Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke (DED), Lusubilo Mwakabibi na Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Edward Haule, bado haujakamilika.
Mwakabibi na Haule, wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka wakiwa watumishi wa Serikali, katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2021.
Hadi leo Agosti Mosi, 2024, kesi hiyo imefikisha siku 1,077 ikiwa katika hatua ya kujatwa huku upelelezi wa shauri hilo ukiwa bado haujakamilika.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Agosti 20, 2021 wakikabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya ofisi na madaraka.
Tangu siku hiyo walipofikishwa mahakamani hadi leo kesi hiyo imetimiza siku 1,077 ambazo ni sawa na miaka miwili na miezi 11 na siku 12, bila upelelezi wa shauri hilo kukamilika.
Leo, Wakili Serikali, Judith Kyamba ameieleza mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba wanaomba terehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kyamba alitoa maelezo hayo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Kutokana na maelezo hayo, hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 2, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika shtaka la kwanza ambalo ni matumizi mabaya ya ofisi, washtakiwa wanaodaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika Manispaa ya Temeke.
Siku hiyo, Mwakabibi akiwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke na Haule akiwa Mratibu wa Mradi wa DMDP, na wakiwa waajiriwa wa Manispaa hiyo, katika Utekelezaji wa ardhi walielekeza ujenzi wa stendi ya mabasi eneo la Buza, kiwanja ambacho kinamilikiwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana bila kuwa na ruhusa.
Shtaka la pili ni matumizi mabaya ya madaraka, tukio wanaodaiwa kulitenda Machi 2020 na Machi 2021 katika eneo hilo, ambapo washtakiwa kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya na kinyume na kifungu cha 3(1) Cha Sheria ya Ardhi na kifungu cha 3,4,5,7 na 11 Cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 2019, ambapo waliruhusu ujenzi wa kituo kufanyika katika eneo linalomilikiwa na kanisa.