BAADA ya kupewa mkono wa kwaheri na Kagera Sugar, Ally Ramadhan ‘Kagawa’ ameziingiza vitani timu nne zikiwemo Geita Gold na Ken Gold zikiwania kupata huduma yake kwa msimu ujao.
Kagawa ni miongoni mwa wachezaji 10 walioachwa na Kagera Sugar kwenye usajili unaoendelea baada ya kumaliza mkataba, wengine ni Gasper Mwaipasi, Abiud Mtambuku, Dickson Mhilu, Saidy Natepe, Appolinaire Ngueko, Mbaraka Yusuph, Ally Nassoro ‘Ufudu’, Alain Ngeleka na Moubarak Amza.
Kagawa aliyedumu klabuni tangu mwaka 2017, alisema yuko kwenye mazungumzo na timu nne baada ya kutoka Kagera Sugar, ambazo ni Geita Gold, Ken Gold, Fountain Gate na Mtibwa Sugar, bado hajaamua akiendelea kuangalia ofa nzuri kwake.
Alisema timu zote nne zinajaribu kumshawishi na Geita Gold na Mtibwa Sugar zilizoshuka kutoka Ligi Kuu zikijiandaa kucheza Ligi ya Championship zinahitaji akawe sehemu ya vikosi vyao ili kurejea Ligi Kuu, huku Fountain Gate na Ken Gold zikipambana kumbakisha Ligi Kuu.
“Nimemaliza mkataba wangu wa miaka miwili na Kagera Sugar ndiyo maana tumeachana na kuagana vizuri kwa sasa nipo sijapata timu ya kuitumikia msimu ujao lakini naendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya timu,” alisema Kagawa na kuongeza;
“Kuna timu nne, Geita Gold, Ken Gold, Fountain Gate na Mtibwa Sugar zote zimenifuata kunihitaji lakini hadi sasa hatujafikia makubaliano, mazungumzo yanaendelea mambo yakitiki tutajulishana.”