Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kuwa na mashahidi watano katika kesi ya kusafirisha kilo moja ya bangi inayomkabili Sauda Athuman (48).
Sauda mkazi wa Majohe, anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 1.02, tukio analodaiwa kulitenda Septemba 21, 2023 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mashahidi hao pamoja na vielelezo, wanatarajia kutoa ushahidi wao, Agosti 22, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga ameieleza mahakama hiyo leo Jumatano, Julai 31, 2024 wakati akimsomea hoja za awali (PH) mshtakiwa huyo.
Mshtakiwa huyo amesomewa maelezo hayo, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.
Mwanga amemsomea maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, anayesikiliza shauri hilo.
Sauda ambaye alitinga mahakamani hapo akiwa amevalia dera rangi ya maroon iliyokoza na mtandio wake akitupia juu ya mabega huku chini akijifunga kitenge cha wax chenye michoro ya matawi ya majani rangi ya chungwa.
Kichwani, Sauda alikuwa amesuka nywele tano za mkono za kawaida maarufu kama mnyoosho au twende kilioni.
Kabla ya kusomewa maelezo yake, wakili Mwanga alimkumbusha shtaka linalomkabili kwa kumsomea upya.
Baada ya hapo, Mwanga alimsomea maelezo ya awali, ambapo alidai Septemba 21, 2023 saa nane mchana alifikia katika Bandari ya Dar es Salaam iliyopo wilaya ya Ilala.
Baada ya kufika bandari hapo alikaa sehemu wanapokaa abiria wanaosafiri kwenda Zanzibar, akiwa na bengi.
“Baadae alipitisha begi lake katika mashine ya ukaguzi iliyopo bandarini hapo, lakini begi hilo lilitiliwa mashaka,” amedai.
Wakili Mwanga ameendelea kudai baada ya begi la Sauda kutiliwa mashaka, maofisa walimwamuru alifugue bagi hilo.
Amedai baada ya kufunguliwa begi hilo ndani yake ulikutwa mfuko wa nailoni uliokuwa umefungwa na kuzungushiwa Kamba,” amedai na kuongeza kuwa.
“Baada ya kufunguliwa mfuko ile wa nailoni ndani yake yalikutwa majani anayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi,” amedai wakili Mwanga na kuongeza:
“Ndani ya begi hilo ilikutwa pia tiketi ya boti ya kwenda Zanzibar na kitambulisho cha taifa chenye jina la Sauda Mohamed Athuman na simu mbili za mkononi aina ya Sumsang,” amedai Wakili.
Ameendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa na mshtakiwa baada ya kukutwa na majani hayo, hati ya ukamataji iliandaliwa na mshtakiwa huyo alisaini.
“Majani yaliyokutwa katika begi la Sauda yalipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na baada ya kuchunguzwa yalibainika kuwa ni dawa ya kulevya aina ya bangi,” amedai Mwanga.
Amedai Sauda alikamatwa na kupelekwa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU) kwa ajili ya mahojiano.
Julai 17, 2024 mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Baada ya kumaliza kusomewa maelezo yake, mshtakiwa alikubali majina yake na anuani yake huku akikana shtaka linalomkabili.
Mshtakiwa huyo amedai begi alilokamatwa nalo siyo lake.
“Nakiri kukamatwa bandarini lakini siyo kukamatwa na bangi na pia simu na vitambulisho vyangu vilikuwa katika pochi yangu ndogo na siyo katika begi,” amedai mshtakiwa.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza hoja hizo, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 22, 2024 itakapoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.