Ahmed Ally amaliza utata wa Dulla Makabila Simba Day

MSEMAJI wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amemaliza utata juu ya  msanii wa muziki wa Singeli, Dulla Makabila kuhusu kutumbuiza katika Tamasha la Simba Day, Jumamosi, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Ahmed Ally ameliambia Mwanaspoti, mashabiki wa Simba watulie kwani klabu hiyo haikumtangaza Dulla  atatumbuiza siku hiyo na hata akiwemo kwenye orodha ya wasanii hatapewa nafasi hiyo kwa sababu tamasha hilo ni kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki wao na kama hawamtaki hawatamuweka.

Amesema hadi sasa msanii aliyetangazwa kutumbuiza siku hiyo ni Alikiba na wengine waliotawatangaza.

“Hili ni tamasha la kuwapa burudani mashabiki wa Simba, ni tamasha lao hili, sasa kama mashabiki hawamtaki msanii kwa nini tumuweke? Hatupo kuwaudhi mashabiki wetu na klabu haijamtangaza Dulla Makabila kama atatumbuiza siku hiyo, wewe umeiona hii taarifa kwenye akaunti ya Simba? Hadi sasa Simba tumewatangaza  baadhi ya wasanii watakaotumbuiza wakiongozwa na Alikiba, hiyo ya Dulla Makabila tunaiona tu mitandaoni.”

“Hata kama awekwe au asiwekwe kwenye orodha  hawezi kutumbuiza, tunawaheshinu na kuwathamini mashabiki zetu hivyo watulie tu,” amesema Ahmed Ally.

Ahmed Ally ameyasema hayo baada ya kava la  wasanii watakaotumbuiza katika tamasha hilo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii akiwemo Dulla Makabila na baadhi ya mashabiki kuibuka na kumkataa kutokana na kauli alizozitoa dhidi ya klabu hiyo.

Dulla Makabila baada ya kuona maoni ya mashabiki ya kukataliwa, amefunguka kwenye ukurasa wake wa Instagram, ameona jinsi mashabiki wa Simba wanavyomkataa kuwa mmoja wa wasanii watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo na kusema yupo njiani anaenda studio kuandaa ngoma ambayo itawafanya wamtake na kumkubali.

Imekuwa kawaida kwa Dulla Makabila kuhama timu hizo za Kariakoo na mara ya mwisho alirudi Yanga akitokea Simba na kabla ya hapo alihamia Simba akitokea yanga.

Related Posts