Alikiba: Nipo tayari kwa shoo ya viwango

KWA mara nyingine tena, mabibi na mabwana, wavulana kwa wasichana, mfalme wa muziki wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ndiye atakuwa kinara wa utoaji burudani katika tamasha la Simba Day, Agosti 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku mwenyewe akifunguka juu ya hilo.

Julai 24, akiwa Morogoro, Alikiba alitangazwa kama mtumbuizaji mkuu katika tamasha hilo la 16 huku akitoa salamu kwa mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza stendi ya zamani kabla ya safari ya kwenda hifadhi ya Mikumi kwa ajili ya uzinduzi wa Wiki ya Simba Day pamoja na utambulisho wa jezi zitakazotumika kwa ajili ya msimu ujao wa 2024/25.

Mpo tayari? Alihoji ofisa habari wa wekundu hao wa Msimbazi, Ahmed Ally kabla ya kumtangaza Alikiba huku akisema siku hiyo ya kilele, atatoa burudani ya ngoma zake zote kali ikiwemo wimbo wao maalumu ‘Mnyama’.

Tofauti na ilivyokuwa katika tamasha lililopita ambapo Alikiba pia alikuwa mtumbuizaji mkuu, safari hii imeelezwa, ‘hit maker’ huyo wa ngoma ya Fallen Angel aliyomshirikisha Bill Nas, atapewa muda wa kutosha ili kukata kiu ya mashabiki wa Simba watakaojitokeza kutazama utambulisho wa kikosi chao.

Kwa upande wa maandalizi yake binafsi kwa ajili ya shoo hiyo, Alikiba alisema kila kitu kipo sawa na yupo tayari kwa tamasha hilo.

“Mashabiki wa Simba wanatakiwa kuja kwa wingi tu maana hawana sababu ya kukosa, mimi na timu yangu tupo tayari kwa ajili ya kuwapa burudani,” alisema msanii huyo ambaye mwaka 2008 alishirikiana na R. Kelly na wanamuziki wengine wa Kiafrika kwenye mradi ambao ulifahamika kama One 8.

Kama unakumbukumbu nzuri miongoni mwa shoo kali alizofanya Alikiba kwenye Uwanja wa Mkapa ni pamoja na ile ya Simba Day iliyopita. Kwa nini? alikuwa na ngoma mbili kali ambazo zilikuwa zikifanya vizuri kwa wakati huo hivyo alienda vizuri na upepo.

Ngoma ya kwanza ilikuwa Sumu ambayo alimshirikisha Marioo huku kile kibao chake cha Mnyama ndio kikiwa cha moto, lingine lililoamsha hamasa na kufanya shauku iwe kubwa ya mashabiki kuhusu shoo hiyo hicho ndio kipindi msanii huyo alihamia upande wa pili.

Ikumbukwe Kiba alikuwa shabiki wa Yanga, hivyo ni kama walipishana na mshindani wake kwenye muzika wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz.

Kuanzia namna alivyoingia uwanjani hapo kwa mbwebwe za kifalme huku akiongozwa na Jenero wake, Mwijaku ilikuwa ya kupendeza huku akisindikizwa na madansa ambao waliunda majukwaa tofauti kama ilivyo katika matamasha mengine  makubwa. Mashabiki wa Simba walifurahia burudani yake.

Ndani ya msimu uliopita King Kiba alihusika katika matukio mawili makubwa yaliyoihusisha Simba, ukianza na tamasha lao hadi katika ufunguzi ya michuano mipya ya African Football League, ilikuwa ni hatua nyingine kwa msanii huyo kutoa burudani kitofauti zaidi, Afrika yote ilikuwa Tanzania.

Nini alifanya? Alikuwa na dakika chache kama mtumbuizaji mkuu katika ufunguzi huo kabla ya mchezo kati ya Simba dhidi ya Al Ahly, hata hivyo, alizitendea haki.

Hakutumbuiza ‘Mnyama’ ila ‘Sumu’ ilipigwa na ilikuwa shoo ya kibabe iliyofanywa ‘Live’ Kwa Mkapa.

Kiba mwenyewe alikiri katika makala yake baada ya ufunguzi ule, ilikuwa ni shoo ya tofauti sana kuanzia katika maandalizi hadi namna alivyopaswa kutumbuiza. Kiba alifanya zaidi ya kile alichotoa kwenye tamasha la Simba Day wiki chache nyuma na kuacha gumzo.   

Katika shoo mbili tofauti za Kiba zilikuwa na viwango. Je! safari hii kutakuwa na upekee gani? Huku ikielezwa atapata muda zaidi wa kukata kiu ya mashabiki wa timu hiyo wakati wakisubiri kuona chama lao likitesti mitambo dhidi ya APR ya Rwanda.

Hiki ni kitendawili ambacho Kiba na watu wake watakuwa na jukumu la kukitegua katika tamasha hilo, akifanya zaidi itakuwa ni heshima kwake na kama kiwango kikipungua basi atakuwa amewapunja mashabiki zake na wapenda burudani.

Pamoja na kwamba kutakuwa na orodha ndefu ya wasanii ambao watatumbuiza katika tamasha la Simba, msanii ambaye amekuwa akihusika karibu kila mwaka, Tunda Man anatarajiwa kuwa sehemu ya historia.

Tunda Man ni kati ya wasanii wabunifu ambao wamekuwa wakijipambanua pale wanapopata nafasi ya kufanya shoo katika majukwaa mbalimbali, mwaka jana aliingia na kufanya igizo la kunyongwa kabla ya kutumbuiza ngoma yake ya hata mfanye nini Simba hawezi kuhama.

Related Posts