Matatizo ya ‘automatic gearbox’ yanatibika, soma hapa

Watu wengi wanaokumbana na matatizo kwenye Automatic gearbox huishia kubadili ‘gearbox’ zao. Mfano wa matatizo hayo ni ‘gearbox’ inagoma kupokea gia au inachelewa kubadili, injini kuendelea kuzunguka katika RPM kubwa hata baada ya kukanyaga breki, ‘gearbox’ kukwama katika ‘Neutral’.

Mengine ni kutopata vizuri gia ya kurudisha gari nyuma (reverse gear), mtikisiko wakati wa kubadili gia na mengine yanayofanana na hayo. Lakini je ni kweli kwamba ‘automatic gearbox’ hazitengenezeki?

Kwanza kabisa ni lazima ujue kwamba urefu wa maisha ya ‘automatic gearbox’ unatakiwa kuwa sawa na urefu wa maisha ya gari kama tu unaitunza vizuri ‘gearbox’ yako ingawa yanaweza kuwepo matengenezo madogo madogo kama kubadili solenoids, valves, filter, Torque converter au valve body yote.

Asilimia kubwa ya matatizo ya kuhama gia kwenye ‘automatic gearbox’ huwa yanazaliwa kutokea kwenye valve body au Torque converter (Hii sitaijadili sana japo na yenyewe inaweza kubadilishwa kama imeleta shida).

Katika ‘valve body’ ambayo mara nyingi hupatikana katika ‘oil pan’ huwa kunakuwa na ‘solenoids’ ambazo baadhi huwa zimeunganishwa na ‘valves’ moja kwa moja au huwa zimewekwa katika uelekeo wa valvu. Gearbox inaweza kuwa na ‘shifting solenoids’ mbili mpaka sita.

Ingawa pia zinaweza kuwepo ‘solenoids’ zingine kama ‘Lock-up solenoid, TCC solenoid na pres¬sure solenoid’. Pia wakati mwengine unaweza kukutana na ‘solenoids’ katika jumba la ‘automatic gearbox’, mfano katika baadhi ya gearbox, TCC solenoid imefungwa upande wa nje kwenye.

Kazi ya hizi valves na solenoids huwa ni kuruhusu au kuzuia mwenendo wa Automatic transmission fluid (ATF) kwa ajili ya mizunguko ya gia, lock up ya Torque convertor, regulating transmission pressure n.k.

Hivyo kama kuna tatizo lolote mfano solenoid kufa, kutopokea umeme unaotakiwa, valve kuwa chafu au valve kuisha inaweza kupelekea matatizo hasa katika kubadili gea kwenye automatic.

Kuharibika kwa hizi solenoids mara nyingi husababishwa na gearbox kupata joto kupita kiasi ambalo husababishwa na vitu mbalimbali kama joto kutoka kwenye clutches, kutumia ATF ambayo haijeelekezwa na watengenezaji kwa gearbox yako, kutumia ATF muda mrefu bila kuibadili na kuharibika kwa Torque converter.

Haya matatizo yanaweza kurekebishika na kitu kizuri zaidi ni kwamba matatizo mengi ya automatic gearbox unaweza kuyapima kwa kutumia kifaa kiitwacho OBD II scanner. Pia ni vizuri zaidi ukathibitisha kwa kuipima hiyo solenoid baada ya kupata majibu kutoka kwenye OBD II scanner.

Sasa changamoto iliyopo watu wengi wakipata matatizo hayo huambiwa na mafundi funga gearbox mpya. Sawa hilo linaweza kutatua tatizo lakini mtu ataingia gharama kubwa na pia hakutakuwa na uhakika kwenye hiyo gearbox ukizingatia kwamba imeshatumika kutoka kwenye gari lingine.

Hivyo vifaa vilivyotajwa hapo juu ni rahisi zaidi kuvibadili na siyo gharama (hata kama utabadili valve body yote) ukilinganisha na kubadili gearbox yote.

Related Posts