Getrude Mongella awaasa vijana waliotupa maadili, uzalendo

Dar es Salaam. Ili kuenzi kazi aliyoifanya muasisi wa Taifa la Tanganyika na Zanzibar, Hayati Mwalimu Julius Nyerere imeshauriwa kiandikwe kitabu, kitakachokuwa na mwongozo kwa vijana kujua misingi ya uzalendo kwa nchi yao.

Hayo yamesemwa na Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika na mwanaharakati wa haki za wanawake nchini, Balozi Getrude Mongella leo Agosti Mosi, 2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni za mbio za baiskeli zilizolenga kumbukizi ya Baba wa Taifa.

Amesema Septemba 14 ni kumbukumbu ya Hayati Mwalimu Nyerere, hivyo kutokana na misingi aliyokuwa anaisimamia wakati wa uongozi wake ni vyema kiandikwe kitabu, ili vijana wakisoma waenzi kazi yake kwa vitendo.

Balozi Mongella amesema Nyerere alipinga ujinga, umaskini na maradhi;

“Alianzisha ujamaa ili jamii ishirikiane kupinga umaskini kwa kufanya kazi kwa umoja, alipenda demokrasia ndiyo maana zamani zilianzishwa hadi shule za watu wazima ili kuwafanya wawe na uhuru wa kuandika na kusoma, afya alikuwa mmoja wa watu wanaozingatia mazoezi, ndio maana wana michezo mbalimbali wanaenzi hilo,” amesema na kuongeza;

“Mchezo wa baiskeli wana kampeni yao, ambapo wataanza kuendesha kuanzia Dar es Salaam hadi Butiama Septemba 29 hadi Novemba 13 watapita katika mikoa mbalimbali, hivyo nawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo ambalo litajenga afya zao.”

Mbunge huyo wa zamani, alikuwa na uzoefu wa Hayati Mwalimu Nyerere, kwani kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 10, mwaka 1955 alikwenda kuonana na Nyerere katika ziara yake ya Ukerewe ambayo ilikuwa ya kupigania uhuru.

“Kilichonivuta wakati huo kwenda Ukerewe kumuona Mwalimu Nyerere, nilikuwa namsikia baba yangu akimsimulia kwamba ni shujaa wa kupigania uhuru, sasa nikawa najiuliza atamshinda mzungu ambaye alikuwepo eneo hilo, ambaye alikuwa anaogopwa na alifunga mbwa mkali, baada ya kufika na kusikiliza hotuba yake, niliamini maneno ya mzee wangu.

“Baada ya kukua nilifanikiwa kufanya naye kazi, alizingatia muda kufika mapema eneo la tukio kwenye upakuaji wake wa chakula, alikuwa anapakua kidogo tofauti na wengine, ndio maana nasema kikiandikwa kitabu kitawafunza vijana, kujua wanapaswa kufanya vitu gani waishi muda mrefu.”

Jambo lingine alilolizungumzia ni maadili ya viongozi wa zamani ambao walikuwa na nia ya kulikomboa taifa, akitofautisha na mabadiliko ya sasa ambapo baadhi yao, wameingiwa na tamaa ya kutanguliza maslahi yao.

“Nyerere alikuwa na hekima na muumini wa kusali, aliwahi kusema naingia kanisani kama Julius Nyerere na siyo cheo changu, hivyo viongozi wa nafasi mbalimbali na dini zao, waingie kanisa kwa imani na mioyo na siyo cheo, watapata hekima ya kuwaongoza watu kwa njia sahihi,” amesema Mongella.

Mkurugenzi wa Vodacom Foundation, Zuweina Farah amesema kilichowashawishi tangu mwaka jana kudhamini kampeni ya waendesha baiskeli ni mambo matatu ambayo ni elimu, afya na kupinga maradhi.

“Nitoe wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kushiriki zoezi hilo, watakapokuwa wanapita barabarani kwenye mikoa mbalimbali, watajifunza mambo ya mazingira na uoto wa asili, pia watajenga afya zao kwani kuendesha baiskeli ni moja ya zoezi zuri,” amesema.

Mkuu wa msafara wa waendesha baiskeli, Gabriel Landa amesema msafara huo utaanza  Septemba 29 hadi Oktoba13, ambapo watapita mikoa 12, lengo ni kuwapa nafasi wananchi kuchangia kampeni yao ya kununua madawati ya kutoa katika shule zenye uhitaji.

“Tulianza kampeni hiyo, mwaka 2010 tumekuwa tukiboresha vitu mbalimbali mfano mwaka jana zilishiriki nchi kama Kenya, Congo, Malawi, Rwanda, Burundi, ambapo kwa mwaka huu zimeongezeka Zimbabwe na Namibia.

“Watanzania wakijitoa kwa wingi watakuwa wamemuenzi baba wa taifa kwa kuchangia elimu kwa maana ya kuwafanya watoto wasome katika mazingira sahihi, tukifika Oktoba 13 siku inayofuata itakuwa ndio ya kumbukumbu ya kifo chake, ambayo tutaitumia kutoa mchango huo,” amesema.

Related Posts