Namna ya kuwa salama dhidi ya utapeli, uhalifu mtandaoni

Teknolojia ya mtandao wa kidijitali ni miongoni mwa mambo ambayo yameshika kasi wakati huu, ikitajwa kuwa kiungo muhimu cha kuongeza tija katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Mtandao hivi sasa ni hitaji la muhimu la kila binadamu na unagusa kila sehemu, sifa yake kuwa ni kurahisisha na kuyafanya mambo kwenda haraka na wakati mwingine kwa gharama nafuu. Hata hivyo neema hiyo imekuja na laana zake.

Kwa Tanzania majaribio ya ulaghai kwa njia ya simu yameongezeka kwa asilimia 57 kati ya Machi 2024 na Juni 2024 huku mkoa wa Rukwa na Morogoro ikiendelea kuwa Kinara, Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza.

Wakati majaribio hayo yakiongezeka, pia matukio ya uhalifu mtandaoni kwa mwaka 2023 nayo yalipaa huku zaidi ya Sh5.06 bilioni zilitapeliwa kutoka kwa wananchi kupitia mitandao ya simu ikihusisha kuhamisha fedha kutoka benki au kutoa pesa kwa kutumia ATM.

Ripoti ya TCRA ya robo ya mwaka unaoishia Juni 2024 inaonyesha kuwa majaribio hayo yalifikia 22,257 kutoka majaribio 17,318 yaliyokuwapo Machi mwaka huu.

Kufuatia hali hiyo, wadau wa masuala ya usalama wa mitandao, wameshauri jamii ipewe elimu ya kutosha kwani teknolojia mpya inapoingia sokoni hakuna mwongozo wowote wanaopewa wananchi bali hujifunza wenyewe bila kutambua yapi yaliyo mema na mabaya.

Ripoti ya TCRA inafafanua kuwa katika idadi ya majaribio yote yaliyoripotiwa, 14,553 yalitoka mikoa ya Rukwa na Morogoro ambayo ni zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote.

Mbeya, Dar es Salaam na Arusha zinafuata kwa majaribio ya ulaghai kwa zaidi ya 1 hadi 10 huku mikoa mingine ya Kaskazini Pemba, Kusini Unguja na Kusini Pemba ina idadi ndogo ya majaribio ambapo kila mkoa ulirekodi 0.01.

Hata hivyo, kabla ya idadi ya majaribio kufikia yaliyopo sasa, takwimu zinaonyesha kuwa kulikuwa na upungufu kwa asilimia 17.29 Machi 2024 kutoka yale yaliyokuwa yameripotiwa Desemba mwaka huu yaliyokuwa 20,939.

Katika uchambuzi wa matukio ya uhalifu kwa njia ya mtandao yaliyoripotiwa jeshi la Polisi kati ya Januari hadi Desemba 2023, Ripoti hiyo inaonyesha ongezeko la matukio 363 sawa na asilimia 36.1.

Hiyo ikiwa na maana kuwa matuko ya uhalifu yaliyoripotiwa yaliongezeka hadi kufikia 1,369 Desemba 2023 kutoka matukio 1,006 kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Uhalifu wenye idadi kubwa ya matukio ni unyanyasaji kupitia mitandao wenye matukio 475 mwaka 2023 kutoka 363 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 30.9, kutoa taarifa za uongo ongezeko kutoka 32 mwaka 2022 hadi 69 mwaka 2923 sawa na asilimia 115.6.

Matukio mengine ni ujumbe unaotumwa bila ridhaa kutoka 57 hadi 64, ponografia za wakubwa matukio 20 mwaka 2022 mwaka 2023 matukio 45 huku matusi ya kibaguzi nayo ikishika haramu kutoka matukio 75 hadi 235.

Hali ikiwa hivyo, nao wananchi wanaotapeliwa fedha kupitia mitandao ya simu wameongezeka hiyo ikihusisha kuhamisha fedha kutoka benki au kutoa pesa kwa kutumia ATM.

Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2023, jumla ya matukio 3,731 ikilinganishwa na matukio 2,951 yaliripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

Hili ni ongezeko la matukio 780 sawa na asilimia 26 ambapo Sh5.06 bilioni za wananchi zilitapeliwa na watuhumiwa 431.

Kufuatia hilo, Jeshi la Polisi linaeleza mikakati ya kupambana na masuala hayo ikiwemo Kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kushawishi taasisi za fedha kupunguza urasimu wa upatikanaji wa mikopo na kupunguza riba kubwa zinazotozwa kwa mikopo hiyo.

“Pia kuwepo na mipango ya utoaji elimu kwa umma hasa elimu ya ujasiriamali, kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kusimamia maadili ya jamii, kuelimisha watumiaji wa mitandao juu ya umuhimu wa matumizi ya neno la siri na umuhimu wa kutomwamini mtu kuhusu nywila zao,” imeeleza taarifa hiyo ya jeshi la polisi.

Pia kuendelea kutoa elimu ya sheria ya makosa ya Mtandao ya Mwaka, 2020 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Hoja ya elimu kwa watumiaji wa mitandao iliungwa mkono na mtaalamu wa masuala ya Tehama, Doreen William ambaye alisisitiza kuwa ni muhimu kabla ya watu kutumia vifaa vya kielektroniki wapewe elimu msingi ukijengwa kuanzia shule za awali.

“Tuwe na programu mashuleni ya kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya Tehama, tunaposubiri watoto wajifunze wenyewe au watu wazima kujifunza bila kuwa na msingi mzuri ni hatari kwa sababu wanaweza kutendewa uhalifu kwa kuomba taarifa zao na kuzidukua,” amesema.

Maneno yake yaliungwa mkono na Anania kapala ambaye ni Mtaalamu wa Tehama kutoka Mwananchi Communications Limited amesema kuelimisha watumiaji ni moja ya njia inayoweza kutumika kudhibiti uhalifu mtandaoni ikiwemo wizi.

“Kuhakikisha watu wanaelewa hatari za mtandao na jinsi ya kujilinda. Hii ni pamoja na kufundisha kuhusu kutengeneza nywila (passwords) imara, kuepuka kubofya (kubonyeza) viungo (link) visivyojulikana, na kutambua ulaghai wa mtandaoni,” amesema Kapala.

Amesema uwapo wa kampeni za ufahamu kupitia mitandao ya kijamii, shule, na vyombo vya habari itasaidia kuongeza ufahamu wa umma kuhusu uhalifu wa mtandaoni.

“Pia kuna suala la teknolojia na zana za usalama, zipo programu za usalama ikiwemo kutumia zana za kutambua ulaghai, kuhakikisha taarifa nyeti zinasimbwa (encrypted) ili kupunguza hatari ya kuibiwa,” amesema Kapala.

Hilo linaweza kusaidiwa kwa karibu na uwepo wa Sheria Madhubuti zinazodhibiti uhalifu mtandaoni na kuhakikisha zinazingatiwa huku udhibiti wa ufikiaji ni muhimu ili kuhakikisha tu watu waliothibitishwa wanaweza kufikia taarifa nyeti.

Kuhusu mitandao ya kijamii alipendekeza kuwapo kwa Udhibiti wa Mawasiliano: Mitandao ya Kijamii: kuweka sera za wazi kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na madhara ya lugha chafu au vitisho. Ripoti na Ufuatiliaji: Kuwahamasisha watumiaji kuripoti vitendo vya uhalifu na vitisho, na kuwa na timu za ufuatiliaji zinazoweza kuchukua hatua za haraka.

Uchambuzi wa kina kutoka kwa wataalamu hao wa Tehama unaendelezwa na Mtaalamu wa usalama mtandaoni Roshan Pyar ambaye anabainisha kuwa ongezeko la uhalifu na kuwapo kwa majaribio ya ulaghai kunaonyesha namna matumizi ya mitandao kwenye jamii ilivyoongezeka.

“Njia nzuri ya kudhibiti hili huo ni mamlaka zinazohusika zitoe elimu ya matumizi sahihi ya mitandao kwa watumishi, naona kwenye jamii ujio wa hizi teknolojia ni watu wenyewe wanajifunza hakuna siku imetangazwa ujio wa teknolojia mafunzo yakatangazwa namna ya kutumia sahihi teknolojia hizo,” amesema Pyar.

Amesema kukosekana kwa elimu hiyo kumechangia taarifa za watu kuvujishwa kwenye mitandao hivi karibuni kupitia kampuni zinazokopesha watu kwa njia ya simu.

Hilo linatokana na watu kabla ya kupewa mikopo katika kampuni hizo kutakiwa kutoa taarifa zao bila kujua na kusababisha mtu kuingiliwa faragha yake kwenye simu bila kujua na akishindwa kulipa mikopo taarifa zake husambazwa kwenye mitandao au kwa watu wa karibu.

Akidokeza kuhusu video za ngono kwa watoto mitandaoni Pyar alisema wazazi wanaruhusu watoto kuingia mitandaoni bila udhibiti wowote na hata mitandao yenyewe haimkingi mtoto dhidi ya uhalifu wowote unaoweza kutokea mtandaoni.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts