Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Geita, imetengua hukumu ya adhabu ya Mahakama ya Wilaya ya Bukombe iliyomhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Kulwa Makoye.
Alihukumiwa baada ya kukiri makosa ya kumteka na kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 14, kutokana na upungufu wa kisheria.
Aidha imebatilisha na kufuta hukumu hiyo iliyotolewa dhidi ya Kulwa, kutokana na mahakama hiyo ya chini kukosea kisheria kumtia hatiani ambapo mahakama hiyo imebaini mshtakiwa hakuelewa kikamilifu mashtaka dhidi yake.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya hakimu aliyesikiliza shauri hilo awali katika mahakama ya chini, kutokuandika kwa usahihi alichokieleza Kulwa wakati anakiri makosa hayo mahakamani.
Pia, imeagiza hati ya kutokuwa na hatia iwasilishwe dhidi ya Kulwa na kesi iendelee pale ilipoishia kabla ya kukiri kosa na kufanya usikilizwaji wa awali na kuendelea na kesi hiyo mbele ya hakimu mwingine.
Uamuzi huo umetolewa jana Jumatano, Julai 31, 2024 na Jaji Graffin Mwakapeje, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo namba 16472 ya mwaka 2024, iliyotokana na kesi ya jinai namba 9690/2024 iliyosikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe.
Jaji ameeleza baada ya kukagua kumbukumbu, ni dhahiri Kulwa hakuelewa kikamilifu mashtaka dhidi yake na zaidi ya hayo, hakukuwa na ushahidi wowote wa kupendekeza kwamba shtaka hilo lilielezwa vya kutosha, wala hakukiri hatia kwa kila kipengele cha shtaka hilo.
Kulwa alishtakiwa na kutiwa hatiani kutokana na maelezo yake mwenyewe ya kukiri makosa ya utekaji na ubakaji kwa mujibu wa kifungu cha 134 na 35; na 130(1)(2)(e) na 131(1) ya Kanuni ya Adhabu.
Katika kila kosa la alihukumiwa kifungo cha miaka mitano na kosa la pili kifungo cha miaka 30 jela, adhabu ambazo zilitolewa kwa pamoja.
Katika mahakama hiyo Kulwa alikabiliwa na kosa la kumteka na kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14, makosa anayodaiwa kutenda kati ya Februari na Machi 2024.
Alidaiwa kutoroka na binti huyo na kuishi naye kama wamefunga ndoa katika Kijiji cha Buntubili Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na baada ya uchunguzi wa kimatibabu, Kulwa alikamatwa na kukiri makosa hayo ambapo alipewa adhabu hiyo ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Baada ya hukumu hiyo, Kulwa alikata Rufaa mahakama hiyo akiwa na hoja tano ambazo ni Mahakama iliyosikiza ilikosea kisheria kumtia hatiani kwa kutumia ombi lake la hatia ambalo lina kutoelewana na kutatanisha.
Nyingine ni mahakama ilikosea kisheria kumtia hatiani kwanini alikiri hatia, kwani yeye na binti huyo waliishi kama mume na mke na hata wazazi walijua kuwa amemuoa binti yao na alitakiwa kulipa Sh1 milioni ambazo alikuwa akiendelea kulipa.
Sababu nyingine ni mahakama ilikosea kisheria kumtia hatiani bila upande wa mashtaka kuleta mashahidi kuthibitisha kweli alimteka na kumbaka binti huyo.
Katika rufaa hiyo Kulwa alijitetea mweneywe, huku upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) ukiwakilihwa na Wakili wa Serikali, Luciana Shabani.
Wakili huyo alidai kwa kiasi fulani anaunga mkono rufaa hiyo na akatetea hoja ya kwanza kwa vile alikuwa na maoni kwamba hiyo inatosha kuondoa rufaa hiyo.
Alieleza mshtakiwa anapofikishwa mahakamani na kusomewa shtaka, utaratibu unamtaka mshitakiwa kujibu hatia au kutokuwa na hatia na iwapo mshtakiwa atakana hatia, kesi hiyo inaendelea kusikilizwa na mashahidi kutoka pande zote mbili.
Wakili alifafanua iwapo mshtakiwa anakiri hatia, ukweli unathibitishwa, na kuwezesha mahakama kuendelea na hatia na hukumu na kudai katika kesi ambapo mshtakiwa anajibu hatia, ombi hilo linapaswa kuwa lisilo na shaka na lisilo na utata, huku akitetea hoja yake kwa kunukuu kesi iliyowahi kutolewa uamuzi na mahakama ya rufaa.
Amedai mshtakiwa alikabiliwa na mashtaka mawili ya utekaji nyara chini ya kifungu cha 135 na 138 na kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu.
Huku akinukuu majibu ya Kulwa kwenye kosa la kwanza “Ni kweli nilimtorosha binti tajwa “na kosa la pili “Ni kweli nilifanya naye tendo la ndoa/kujamiana na binti tajwa mwenye umri wa miaka 14.”
Wakili alikuwa na maoni kwamba kauli hizi zilifanya kutokidhi vigezo vya ombi halali kuhusu makosa yaliyoshtakiwa, ombi hilo lilikuwa la usawa na halieleweki na hakimu wa mahakama alikuwa ameandika taarifa ambazo Kulwa hakutoa kama inavyotakiwa.
Wakili huyo alidai kisheria inahitaji ukweli kutaja viambato vya kosa na kuwa ilipaswa kubainishwa mwathiriwa alikuwa na umri chini ya miaka 14 na alichukuliwa kutoka kwa wazazi wake bila idhini yao kwa madhumuni ya ndoa.
Alidai umri wa mwathirika wa tukio hilo haukutajwa na kuhitimisha kuwa upande wa mashtaka ulitakiwa kuleta mashahidi ili kusikiliza shauri hilo kwa ukamilifu kwa kuwa ombi hilo halikukidhi viwango vinavyotakiwa.
Kutokana na sababu hizo aliomba hukumu kuwekwa kando na kwamba kesi ianze upya katika mahakama yenye mamlaka husika, ambapo baada ya uwasilishaji huo, Kulwa hakuwa na chochote cha kujibu katika maelezo yake.
Baada ya kusikiliza mawasilisho hayo Jaji Mwakapeje alianza kwa kueleza anaanza kwa kuangalia sababu za kukata rufaa kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 228 (1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, inasema:
“(1) Msingi wa shtaka utaelezwa kwa mtuhumiwa na mahakama na ataulizwa kama anakubali au anakataa ukweli wa shitaka.
“(2) Endapo mtuhumiwa atakubali ukweli wa shtaka, kukiri kwake kutarekodiwa iwezekanavyo katika maneno anayotumia, na hakimu atamtia hatiani na kutoa hukumu au kutoa amri dhidi yake isipokuwa kama itaonekana kuwa sababu ya kutosha kinyume chake.”
Jaji alieleza endapo mshtakiwa atatiwa hatiani kwa kukiri kwake mbele ya mahakama, kanuni inaamuru haruhusiwi kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Alieleza hata hivyo, anayo haki ya kupinga adhabu hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 360 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Huku akinukuu shauri lililotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani, Jaji alieleza pamoja na kanuni iliyowekwa katika kifungu hicho imeweka tofauti kuhusu kutumika kwa kifungu hicho, ambapo mtu anaruhusiwa kukata rufaa kwa maelezo yake mwenyewe ya hatia.
Katika kesi ya Laurent Mpinga dhidi ya Jamhuri (1983), iliyotajwa na Mahakama ya Rufani kwa kibali katika kesi ya Kalos Punda dhidi ya Jamhuri katika Rufaa ya Jinai 153/ 2005, mambo kadhaa yaliwekwa kwa mtu kukata rufaa dhidi ya hatia kwa ombi lake mwenyewe la hatia.
“Kwamba hata kwa kuzingatia ukweli uliokubaliwa, ombi hilo halikuwa kamilifu, lisiloeleweka au halijakamilika, na kwa sababu hiyo, mahakama ya chini ilikosea kisheria kulichukulia kama ombi la hatia.
“Kwamba mrufani alikiri hatia kutokana na makosa au kutoelewa.Kwamba shtaka lililowekwa kwenye mlango wa mrufani halikuonyesha kosa lolote linalojulikana kwa sheria na kwamba juu ya ukweli uliokubaliwa, mrufani hakuweza, kisheria kutiwa hatiani kwa shtaka la kosa.”
Alieleza hati ya mashtaka ilisomwa kwa lugha ya kiswahili ambapo alikiri makosa yote mawili na baada ya mahakama kurekodi maelezo ya Kulwa kukiri wakili wa mashtaka alitoa maelezo ya onyo ya mshtakiwa na fomu ya matibabu namba tatu (PF3).
Jaji alieleza kumbukumbu za mwenendo wa shauri hilo zinaonyesha Kulwa alialikwa kueleza usahihi na ukweli na alirekodiwa kama ifuatavyo.
” Nakubaliana na maelezo yaliyosomwa pamoja na vielelezo cha kwanza na cha pili vya Jamhuri ni kweli tupu.”
Jaji alieleza kwa kuzingatia yaliyotangulia, suala la kuzingatia ni iwapo ombi la mrufani lilikuwa la usawa na ilikidhi masharti ya kesi tajwa juu na kuwa swali linalofuata mara moja ni je Kulwa, katika taarifa kama hizi, anaweza kuchukuliwa kuwa amekiri hatia katika mazingira hayo?
Jaji akinukuu uamuzi wa kesi uliotolewa na Mahakama ya Rufani, ilielezwa katika kesi yoyote ambayo hatia inaweza kuendelea kwa ombi la hatia, inafaa zaidi siyo tu kwamba kila sehemu ya shtaka inapaswa kuelezewa kwa mshtakiwa lakini atatakiwa kukiri au kukataa kila sehemu ya kosa.
Ilielezwa anachosema kinapaswa kurekodiwa na katika fomu ambayo itaridhisha mahakama ya rufaa kwamba alielewa shtaka hilo kikamilifuna kukiri hatia kwa kila kipengele chake bila shaka…(Msisitizo umetolewa).
“Kwangu mimi, ombi la mrufani halikunakiliwa ipasavyo katika maneno yake kamili na hiyo hairidhishi vya kutosha kuthibitisha kwamba mrufani alielewa shtaka kikamilifu,” alieleza Jaji.
“Kwa heshima, neno “supra” lililoingizwa si neno la Kiswahili na halikujumuisha ombi halali, ni dhahiri kwamba alichoeleza mrufani hakikuandikwa kwa usahihi badala yake, ulikuwa ni msemo ulioletwa na hakimu,” amesema.
Jaji alieleza katika shtaka la pili, ombi la mrufani lilielezwa kama ifuatavyo:”Ni kweli nilifanya tendo la ndoa/kujamiiana…” Baada ya uchunguzi wa kina wa maneno yaliyotumika, tafsiri mbalimbali zinaonyesha tofauti kubwa.
Alieleza katika tathmini yake ya kitaalamu, ombi la mrufani katika mahakama ya awali lilishindwa kukidhi vigezo vilivyoainishwa katika aya ya (2), (3), na (5) kama ilivyobainishwa katika kesi ya Michael Adrian dhidi ya Jamhuri (supra).
“Kulingana na uchunguzi uliotajwa hapo juu, nakubaliana na hoja ya Wakili Luciana kwamba maombi ya mrufani yalikuwa na utata. Kwa kuzingatia kwamba hii pekee inatosha kushughulikia rufaa ya sasa, sitaingia katika misingi iliyobaki ya rufaa,” amesema.
Baada ya kutengua hukumu hiyo alielekeza Kulwa atakapopatikana na hatia muda aliotumikia kama mfungwa uzingatiwe.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.