ULIMUANGALIA Maxi Nzengeli kwenye mechi zake tatu za kirafiki za Sauzi? Mabosi wa Yanga wameshtukia jambo na kumuita mezani kuanza mazungumzo mapya ya mkataba mpya.
Maxi atakapoanza msimu ujao ndio utakuwa mwaka wa mwisho wa mkataba wake wa miaka miwili na Yanga aliousaini akitokea Union Maniema ya DR Congo.
Kwenye mechi tatu za kirafiki kiungo huyo amekiwasha kiwango kikubwa na kuwakosga makocha wawili akiwemo kocha wake Miguel Gamondi.
Kumbe sio tu makocha hao mabosi wa Yanga nao wanamsoma kiungo huyo na Sasa wameanza kuchukua hatua za haraka kumpa mkataba mkubwa mwingine wa miaka miwili.
Maxi kiufundi ana nafasi kubwa ya kuwepo kwenye safu ya kiungo ya Yanga kutokana na ubora wake wa kuzunguka Uwanja mzima akiwa eneo la ulinzi wakati timu yake inashambuliwa, yuko pia eneo la kiungo wakati kikosi chake kikiwa kinautafuta mpira na hata kikishambulia lakini pia mbele akitengeneza na hata kufunga.
Pia ndio kiungo mwenye nidhamu kubwa uwanjani na hata nje ya uwanja achilia mbali kuchomekea kwake akiwa ndani ya uwanja.
Ubora huo ukawafanya mabosi wa Yanga kuharakisha mchakato huo wa kumpa mkataba mrefu ambao utamfanya kusalia zaidi nyumba ya Mabingwa hao wa Kihistoria.
“Tumeshaanza maandalizi ya kumpa mkataba mpya, tunaona kila kitu na kifupi tumekuwa tukimboreshea mambo baadhi taratibu kwa kuwa tunafuatilia kila kitu kuhusu wachezaji wetu,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.
“Tunataka kumbakisha zaidi hapa, huyu ndio mmoja ya wachezaji wenye nidhamu kubwa kwenye kikosi chetu kwahiyo ni heshima kwetu kubaki naye na uzuri ni kwamba hata yeye (Maxi) ana furaha zaidi na hapa.”
Msimu uliopita ambao Maxi aliyemaliza na mabao 11, Mwanaspoti linafahamu kuwa mabosi wake walimboreshea mshahara wake pamoja na kumpa gari baada ya kuanza vyema ndani ya timu hiyo.
Kocha Gamondi akizungumzia Maxi alisema anafurahia kiwango cha kiungo wake huyo kwa kuwa ndio mchezaji anayekimbia umbali mrefu akiwa uwanjani.
Gamondi alisema kimekuwa na faida kubwa kwa kikosi chake kuwa na Maxi kutoka na nguvu yake akiwa hana mpira na wakati ana mpira kwa kutengeneza idadi nzuri kwenye idara tatu za ndani ya uwanja.
“Kuwa na Maxi kwenye timu yetu ni faida kubwa, ni mchezaji ambaye ana jitihada kubwa kuanzia mazoezini mpaka kwenye mchezo,”alisema Gamondi.
Akizungumzia kiwango cha Maxi kwenye mchezo dhidi ya timu yake ikilala kwa mabao 4-0 kocha wa Kaizer Chiefs Nasredine Nabi alisema kiungo huyo ni mmoja ya wachezaji wa Yanga waliokipa shida kikosi chake kwa kufanya kazi kubwa kwenye upokonyaji wa mpira.
“Kwenye mchezo ule alikuwa karibu kila eneo anapambana ni mchezaji ambaye anasukuma presha kubwa kwa wapinzani wakati wanautafuta mpira,” alisema Nabi
Kocha wa Union Maniema ya DR Congo iliyomuibua Nzengeli, amecheki kiwango cha staa huyo akamshauri kitu tayari kwa msimu mpya.
Papy Kimoto ambaye aliwahi kumfundisha Maxi kabla ya kutimkia Yanga, amekiri kuwa mchezaji huyo anayemfahamu sio huyu wa sasa, kwani kuna vitu vimepungua.
Akizungumza na Mwanaspoti, ameeleza kuwa baada ya kumwangalia Max katika mechi tatu mfululizo za hivikaribuni amegundua kuwa kuna kiwango cha uchezaji hakipo sawa kwake kama ilivyokuwa hapo awali.
Alisema kuwa licha ya Yanga kusumbua na kushinda michuano iliyoshiriki pre season, lakini anatakiwa aongeze utulivu hasa anapokuwa eneo la kumalizia.
“Japokuwa amefunga mabao 10 na kupata namba na kuchezea timu yenye wachezaji wazuri na wenye uzoefu mkubwa, hiyo tu inaonyesha kuwa yeye ni bora zaidi ya wale wanaobaki benchi na kocha anaona kitu ndani yake.
“Ila katika msimu uliopita na mechi tatu zilizopita alikuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi ila anakosa utulivu, ndio maana nilimshauri arudishe uwezo wake kupiga mashuti makali na ya mbali kama alivyokuwa Maniema.”
Aliongeza kuwa, “kama msimu ujao atabadilisha jambo hilo tu, basi atajiongezea thamani zaidi ya aliyonayo ndani ya kikosi hicho kwa sasa na ataweza kufunga mabao mengi.”
Staa huyo ni miongoni mwa wachezaji waliofanikiwa kupenya katika hesabu kali za kocha Miguel Gamondi tangu alipotua katika kikosi hicho msimu uliopita kutokana na uwezo alionao.
Pindi anapokuwa uwanjani unaweza kumuona Max akizunguka eneo lote japokuwa ana uwezo wa kucheza kama winga, kiungo mshambuliaji na hata eneo la ulinzi.
GAMONDI KUHUSU DUBE, MZIZE
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema ni mapema, lakini amefurahishwa na pacha iliyotengenezwa na Prince Dube wakishirikiana na Clement Mzize akiwataja kuwa wanamuofa vitu vingi uwanjani.
Wawili hao kwenye mechi tatu za kirafiki zilizochezwa na Yanga, Afrika Kusini wameanza pamoja kwenye mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Mbali na mchezo huo Yanga ilicheza na TS Galax wakishinda bao 1-0, Dube alianzia benchi huku Mzize akianza kikosi cha kwanza na mechi ya tatu ilikuwa ni dhidi ya FC Augsburg ambao pia Dube aliingia akitokea benchi.
Kwenye mechi hizo tatu washambuliaji hao kila mmoja amefunga bao moja kwenye mchezo walioanza pamoja dhidi ya Kaizer Chiefs timu hiyo ikitwaa taji baada ya ushindi wa mabao 4-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema ana kikosi kizuri na kila mchezaji anaonyesha ubora lakini amefurahishwa namna Dube na Mzize wameweza kuelewana kwa uharaka.
“Dube na Mzize wamecheza pamoja mechi zote tatu japo kuna mbili mmoja kaanzia benchi lakini mara baada ya kuwa wote uwanjani wamekuwa wakicheza vizuri kwa kuelewana,” alisema na kuongeza;
“Wawili hao bila ya kuelekezwa wamekuwa wakibadilishana upande kiwandani kwa kuingia ndani ya 18 wakitokea pembeni na wana uwezo sawa kwenye mashambulizi na kukaba wananipa vitu viwili tofauti kiwanjani.”
Gamondi alisema anaelewa juhudi za Mzize kiwanjani hasikilizi maneno ya mashabiki ataendelea kumtumia kwasababu kile anachomuelekeza anafanya huku akiweka wazi kuwa suala la kufunga hakuna mchezaji anafundishwa inatokea tu.
“Mbinu zote ninazomuelekeza anazifanya na amekuwa mchezaji ambaye anafanya mambo mengi uwananjani huwa sisikilizi nini kinasemwa naangalia nini kinafanyika na ndio maana nimekuwa nikimtumia, mechi zote tatu ameanza sababu ni anafanya kazi yake,” alisema na kuongeza:
“Mzize ni mchezaji ambaye ni nadra sana kuwa naye kikosini kwani anauwezo wa kutumia miguu yote miwili hivyo ni rahisi kwake kukaa kwenye maeneo bila kujali mguu gani atatumia wakati huo.”
Mzize alisema: “Maneno ni mengi kunihusu hasa nikikosa nafasi ya kufunga mimi pia naumia lakini napata nguvu kutoka kwa Gamondi ambaye siku zote amekuwa akiniambia mimi ni bora na natakiwa kuonyesha bila kujali ukiachana na maneno yake amekuwa akiendelea kunipa nafasi,” alisema na kuongeza:
“Nafikiri kuendelea kuaminiwa na kupewa nafasi ndio siri.”