Kuwa Sehemu ya Mabadiliko – Mbio za Baiskeli za Vodacom Twende Butiama 2024

Tanzania inapoelekea kuadhimisha miaka 25 tangu kufariki kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Vodacom Tanzania na Klabu ya Baiskeli ya Twende Butiama wametangaza kufunguliwa rasmi kwa usajili wa mbio za baiskeli za Twende Butiama Mwaka 2024.

Mbio hizo, zitakazofanyika kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 14, zinaadhimisha urithi wa Baba wa Taifa kupitia uendeshaji baiskeli, shughuli za kijamii, na hisani.

Mbio za Twende Butiama zilianzishwa mwaka 2019 na kikundi cha waendesha baiskeli, ili kuadhimisha upendo wa Mwalimu Nyerere wa kuendesha baiskeli na maono yake kimaendeleo katika maeneo matatu muhimu ambayo ni elimu, afya, na utunzaji wa mazingira ambayo yanaweza kuwasaidia Watanzania kupiga hatua kijamii na kiuchumi.

“Tunayofuraha kubwa kufungua rasmi usajili wa Vodacom Twende Butiama Cycling Tour 2024.

Mwaka huu hatuadhimishi tu kumbukumbu ya Baba wa Taifa bali pia tunalenga kuleta mabadiliko yanayodumu kwa muda mrefu.

Washiriki watajumuika katika kampeni kuhusu utunzaji wa mazingira, kuboresha mazingira ya kujifunzia, na kusaidia katika upatikanaji wa huduma za afya kwa wote kupitia kambi za matibabu.

Tunawakaribisha waendesha baiskeli wa ngazi zote kutoka ndani na nje ya Tanzania kujiunga nasi kwenye tukio hili la siku 14 na kufikia zaidi ya Kilomita 1500 katika mikoa 12 nchini,” alisema Gabriel Landa, Mwanzilishi wa mbio za baiskeli za Twende Butiama.

Kwa mwaka wa pili mfululizo Vodacom Tanzania imekua mdhamini mkuu wa mbio hizi na walielezea dhamira yao katika kufikia malengo ya mwaka huu. Mwaka jana, kwa kushirikiana na Twende Butiama, walifanikiwa kupanda miti zaidi ya 6000, na kutoa huduma za afya kwa watu zaidi ya 3200 katika wilaya tatu ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara.

Pia, tukio hilo liliambatana na utoaji wa jumla ya madawati 610 katika shule 13 za msingi. Juhudi hizi zinaendana na malengo ya Vodacom Tanzania ya kuwawezesha watu na kulinda ustawi wa sayari yetu.

“Mwaka huu, tunajivunia kuendelea kuwa sehemu ya jambo hili linalochangia kuleta mabadiliko Chanya kwenye jamii.

Mbio za mwaka 2024 zimepanua wigo, kujumuisha mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na kambi za matibabu zitakazohusisha uchunguzi na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kwenye mikoa 12 nchini.

Tunawahimiza waendesha baiskeli wote wa umbali mrefu na mfupi kujisajili na kuungana nasi kufanikisha jambo hili. Hii ni pamoja na wadau wengine na wapenda maendeleo walio tayari kushirikiana nasi,” alisema Bi. Zuweina Farah, Mkurugenzi wa Mahusiano na Vodacom Tanzania Foundation.

Gertrude Mongella, Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (kushoto), akizungumza wakati wa uzinduzi wa msafara wa Vodacom Twende Butiama Mwaka 2024 zitakazoanzia jijini Dar es Salaam Septemba 28 na kuisha Oktoba 14 katika Kijiji cha Mwitongo, Butiama alikozaliwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kushoto kwake ni Mkuki Bgoya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota wakiwa katika tukio hilo lililofanyika tarehe 1 Agosti 2024 jijini Dar es Salaam likiwa na lengo la kusaidia jamii kuboresha elimu, afya, na mazingira wakati wa msafara huo utakaochukua siku 14.

Zuweina Farah (kulia), Mkurugenzi wa Mahusiano Vodacom na Vodacom Tanzania Foundation, akizungumza wakati wa uzinduzi wa msafara wa Vodacom Twende Butiama Mwaka 2024 utakaoanzia jijini Dar es Salaam Septemba 28 na kukamilika Oktoba 14 katika Kijiji cha Mwitongo, Butiama alikozaliwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wengine kuanzia kushoto ni Gertrude Mongella, Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuki Bgoya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota, na Gabriel Landa, Mwanzilishi wa Twende Butiama wakiwa katika tukio hilo lililofanyika tarehe 1 Agosti, 2024 jijini Dar es Salaam.

Related Posts