Mwanza. Watu watano wamefariki dunia katika matukio matatu tofauti akiwamo mtoto wa miaka mitatu, huku wivu wa mapenzi ukitajwa kuchangia mauaji hayo.
Matukio hayo yamebainishwa leo Alhamisi Agosti Mosi, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema tukio la kwanza lilitokea Julai 28, 2024, baada ya mtoto wa miaka mitatu, Lukonya Kisumo kuuawa kwa kunyongwa shingoni na baba yake mzazi, Kisumo Emmanuel (38).
Mutafungwa amesema muuaji huyo aliyekuwa akimtuhumu mkewe (jina linahifadhiwa) kuzaa na mwanamume mwingine, alichukua mwili wa mtoto huyo na kuutupa katika kisima cha maji kilichopo kwenye shamba la mpunga, kisha naye kujinyonga juu ya mti.
“Wakati polisi wanamtafuta mtuhumiwa, walimpata akiwa ameshafariki dunia huku mwili wake ukiwa umening’inia kwenye mti ndani ya shamba la jirani yake umbali mfupi kutoka alipokuwa anaishi.
“Tayari uchunguzi wa miili hiyo umefanyika na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko,” amesema Mutafungwa.
Katika tukio lingine, Kamanda Mutafungwa amesema Mkazi wa Kisamba Kata ya Lubugu wilayani Magu mkoani humo, Fednand Mabula (41) alimuua mke wake, Christina Kisinza (40) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni kisha naye kujinyonga baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Kamanda Mutafungwa, amesema Fednand anadaiwa kumuua mke wake Julai 30, 2024 saa 4:30 usiku katika Kitongoji cha Nela wilayani humo wakiwa wamelala chumbani kwao huku chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
“Baada ya kumtuhumu mke wake kuwa ana mahusiano na mwanamume mwingine, alimuua na kutoweka kwenda kusikojulikana, wakati polisi wakiendelea kumsaka walipewa taarifa kutoka kwa wananchi kuna mwili wa mwanamume unaning’inia juu ya mti, walipofika walikuta mtuhumiwa huyo akiwa ameshafariki dunia,” amesema Mutafungwa.
Wakati huohuo, Jeshi hilo linamsaka Mkazi wa Kijiji cha Isegeng’e Kata ya Mwakiliambiti Wilaya ya Kwimba mkoani humo, Benjamini Masanye (29) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Veronica Ndabile (23) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Kamanda Mutafungwa amesema mtuhumiwa anadaiwa kutekeleza mauaji hayo Julai 31, 2024, saa 2:30 usiku.
Amesema Veronica akiwa amelala nyumbani kwa wazazi wake, alivamiwa na mumewe kisha kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya mabegani, shingoni na miguuni.
“Mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mama mkwe wake aitwaye, Limi Nyanda na kuingia kwenye chumba ambacho Veronica alikuwa amelala na kumuua. Baada ya kutekeleza unyama huo alimpigia simu baba wa marehemu na kumueleza yeye ndiye ametekeleza mauaji hayo.”
“Alimweleza baba mkwe wake alitekeleza mauaji hayo kwa sababu (wakwe) walimkatalia asimchukue na kwenda kuishi naye. Polisi tunaendelea na msako wa kumkamata mtuhumiwa ili akakabiliane na mkono wa sheria, tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano utakaowezesha kumkamata,” amesema.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo linawashikilia wafanyabiashara na wakazi wa Mwanza ambao ni Majani Masagati (47), Kiruma Lucas (31), Sharifu Juma (29) na Selemani Mbuga (39) kwa tuhuma za kurusha sakafuni fedha mbalimbali zikiwemo noti za Tanzania na Dola kinyume cha sheria.
Kamanda Mutafungwa, amesema watuhumiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2024 katika ukumbi wa sherehe wa Kwa Tunza Beach wilayani Ilemela mkoani humo walipokuwa wakitoa zawadi kwenye harusi ya rafiki yao, Robert Shija.
“Picha mbalimbali zikionyesha tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii Julai 18, 2024, katika harusi hiyo baadhi ya wageni waalikwa walihusika katika utoaji wa zawadi kwa kuzirusha sakafuni kisha fedha hizo kuzolewa na kuwekwa kwenye kikapu.”
“Kitendo hicho kilionyesha taswira mbaya katika suala zima la utunzaji wa fedha za Kitanzania ambazo ni tunu ya Taifa. Polisi kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tayari tumewakamata watuhumiwa wote na tunaendelea kufanya mahojiano nao,” amesema kamanda huyo.
Kamanda huyo ameenda mbali na kuiomba jamii kujiepusha na matukio ya kikatili, kujichukulia sheria mkononi na kuzingatia utunzaji sahihi wa fedha kwa kile alichodai kuchafua fedha kwa makusudi, kuzikanyaga, kuzichora, kuzichana na kuzihifadhi kama uchafu ni kinyume cha sheria.
Walichokisema daktari, askofu
Kuhusu matukio ya mauaji, Mwananchi imezungumza na wanasaikoloajia kupata mitizamo yao na kile kinachosababisha kutendeka kwake.
Mwanasaikolojia na Daktari wa Binadamu mkoani Mwanza, Jacinta Mutakyawa amesema mauaji hayo yanachangiwa na ongezeko la tatizo la afya ya akili, malezi mabovu, ubinafsi na wanandoa kukosa maarifa ya kukabiliana na changamoto.
Dk Jacinta ameitaka jamii hususan wanandoa kupima afya ya akili kabla ya kuchukua uamuzi wa kuanza kuishi pamoja ili kuepusha vitendo vya ukatili wa kijinsia na mauaji pindi mmojawapo anapoanza kuonyesha madhaifu yake na mwenzake kushindwa kuyahimili.
“Watu wanaingia kwenye mahusiano hadi ndoa bila kupata taarifa sahihi kuhusiana na wenza wao, unakuta mwingine alishapitia changamoto lukuki kabla ya kuoa ama kuolewa, sasa mkishaanza kuishi pamoja ukweli ukafahamika ama kukatokea changamoto na mmoja asihimili, ndiyo maana mauaji yanatokea,” amesema Jacinta.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Tabernacle Gospel Church (TGC), Robert Bundala ametaja ukosefu wa hofu ya Mungu na wanandoa kuanza kuishi pamoja bila kupatiwa elimu ya ndoa, kunachangia mauaji hayo.
Ameonya kuwa, hatua hiyo isipofuatwa huenda mauaji ya wanandoa yakaendelea kutokea.
Pia, ametaja changamoto ya uelewa mdogo wa jamii kuhusiana na masuala ya haki ikiwamo ya kuishi, hivyo kuchangia ukatili huo na kuitaka Serikali kuongeza nguvu kujenga uelewa miongoni mwa wananchi na kuheshimu haki mbalimbali.
“Watu wamejitenga na Mungu hata kanisani siku hizi wanakuja kuchungulia tu hakuna wanachojifunza kisha wanarudi nyumbani. Pia, zamani wanandoa walikuwa wanapewa mafunzo maalumu ya kukabiliana na changamoto za ndoa ndiyo maana matukio yalikuwa machache lakini siku hizi ni sogeza tukae,” amesema.
“Kuna haja sasa jamii iamke na kurejea kwenye misingi ya kidini na hofu ya Mungu ili kujiepusha na mauaji na kuongeza uvumilivu katika jamii na kwa wanandoa.”
Miongoni mwa matukio ya mauaji yanayohusisha wapenzi yaliyotikisa ni pamoja na lililotokea Mei 28, 2022, mfanyabiashara na Mkazi wa Buswelu wilayani Ilemela mkoani humo, Said Oswayo alimuua mke wake, Swalha Salum (28) kwa kumpiga risasi maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Said baada ya kutekeleza mauaji hayo alitokomea kusikojulikana, kesho yake mwili wake ulipatikana ukielea katika ufukwe wa Ziwa Victoria eneo la Bismark Rock jijini Mwanza huku ukiwa na jeraha linalodhaniwa kuwa la risasi kichwani.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.