Dar es Salaam. Kamati ya Rufaa ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), imepanga kutoa matokeo ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa mgombea uenyekiti wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo.
Taarifa hiyo, imekuja leo wakati tayari Doyo akiwa ametishia kuishitaki kamati hiyo mahakamani kwa kuchelewesha majibu ya rufaa yake.
Doyo aliyegombea uenyekiti wa ADC Juni 29, 2024, alikata rufaa akipinga matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Shaban Itutu aliyepata kura 121 dhidi ya kura zake 70.
Katika rufaa hiyo, Doyo amelalamikia ongezeko la wapiga kura, mkutano kutofuata sheria ya vyama vya siasa, wajumbe wa bodi ya uongozi Taifa hawakuchaguliwa bali waliteuliwa.
Pia, amelalamikia msimamizi wa uchaguzi kuwazuia kufanya kampeni wakati wa uchaguzi na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hamad Rashid kuendelea na uenyekiti wa kikao cha uchaguzi hadi mwisho ikiwa ni kinyume na katiba na kanuni za ADC.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 1, 2024, mjumbe wa kamati hiyo, Said Miraji amesema rufaa hiyo imecheleweshwa kwa sababu walitaka kusikiliza pande za mlalamikaji na mlalamikiwa.
Amesema pia walikuwa wakikusanya vielelezo vyote ili watakapotoa majibu wasionekane kupendelea upande wowote.
“Katika moja ya vielelezo tulivyovitumia kujidhihirisha ni pamoja na kuangalia CD ya video ya mkutano wao mkuu kuona namna uchaguzi huo ulivyuoendeshwa mwanzo mwisho.
“Lingine ni kuwahoji watu wote waliotajwa katika malalamiko hayo. Hivyo kwa vielelezo vyote tulivyopvitumia, tulidhani ni jambo ambalo lisingeweza kuchukua muda mfupi, kwani kulikuwa na kazi kubwa,” amesema.
Julai 8, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati ya rufaa, Charles Kitima, Miraji alisema katika kushughulikia rufaa hiyo, wameona waanze kwanza na upatanisho ndani ya chama.
Maamuzi hayo alieleza kuwa yaliridhiwa na pande zote mbili na walijipa siku tano wawe wamemaliza kazi hiyo (yaani hadi Julai 13) na ambaye hataridhika na uamuzi ataruhusiwa kuendelea kutafuta haki katika ngazi zinazofuata.
Kwa upande wake Doyo alipotafutwa kwa simu amesema ni kutokana na kuchelewa huko kwa majibu yake, ameona Jumatatu ya wiki ijayo akafungue kesi.
Akieleza sababu za kukimbilia mahakamani, Doyo amesema mbali ya kwenda kuishtaki kamati hiyo kwa kuchelewa kumpa majibu yake, pia anakwenda kukishtaki chama hicho akidai kilivunja katiba kwenye uchaguzi mkuu uliopita.