Wanakijiji wapewa siku 14 kupinga uamuzi wa RC Tanga

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo  ya Tanga, imetoa siku 14 kwa wananchi 11 wa Kijiji cha Nghobore, kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga uamuzi wa mkuu wa mkoa wa huo, kugawa eneo la hekta 13,000 kwa kijiji cha jirani na Jeshi la Wananchi Tanzania  (JWTZ).

Aidha, Mahakama hiyo imekataa kutoa zuio la kusitishwa kwa amri ya mkuu wa Mkoa wa Tanga, aliyoitoa mwaka 2023, kuwa ardhi ya vitongoji viwili kutoka kwenye vijiji hivyo kuhamishiwa kijiji cha jirani na nyingine kupewa JWTZ.

Uamuzi huo umetolewa Julai 29, 2024 na Jaji Messe Chaba, baada ya kukubaliana na hoja moja kati ya mbili zilizowasilishwa na wananchi hao waliokuwa wakiomba ruhusa ya kufungua maombi ya marejeo na kuomba Mahakama itoe zuio la amri ya mkuu huyo wa mkoa.

Jaji Chaba amesema Mahakama inatoa siku 14 kwa wananchi hao kuwasilisha maombi yao kama ilivyoainishwa na sheria na kukataa kutoa amri ya zuio la amri ya mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Jaji, amesema katika kutumia mamlaka iliyopewa Mahakama hiyo kwa masilahi ya haki, anaona si vyema kutoa amri ya kusitishwa kwa uamuzi wa mkuu huyo wa mkoa.

“Kwa sababu zilizotajwa, na kwa kuzingatia yale ambayo nimejitahidi kuonyesha ninatoa muda wa siku 14 kama ilivyoainishwa na sheria kuwasilisha maombi yao mahakamani,”ameeleza Jaji Chaba.

“Hata hivyo, kwa ajili ya haki, nakataa kutoa amri iliyoomba kusitishwa kwa uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati maombi ya msingi yatakapotolewa.”

Maombi hayo yalitolewa na Emanuel One Saning’o, Mary William, Rahel Isaya, Baraka Olepinyo, Neng’ida Sembeta, Maika Lekudia, Mako Masiar, Saimon Lesaito, Yona Kistei, Laiza Olesanago na Isaya Ngaruko.

Katika maombi hayo ya madai namba 7816/2024 dhidi ya mkuu wa Mkoa wa Tanga na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wananchi hao waliyawasilisha mahakamani hapo wakiomba itoe kibali kwa waombaji kuwasilisha maombi ya hati miliki.

Wanaiomba Mahakama itengue na kutangaza uamuzi wa mkuu wa Mkoa wa Tanga kuhusu kuchukua ardhi ya vitongoji vya Lembapaa na Lekirumu katika kijiji chao na kuikabidhi kwa Kijiji cha Gitu na JWTZ, wakidai hatua hiyo haikufuata utaratibu.

Kupitia hukumu iliyopo kwenye mtandao wa Mahakama Kuu wa TanzLii, hoja nyingine ni kuomba ruhusa ya kufungua maombi ya marejeo kufuatia zuio hilo; na amri yoyote ambayo Mahakama inaona italeta haki na usawa.

Maombi hayo yaliwasilishwa kwa njia ya wito wa Mahakama chini ya hati ya dharura, yakiongozwa na hati za kiapo zilizowekwa na kila mwombaji.

Katika maelezo ya hati ya kiapo, inadaiwa Septemba mosi 2023, mkuu wa Mkoa wa Tanga, alichukua hekta 13,000 kutoka vitongoji viwili vya kijiji hicho na kutoa hekta 11,000 kwa kijiji cha jirani na hekta 2,000 kwa JWTZ.

Wakati wa usikilizaji wa maombi hayo, wananchi waliongozwa na mawakili Yonas Masiaya na Denis Moses, huku mkuu wa mkoa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwakilishwa na mawakili wa Serikali, Agnes Gombe na Upendo Sakatu.

Wakili Yonas aliiomba Mahakama ipitishe na kuthibitisha hati ya maombi hayo kwa kuwa yametimiza masharti matatu yaliyoainishwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Masharti hayo ni maombi ya kuwasilishwa ndani ya muda uliowekwa, mwombaji kuonyesha nia juu ya suala hilo na waombaji kuanzisha kesi inayoweza kubishaniwa kuamuliwa katika maombi ya msingi.

Wakili Yonas amedai kuwa, maombi hayo yaliwasilishwa kwa wakati na wananchi hao wameonyesha wana masilahi ya kutosha katika suala hilo kwa kuzingatia haki zao za asili.

Amesema katika Mahakama hiyo kwenye rufaa ya madai namba 74/2012 ya Emma Bayo dhidi ya  Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana na wengine wawili, masharti matatu yalitakiwa kutekelezwa.

Masharti hayo ni maombi lazima yawasilishwe ndani ya muda uliowekwa wa miezi sita tangu tarehe ambayo uamuzi ulifanywa,mwombaji lazima aonyeshe ana nia ya suala hilo  na waombaji waanzishe kesi inayoweza kubishaniwa kuamuliwa katika maombi ya msingi.

Akifafanua sharti la kwanza, wakili Yonas amedai kuwa maombi hayo yaliwasilishwa ndani ya muda uliopangwa na kuwa amri ya kiutawala ilitolewa Septemba mosi, 2023 na maombi kuwasilishwa mara ya kwanza Machi mosi 2024 na kuwasilishwa upya tena Machi 25 na Aprili 12,2024.

Kuhusu sharti la pili, amedai wananchi hao kupitia taarifa yao wameeleza kuwa, ni wakazi wa Kijiji cha Nghobore  na wameweza kuonyesha wana masilahi ya kutosha kuhusiana na suala hilo.

Wakili Yonas amedai kuwa, uamuzi wa mkuu wa mkoa ulikiuka kanuni ya haki asilia; na ulifanywa bila sababu kwa kutozingatia shughuli endelevu zinazofanywa na wananchi hao na kuomba Mahakama iruhusu ombi hilo.

Pia,  ameomba Mahakama isitishe amri ya mkuu wa mkoa hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na iwapo agizo hilo halitasitishwa, utekelezaji wake utaathiri shughui endelevu zinazofanywa na wananchi hao ambazo ni kutumia eneo hilo kwa ajili ya malisho.

Kwa upande wa wakili Denis amesema kitendo hicho hakikuwa tu kwa ajili ya kubainisha mipaka bali pia kilihusisha kuchukua ardhi na kuigawia Kijiji cha Gitu na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). “Hatua hii imeathiri maisha ya wananchi hao kwa sababu eneo hilo walikuwa wakilitumia kwa malisho ya mifugo yao,” amedai wakili huyo.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali aliomba Mahakama kupitisha hati ya kiapo ya walalamikiwa iliyowasilishwa ili iwe sehemu ya mashauri, akidai walalamikiwa wamekidhi sharti la kwanza.

Hata hivyo, wakili wa Serikali amepinga masharti ya pili na ya tatu, akidai hayakufikiwa na wananchi hao.

Kuhusu sharti la pili, wakili wa Serikali amedai kuwa, wananchi hao hawana masilahi katika suala hilo kwa kuwa hakuna kipande cha ardhi kilichochukuliwa kutoka vitongoji vya Lekirumu na Lembapaa ndani ya Kijiji cha Ng’hobore na kugawiwa kwa watu wengine.

 Amedai kuwa, kilichofanywa na mkuu wa  mkoa ni kusuluhisha mizozo ya muda mrefu ya mpaka kati ya halmashauri za vijiji hivyo; na kazi hiyo ilihusisha utambuzi wa mipaka ya vijiji vinavyopakana, bila kuchukua ardhi yoyote kutoka kwa waombaji au wenzao ndani ya kijiji.

Kuhusu sharti la tatu, wakili huyo amedai kuwa, baada ya kupitia maombi ya wananchi hao, alibaini hakuna kesi ya msingi au masuala yanayobishaniwa kati ya pande zote. Akizungumzia suala la ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa, amedai kuwa haki hiyo haikukiukwa, hivyo madai ya wananchi hayana msingi na aliomba maombi hayo yakataliwe kwa sababu wameshindwa kutoa sababu za kutosha za kuishawishi Mahakama kutoa amri iliyoombwa.

Jaji Chaba amesema katika mazingira hayo, masuala yenye utata yatakayoamuliwa na Mahakama hiyo ni mawili, kama waombaji wana masilahi ya kutosha na pili iwapo kuna kesi inayoweza kubishaniwa inavyostahili na kuamuliwa.

Jaji amesema Mahakama inalazimika kujiridhisha kwamba mwombaji ameonesha nia ya kutosha kuhusu jambo hilo na ameleta kesi inayobishaniwa ili kuhalalisha ombi kuu.

Katika kuamua hilo, amesema ni marufuku kujadili uhalali wa kesi kwa wakati huo.

Akizungumzia hoja ya kwanza, Jaji amesema ni kweli ardhi hiyo haiwaondolei waombaji masilahi yao.

Baada ya kusoma na kuchunguza taarifa hiyo, viapo vya waombaji na mawasilisho ya mawakili wa waombaji, amethibitisha kuwa waombaji wameonesha nia yao ya kupinga amri iliyokusudiwa.

Pia, Jaji amesema viapo vya wananchi hao vinaonesha wao ni wakazi wa Kijiji cha Nghobore, eneo ambalo lina mgogoro huo.

“Inafaa kufahamu kuwa haki ya kusikilizwa, kama inavyodaiwa, ni kanuni ya haki ya asili inayojikita katika kanuni ya msingi ya mfumo wetu wa kisheria, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Kwa hiyo, madai haya pekee yanatosha kuanzisha kesi inayostahili kuzingatiwa na mahakama,” ameeleza Jaji.

Jaji, amefafanua zaidi kuwa, kama ilivyoelezwa na waombaji, walinyimwa haki yao ya kusikilizwa na ana maoni kwamba, wameonyesha kesi inaweza kubishaniwa na inahitaji kuamuliwa katika ombi kuu lililokusudiwa.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts