Morogoro. Viongozi wa mradi wa ushirika wa wakulima wa zao la miwa katika Bonde la Kilombero mkoani Morogoro, wamewahakikishia wananchi kuwa hakutakuwa na kushuka kwa bei ya zao hilo kutokana na uhusiano mzuri kati ya wakulima na wadau wa sekta ya sukari.
Akizungumza na Mwananchi mjini Ruaha leo Alhamisi Agosti mosi, 2024, mwenyekiti wa mradi huo, Baraka Mkangamo amesema bei ya miwa haitapungua na itaendelea kuuzwa Sh108,000 kwa tani moja.
Mkangamo amesema Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alishatangaza bungeni kuwa wizara yake imetenga bajeti ya Sh7 bilioni kwa ajili ya wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero, kwa lengo la kusaidia kuandaa vitalu vya mbegu bora za miwa ili kuongeza mavuno.
“Tumekuwa tukisikia kwenye mitandao ya kijamii kwamba bei ya miwa itashuka kwa asilimia 70, huku mwanasiasa mmoja akidai hivyo, lakini hiyo si kauli ya viongozi wenu. Tuna utaratibu wa kuwasilisha mapendekezo ya bei ya miwa kwa mamlaka husika kwa sababu bei ya sasa ni Sh108,000 kwa tani moja na kuna taratibu zinazopaswa kufuatwa kwa mujibu wa mkataba,” amesema Mkangamo.
Mmoja wa wakulima wa Chama cha Ushirika wa Masoko ya Kilimo (Amcos) cha Kata ya Sanje wilayani Ifakara, Tabu Lwena, amepongeza uamuzi wa Serikali kuondoa asilimia mbili ya zuio la mapato ya wakulima wa miwa, akisema hatua hiyo imewanufaisha wakulima wengi wa bonde hilo.
Meneja wa uendeshaji wa mradi huo, Seif Mwego amesema Bonde la Kilombero lina wakulima wadogo wa miwa wanaowakilisha asilimia 90 ya wakulima wote wa miwa nchini. Amesema tangu wawekezaji walipoingia mwaka 1999/2000, uzalishaji wa miwa umepanda kutoka tani 160 hadi kufikia tani 8,500.
Hata hivyo, amesema changamoto ya tani 2,500 za miwa zilizobaki shambani kutokana na uwezo wa kiwanda kuchukua tani 6,000 pekee, itatatuliwa na upanuzi wa kiwanda cha Kilombero unaotarajiwa kukamilika mwaka ujao.