Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia siku 30 kabla ya kufungwa kwa dirisha la uombaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini Tanzania, makosa kadhaa yamebainika kufanywa na waombaji hali inayowaweka katika hatari ya kupoteza fursa hiyo.
Dirisha hilo kwa mwaka wa masomo 2024/2025 lilifunguliwa Juni 1, 2024 likitarajiwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 245,000 wakiwemo 80,000 wa mwaka wa kwanza ambapo kiasi cha Sh787 bilioni kimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo.
Baadhi ya makosa yaliyobainika ni kutokamilisha taarifa muhimu zinazotakiwa katika utumaji wa maombi hayo huku ikibainika kuna wazazi wanaojaza fomu za maombi ya mikopo kwa niaba ya waombaji.
Kufuatia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Dk Bill Kiwia amewataka wazazi kuacha kuwajazia fomu za maombi watoto wao kwa kile alichoeleza wengi wao hawana taarifa muhimu zinazohitajika hivyo kusababisha maombi kutokamilika.
Dk Kiwia amesema hayo leo Agosti 1, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema katika kipindi cha siku 60 tangu kufunguliwa kwa dirisha wamebaini kuna maombi ambayo hayakamiliki kwa sababu yanatumwa na watu wasio sahihi.
“Inawezekana mzazi anafanya kwa nia njema kabisa kumuombea mtoto wake mkopo, kinachotokea kuna taarifa ambazo anaweza asiwe nazo na hii inasababisha maombi yasikamilike na akamkosesha fursa hiyo,” amesema Dk Kiwia.
Mkurugenzi huyo amewataka wazazi kuwawezesha watoto kufikia huduma za mtandao ili waweze kutuma maombi lakini wawaache wajaze wenyewe fomu hizo kwa kuwa ndiyo wenye taarifa sahihi
Akitoa ufafanuzi wa kina kuhusu hilo, Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Dk Peter Mmari amesema kinachofanyika ni wazazi kuchanganya taarifa na wakati mwingine kushindwa kujaza taarifa sahihi zinazohitajika.
“Nitolee mfano kuna mtoto labda amefanya mtihani wa kidato cha nne mara mbili, kwenye maombi anatakiwa kuandika namba zote mbili alizowahi kufanyia mtihani sasa inatokea mzazi anaijua moja tu.
Tumefuatilia pia kwenye mfumo tumeona kuna baadhi ya taarifa ni za kawaida kabisa kwa mwanafunzi lakini sababu si yeye aliyejaza fomu ya maombi zinakuja tofauti au anayeomba anaacha wazi,” amesema na kuongeza
“Unakuta mwingine hajui aina ya mkopo, mtoto wake anataka kujiunga na shahada ya kwanza yeye anaomba mkopo wa diploma au shahada ya udhamiri, makosa ya aina hii yanafanya maombi yasikamilike na mwombaji atapoteza fursa,” amesema Dk Mmari.
Mbali na hilo changamoto nyingine iliyobainika ni kwa waombaji kutosoma mwongozo kwa ufasaha na watoa watoa huduma za steshenari kuchanganya taarifa wakati wa wanapokuwa na fomu nyingi za maombi.
“Baadhi ya waombaji hawasomi mwongozo ambao ndiyo unatoa maelekezo yote ya uombaji hali inayosababisha makosa kufanyika. Miongozo inaelekeza waombaji kuhakiki vyeti vya kuzaliwa au vya vifo kwa mamlaka husika lakini baadhi hawafanyi hivyo matokeo yake wanashindwa kuendelea na maombi.
Pia, baadhi ya watoa huduma za intaneti wanafanya kosa la kuchanganya taarifa za waombaji wanaopata huduma kwenye vituo vyao. Hapa tusisitize waombaji wajiridhishe kuwa maombi yamefanyika kwa usahihi na taarifa zimewekwa kwenye mfumo,” amesema Dk Kiwia.
Akizungumzia mwenendo wa uombaji mikopo, Dk Kiwia amesema hadi sasa wamepokea maombi 40,000 kati ya hayo 25,000 yameshafanyiwa kazi na bodi hiyo inaendelea na uchakataji.
“Niwasisitize waombaji wazitumie vyema siku 30 watume maombi katika muda uliopangwa hakutakuwa na muda wa kuongeza kwani mfumo wetu hauturuhusu.
Pia, nitumie fursa hii kuwaarifu wale wanaotaka kuomba ufadhili kupitia Samia Scholarships, dirisha litakuwa wazi kuanzia Agosti 3, makundi mengine yote tulishafungua dirisha litafungwa Agosti 31,2024,” amesema Dk Kiwia.
Katika hatua nyingine amesema HESLB kupitia kampeni ya Fichua imeweza kubaini wanufaika 234 wasiorejesha mikopo wenye madeni ya thamani ya Sh1.34 bilioni na wameshawasilishiwa hati za madeni baada ya kufichuliwa na watu wao wa karibu.