Ubovu barabara, ukosefu maji vyawasuta madiwani kwa wananchi

Mwanza. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, wameingiwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kupoteza kura za wananchi kutokana na ukosefu wa maji na ubovu wa barabara katika maeneo yao.

Wakizungumza leo Jumatano Julai 31, 2024, kwenye kikao cha robo mwaka cha Baraza la Madiwani kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2024, wamesema hali hiyo inaweza kutoa mwanya kwa vyama vya upinzani kupita kirahisi kwenye kata na majimbo wanayoyaongoza.

Ikumbukwe madiwani wote wa Wilaya ya Misungwi wanatokana na Chama cha Mapinduzi (CCM)

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Mamaye, Christina Nyanda amesema licha ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo, utekelezaji wa miradi ya maji umekuwa wa kusuasua hali inayowapa hofu wanapoelekea kwenye chaguzi zijazo.

Diwani wa Sumbugu, Jogoli Mayombo ameunga mkono hoja hiyo huku akimshutumu Meneja wa Mamlaka ya Maji Vijijini (Ruwasa) kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, hali inayowaweka madiwani hao katika wakati mgumu.

Hata hivyo, Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Misungwi, Marwa Kisibo ameijibu malalamiko hayo kuwa mpaka sasa wametoa huduma ya maji kwa vijiji 53 kati ya 10, na miradi inayoendelea itakapokamilika, wilaya hiyo itafikia lengo la kutoa huduma ya maji kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Akizungumzia kero ya barabara, Diwani wa Kanyelele, Daniel Makoye amesema Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) anapaswa kuja na mikakati madhubuti ya kutengeneza barabara hizo ili kunusuru kura zao.

“Barabara zote za Misungwi ni mbovu ukizingatia sisi madiwani tunatetea kitumbua chetu, tunaelekea katika uchaguzi na changamoto kubwa iliyopo ni ubovu wa barabara kwa hiyo kinachotakiwa tuwekewe mikakati ya Tarura wanaanza lini kutengeneza barabara ili tukienda kwenye mikutano ya hadhara tuwe na kitu cha kuwaeleza wananchi,” amesema.

“Kuna mwanachama wangu anafanya kazi Zanzibar alipata msiba wa baba yake mzazi wakawa wamekuja viongozi wakubwa lakini cha kusikitisha gari zao zilizama kutokana na ubovu wa barabara mpaka ikafikia wakati wakaanza kunisema kwamba hivi eneo hili kuna diwani kweli,” amesema Makoye.

Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Misungwi, Dickson Mwangwa amesema athari za mvua kubwa zilizonyesha zimesababisha kuharibika kwa barabara nyingi wilayani humo, lakini serikali inaendelea na matengenezo.

“Tunaendelea kuchukua hatua na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa hiyo madiwani tuendelee kuvuta subira kwa sababu sio hapa tu ni kote lakini kwa sasa kipaumbele wanaangalia barabara kuu kabla ya kwenda kwenye hizi barabara za vijijini,” amesema Mwangwa.

Amesema ili kufikia lengo la Serikali la utoaji huduma ya maji maeneo ya vijijini kwa asilimia 85 Ruwasa inatekeleza miradi minne inayogharimu zaidi ya Sh890 milioni ambayo inaenda kuhudumia wananchi 285,620 ambayo hadi Desemba mwaka huu itakuwa tayari hivyo kuwatoa hofu madiwani hao.

“Tuna amini hadi ifikapo 2025 tunaenda kutimiza lile lengo la ilani kwa kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji Misungwi kwa sababu miradi ambayo tunatekeleza ikikamilika yote kwa pamoja inaenda kuhudumia wananchi wengi kwa hiyo niwatoe hofu madiwani hadi mwakani itakuwa tayari na siyo tu kwamba tuna angalia uchaguzi tu,” amesema.

Enos Mihayo ni diwani wa Gulumungu, alitoa wito kwa Ruwasa na Tarura kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kuomba fedha zaidi kutoka serikalini ili kutatua changamoto hizo badala ya kusubiri kusukumwa na baraza la madiwani.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi aliwasihi Tarura na Ruwasa kusimamia vyema fedha zinazotolewa na serikali na kuhakikisha changamoto hizo zinapungua kwa kiwango kikubwa ifikapo Desemba mwaka huu.

Related Posts