Simiyu.Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemuhukumu kwenda jela miaka 15 Katibu wa Chama cha Ushirika cha Msingi (Amcos) Kijiji cha Kidema, Richard Nchemba baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya uhujumu uchumi.
Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Agosti Mosi, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Enos Misana baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka katika Kesi ya uhujumu uchumi namba 1/2023.
Katibu huyo alifikishwa mahakamani hapo Januari 5, 2023 akishtakiwa kwa makosa mawili, la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu wa fedha kinyume na Kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2019, kikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura 200 Marejeo ya mwaka 2019.
Kosa la pili anashitakiwa kwa wizi wa fedha akiwa kama wakala wa kampuni ya ununuzi wa zao la pamba kinyume na Kifungu cha 265 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni za adhabu Sura 16 Marejeo ya Mwaka 2019.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wilaya ya Maswa, Bahati Madoshi ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitoa zaidi ya Sh1.2 milioni (Sh1,228,000) kwenye akaunti ya kidema Amcos na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi badala ya kulipa ushuru kwenye akaunti ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU 2018 LTD).
Baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia, Mahakama imempa nafasi ya kujitetea na amesema wakati ametoa fedha hizo benki kwenye akaunti ya Kidema Amcos, ghafla alivamiwa na Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya kununua pamba ya Bilchard (jina halikutajwa) akamnyang’anya fedha hizo na kutokomea nazo.
Mahakama ilipomtaka mshitakiwa kuthibitisha hakuweza kuleta ushahidi ndipo akatiwa hatiani kutumikia kifungo cha miaka 15 jela.