Dar es Salaam. Viongozi wa dini nchini Tanzania wamemuelezea Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa ni kiongozi aliyeacha alama zinazoendelea kukumbukwa na Watanzania wengi, kupitia huduma za afya nchini.
Katika kipindi cha Taasisi ya Benjamin Mkapa jumla ya wataalamu wa afya 1,150 wamesomeshwa na kutoa ajira zaidi ya 13,000 katika sekta ya afya maeneo mbalimbali hususan pembezoni.
Wakizungumza leo Jumatano Julai 31, 2024 wakati wa kumbukizi ya tatu ya Urithi wa Benjamin Willam Mkapa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam, wamesema alama hizo zimeendelea kuwagusa Watanzania wengi.
Viongozi wa wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanashiriki kumbukizi hiyo wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkapa alihudumu kama Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005. Alifikwa na mauti Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam na kuzikwa kijijini kwake, Lupaso, Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.
Sheikh Ally Hamis Ngiluko kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) amesema taasisi hiyo ni kivutio na baraka kwa nchi na kwamba maisha ya Mkapa ni zawadi kwa Watanzania wote.
“Taasisi kama hizi zikiwepo katika jamii ni kama mtu aliyepanda miti mingi kwenye jamii yake inaleta hewa nzuri ni kivutio cha baraka na rehema za mwenyezi Mungu. Mzee Mkapa ameacha kitu kikubwa katika jamii ya Kitanzania,” amesema.
Askofu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Christian Likoko amesema kiongozi huyo atakumbukwa kutokana na yale matendo mema aliyoyafanya akiwa hai, ambayo yanaendelea kusaidia Watanzania wengi mpaka sasa.
Askofu kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Jackson Sostenes amesema alama ya Rais wa awamu ya tatu kupitia Mkapa Foundation, imesaidia kuwafikia Watanzania walio wengi na wanyonge wasio na msaada huku akiishukuru Serikali kufungua milango.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Thobias Makoba amesema jamii inakutana kuenzi kazi yake kwa kuwa alijenga Tanzania imara na endelevu.
Makoba amesema kumbukizi ya mwaka huu inatazamwa tofauti ikiwemo kuhuisha na kuonyesha mchango wake haukuwa kwenye afya kwani ni pamoja na mambo mengine.
“Kwanza ni kuhusu dira ya nchi yetu awamu yake ya kwanza, dira ya muda mrefu ilianza kutumika mwaka 2000 inatupeleka mpaka mwaka 2025.
“Rais Samia sasa unakwenda kuandaa dira ya miaka 25 mingine kutoka 2026 mpaka 2050, tunakutakia kila la kheri kwa kubebea maono ya Watanzania, hii ni namna bora ya kumbukizi hii,” amesema Makoba.
Makoba amesema Hayati Mkapa aliendesha mradi wa kimapunduzi hata kwenye sekta ya uchumi:”Tunafahamu kesho Agosti Mosi unazindua safari za SGR, wazo la mradi huu lilianzia awamu ya tatu, umehakikisha tunakwenda kilomita 2,354 za mradi huu hii inajibu kwa vitendo dhana yako ya Kazi Iendelee.”
Pia, Makoba amesema Hayati Mkapa alikuwa mwanahabari, mhariri na mwanzilishi wa Idara ya Habari Maelezo, lakini pia amehudumu vipindi viwili kwa kuwa Waziri wa Habari.