Iran yaapa kulipa kisasi kwa Israel mauaji ya bosi wa Hamas

Tehran.  Ikiwa ni siku moja imepita tangu yalipotokea mauaji ya kiongozi mkuu wa kisiasa wa Kundi la Hamas la Palestina, Ismail Haniyeh mjini Tehran, sasa Iran imetangaza kuishambulia Israel ikiwa ni hatua ya kulipa kisasi.

Kwa mujibu wa Hamas, Haniyeh na mmoja wa walinzi wake waliuawa alfajiri ya jana Jumatano Julai 31, 2024 baada ya jengo walilokuwa wakiishi kuvamiwa na kushambuliwa.

Kutokana na mauaji hayo, Israel inanyooshewa kidole kuhusika ingawa haijatoa taarifa kuhusu tukio hilo.

Hata hivyo, Tovuti ya Times of Israel imemnukuu Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei kuamuru shambulio dhidi ya Israel.

Khamenei na maofisa wengine wa Iran wameapa kujibu mapigo licha ya kwamba haijaelezwa ni lini watatekeleza mashambuzi hayo.

Hata hivyo, ikiwa Iran itatekeleza shambulio hilo itakuwa si mara ya kwanza, kwani Aprili 14, 2024, Iran iliishambulia Israel kwa makombora takribani 300 baada ya Israel kudaiwa kushambulia ubalozi wake uliopo Damascus na kuua makamanda wa Iran.

Taarifa zaidi inasema ikiwa kama sehemu ya amri hiyo, maofisa hao wamesema Khamenei amewaambia makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Jeshi la Iran kuandaa mipango ya mashambulizi.

Vilevile kutokana na tuhuma hizo, Israel haijazungumzia tukio hilo, huku kwa upande mwingine vita vyake na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza vilivyoanza Oktoba 7, 2023 kuendelea.

Pia, wingu jeusi ukanda wa Mashariki ya Kati linazidi kutanda baada ya shambulio la Jeshi la Israel (IDF) huko Beirut, Lebanon kumuua kamanda mkuu wa kundi la Hezbollah.

“Siku zenye changamoto zinakuja, lakini akaapa kuwa nchi hiyo iko tayari kwa kila hali na itakabiliana na hali ngumu, na uchokozi wowote dhidi yao,” Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameonya katika hotuba yake Jumatano jioni.

Related Posts