utakwenda kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa ikiwamo kuhakikisha unakamilika kwa muda uliopangwa.
ZRA na NTA zina makubaliano ya muda mrefu. Ambapo kupitia makubaliano hayo, ZRA imenufaika katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujengewa uwezo katika eneo la miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kuimarisha muundo wa taasisi.