Wadau wataja yanayokwamisha mipango ya matumizi ya ardhi kwa wanawake

Dar es Salaam. Wataalamu wa masuala ya mipango ya ardhi nchini Tanzania wamesema kinachokosekana katika uandaaji wa mipango hiyo ni Serikali kutoipa kipaumbele sekta ya ardhi kwenye bajeti.

Wamesema zipo hatua sita za utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi lakini Serikali na wadau wa maendeleo hawatoi fedha kufikia hatua hizo.

Mpango wa matumizi ya ardhi ni mchakato wa kupanga na kuamua jinsi  ardhi itakavyotengwa na kutumiwa kwa matumizi endelevu ikiwemo kilimo, makazi, biashara hifadhi ya mazingira na miundombinu.

Lengo la kuandaa mipango hiyo ni kusimamia matumizi ya ardhi kwa njia endelevu na kukuza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kuhakikisha matumizi endelevu.

Hoja hizo kuhusu dhana ya mipango bora ya matumizi ya ardhi  zimeibuliwa leo Jumatano Julai 31, 2024 kwenye mjadala wa X Space unaoandaliwa na Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat) ukiwa na mada isemayo ‘Mipango ya matumizi ya ardhi, uhifadhi wa maliasili na haki za wanawake.’

Akichangia mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki Ardhi, Cathbeth Tomitho amesema kinachokosekana katika uandaaji wa mipango ya ardhi ni utashi wa kisiasa.

“Tanzania inategemea kilimo kama njia ya uzalishaji chakula na kukuza uchumi wa taifa, lakini kilimo kinategemea rasilimali ardhi bahati mbaya sana Serikali haijaipa kipaumbele eneo la ardhi kwenye bajeti,” amesema na kuongeza kuwa.

“Ukiangalia vipaumbele vitano vya juu vya Serikali sekta ya ardhi haipo, bajeti yake ni ndogo sana hivyo kuna utashi mdogo wa kisiasa ndio maana hakuna bajeti ya kutosha kwenye mipango ya matumizi ya ardhi, utatuzi wa migogoro na utawala mzima wa ardhi,” amesema.

Tomitho amesema pamoja na umuhimu wa mipango ya ardhi, zipo hatua sita za utekelezaji wa mipango hiyo lakini Serikali na wadau wa maendeleo hawatoi fedha kufikia hatua hizo.

Mfano, amesema ipo hatua ya utoaji wa hati miliki ambayo ni mara chache mipango ardhi iliyofanyika hufikia ikiwemo utoaji wa hatimiliki za kimila jambo ambalo husababisha wanamke kukosa haki ya kumiliki ardhi.

Hatua nyingine ni mpango wa kina wa matumizi ya ardhi ambayo mipango mingi haifiki katika hatua hiyo.

“Dhana nzima ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ni kuboresha maslahi yaliyopo katika ardhi, haina maana kuwa na mpango bora ya matumizi ya ardhi ambayo kimsingi hayaboreshi maisha ya wamiliki na watumiaji wa ardhi,” ameeleza.

Kutokana na hayo, ameeleza mipango mingi ya uboreshaji wa ardhi iliyoandaliwa haijakamilika na haionyeshi tija kwa wamiliki wa ardhi hususani wanawake ambao ndio watumiaji wakubwa wa ardhi nchini.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Obed Katonge amesema, kuwajengea uwezo wanawake kwenye masuala ya ardhi huendana na kutoa elimu kwa jamii ikiwemo kundi hilo kuwapatia elimu na mafunzo juu ya haki zao na namna ya kuzitetea.

Amesema suala la umiliki wa ardhi wanasisitiza katika upangaji wa matumizi ya ardhi wanapofikia hatua ya umilikishaji wanahamasisha ugawaji wa ardhi kwa kuangalia jinsia ya wanawake kumilikishwa kwa majina yao.

“Mipango ya matumizi ya ardhi huondoa migogoro ambayo mara nyingi wanawake ndio huathirika kutokana na nafasi zao kwenye jamii kwa kuonekana ni dhaifu,” amesema.

Ameeleza mipango ya matumizi ya ardhi hupunguza migogoro hivyo wanawake wanaendesha shughuli zao bila kuwa na hofu ya kupoteza ardhi zao.

Ardhi na umiliki wa vijiji

Kwa upande wake, Ofisa Programu kutoka Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (Leat), Franklin Masika amesema ardhi kubwa hapa Tanzania ipo kwenye umiliki wa vijiji ikifuatiwa na ardhi ya hifadhi na ile ya jumla.

Ameeleza vijiji vina rasilimali nyingi hivyo kitendo cha kukosa mipango ya kusimamia basi matokeo yake changamoto hujitokeza.

Kufuatia hayo, amesema wadau hujitokeza kwenye azaki kuwasadia wanaviijiji kupitia mipango ya matumizi ya ardhi ili kuzitumia rasilimali zao kwa maendeleo.

“Tunaweza kuwa na mijadala tofauti juu ya mipango ya ardhi kutumika kunyanganya ardhi ya wanavijiji endapo hawatapata usaidizi wa kutosha,” amesema.

Akichokoza mada kwenye mjadala huo, Mwandishi wa Mwananchi, Elias Msuya amesema Tanzania ina idadi ya vijiji 12,319 lakini vilivyofanyiwa mipango ya matumizi ya ardhi ni chini ya asilimia 30, hivyo kuna zaidi ya asilimia 70 ya vijiji hivyo havijafanyiwa mipango hiyo.

Msuya amesema utashi wa kisiasa, migogoro kati ya vjiji na mamlaka zingine kama za hifadhi za wanyama ni miongoni mwa changamoto zinazokabili kufanya mipango ya matumizi ya ardhi. 

Akitaja faida za kufanya mipango ya matumizi ya ardhi amesema “Ni kulinda makazi ya watu, kuboresha miundombinu, kuwezesha upatikanaji ardhi kwaajili ya makazi kwa makundi yote ya jamii na kupanua wigo wa ajira,”amesema.

Mhariri wa Habari za Kijamii wa Mwananchi, Elizabeth Edward amesema suala umiliki wa ardhi kwa mwanamke limekuwa kilio kwa miaka mingi kutokana na mila na desturi za baadhi ya jamii zinazomfanya asiwe na haki ya kumiliki ardhi.

“Katika ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotoka mwaka 2023 imeonesha kuna watu asilimia 32.5 wanaomiliki ardhi wenye umri wa miaka kuanzia 15 na kuendelea wanawake ni asilimia 29.

“Hata kauli ya Serikali iliyotolewa Aprili mwaka bungeni ilisema kuna ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi ikifikia asilimia 41 hivyo kuna ongezeko lakini bado kuna tatizo la kumiliki ardhi kwa wanawake.

Elizabeth amesema wanawake ndiyo wanaoiendeleza ardhi kwenye umiliki wanawekwa pembeni.

Hoja hiyo inachangiwa pia na Glory Sandewa kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania na Mwenyekiti wa Kampeni ya Linda Ardhi ya Mwanamke ambaye amesema kuna utofauti kati ya sheria ya ardhi na uhalisia uliopo.

Amebainisha utofauti huo unatokana na mila na desturi kandamizi zilizopo kwenye jamii juu ya umiliki ardhi kwa mwanamke japokuwa sheria na Katiba ya nchi zinaonesha haki sawa ya umiliki.

Kutokana na hayo amesema changamoto hujitokeza kwenye utekelezaji wa sheria na sera zilizopo ndio maana wakaja na kampeni iliyoanza tangu mwaka 2019 nchini kwaajili ya kuondoa mila hizo zilizopo kwenye jamii. 

“Kampeni inamtaka mwanamke pia apate nafasi katika ngazi za maamuzi ili aweze kutumia ardhi hiyo,” amesema.

Related Posts