SIKU hazigandi. Kama utani umefikia muda wa Simba kuadhimisha siku yao.
Ndio, Wazee wa Kimataifa, Simba wanajiandaa kuadhimisha siku maalumu kwa klabu hiyo maarufu kama Simba Day. Hii ni Simba ya rekodi.
Msimu huu pati limerudi tena mwezi wa nane, lakini likifanyika Agosti 3.
Tamasha hilo ni maalumu kwa ajili ya utambulisho wa kikosi na jezi mpya za msimu kwa timu ya Simba, sambamba na kutoa tuzo kwa wadau wake.
Tamasha la mwaka huu ni la 16 tangu Simba Day ilipoanzishwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa Hassan Dalali ‘Field Marshal’ na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ na wenzao ambao baadhi yao wametangulia mbele ya haki.
Kina Dalali waliasisi siku hiyo ili kukutanisha wanasimba wote bila kujali ni nani au una cheo gani, ili kupanga mikakati ya maendeleo kwa timu yao kabla ya kugeuzwa kuwa ni mahususi kutambulisha kikosi na jezi mpya za msimu ikiambatana na mechi maalumu ya kirafiki.
Mwaka huu tamasha hilo linafanyika kama ilivyo kwa misimu mingine na litapambwa na burudani mbalimbali ikiwamo kumalizia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya APR ya Rwanda.
Simba inalifanya tamasha hilo siku chache tu kabla ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ili kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ambao utakuwa wa 61 tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965.
Wanasimba wakijiandaa kufanya tamasha hilo linaloenda sawia na miaka 88 tangu klabu yao iasisiwe rasmi mwaka 1936 na Mwanaspoti inakuletea baadhi ya rekodi za kusisimua za klabu hiyo ya Simba.
Achana na rekodi za kuwa klabu ya kwanza kuvaa jezi, viatu nchini au kumiliki gari kama sio ile ya kuwazawadia nyota wa timu hiyo magari, Simba pia ina rekodi nyingine tamu ikiwamo ya kuwa timu yenye bahati ya kunyakua kila taji jipya likianzishwa.
Simba ndio klabu ya kwanza kubeba taji la Ligi ya Soka Tanzania (sasa Ligi Kuu Bara) ikifanya hivyo mwaka 1965. Klabu hiyo ilibeba bila kutoka jasho baada ya watani zao Yanga kususia mechi yao iliyovunjika dakika ya 80, huku wakiwa mbele kwa bao 1-0 na Chama cha Soka (FAT) kuamuru urudiwe na Vijana wa Jangwani kuingia mitini na Simba kupewa taji.
Simba ililitetea taji hilo kipindi hicho ikitumia jina la Sunderland kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Simba mwaka 1971. Klabu sita pekee ndizo zilizoasisi Ligi Kuu ya sasa ambazo ni Tobacco au Sigara (Pwani), Young African, Coastal Union na Manchester United (Tanga), TPC (Moshi) na mabingwa Sunderland (Pwani).
Pia Simba ndio klabu ya kwanza kubeba taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) ikifanya hivyo mwaka 1974, michuano iliyorejeshwa upya tangu ilipofanyika mara ya kwanza 1967 na kuendelea kudumu hadi sasa, msimu huu ikichezwa tena nchini.
Kama haitoshi imelibeba pia taji la Tusker lililoasisiwa mwaka 2001 na kulitetea kwa miaka mingine miwili mfululizo, kadhalika ilikuwa ya kwanza kubeba taji la michuano ya BancABCSuper8 iliyofanyika mara mmoja tu na kuzimika 2012.
Lakini, hata Simba Day ndilo tamasha la kwanza kwa klabu za soka nchini, kabla ya Yanga na Azam nao kufuata mkumbo, mbali ya kuwa klabu ya kwanza kuingia mfumo wa hisa ikiwapiga bao watani wao Yanga.
Mwaka juzi Simba ilikuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kushiriki michuano mipya ya African Football League (AFL) na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini mbele ya Al Ahly, Misri baada ya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3, japo taji lilienda kwa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Licha ya Yanga kuwa klabu ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa kwa timu za Tanzania na kufika robo fainali kwa miaka miwili mfululizo 1969 na 1970, lakini Simba ndiyo yenye rekodi tamu katika mechi za kimataifa.
Simba ndio klabu ya kwanza Tanzania kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (enzi hizo Klabu Bingwa Afrika) 1974, pia ilikuwa ni klabu ya kwanza Bongo kufika fainali za Afrika ikifanya hivyo kwenye Kombe la CAF 1993.
Simba ilipoteza 2-0 nyumbani mbele ya Stella Abidjan baada ya suluhu ya mechi ya ugenini, Ivory Coast, kabla ya Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho 2022.
Wekundu hao, pia ndio klabu pekee nchini kuwahi kumvua taji mtetezi wa Afrika ikifanya hivyo 2003 dhidi ya Zamalek ya Misri na kutinga makundi.
Na inashikilia rekodi ya kucheza hatua ya robo fainali za Afrika kwa misimu mitano katika miaka sita.
Msimu uliopita ilikwamia kwa Al Ahly ya Misri, ikiwa sambamba na watani wao Yanga waliong’olewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Pia Simba ndio timu pekee ya Tanzania inayozitetemesha klabu za Ukanda wa Afrika ya Kaskazini maarufu kama Waarabu kwani imekuwa ikizinyanyasa hasa zikija Tanzania.
Klabu nyingine kama Yanga nayo kwa sasa imeanza kuzinduka baada ya muda mrefu wa kutaabika hasa ilipokuwa ikikutana na timu za Misri ikiwamo Al Ahly na kwa sasa Yanga inashinda hata ugenini dhidi ya Waarabu baada ya kelele nyingi za watani wao waliokuwa wakizinyanyasa timu hizo.
Ni kweli Yanga ndio klabu ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani wa jadi nchini ikiisulubu Simba mabao 5-0 mnamo Juni 1, 1968, ila inateseka na kipigo cha paka mwizi cha 6-0.
Simba ililipa kisasi na kuandikisha rekodi inayowatesa Yanga kwa miaka 47 ilipoitandika mabao 6-0 Julai 19, 1977 ikishuhudiwa King Abdallah Kibadeni akipiga hat-trick pekee katika Dabi ya Kariakoo hadi leo hii.
Kama haitoshi wakati Yanga ikipambana kutaka kufuta aibu hiyo wakati ikitimiza miaka 35, iliongezewa tena dozi nyingine kwa kukandikwa mabao 5-0 na Simba katika mechi ya Mei 6, 2012, japo Novemba 5 mwaka jana, Yanga ilijikomboa kwa kumrarua Mnyama kwa mabao 5-1.
Hata kwenye michuano mingine Simba imekuwa ikitoa dozi kwa watani wao, ikifanya kwenye Kombe la Tusker na Mapinduzi na hata miaka michache iliyopita katika Kombe la Shirikisho (ASFC) waliwanyoosha watani wao kwa mabao 4-1.
Ukiondoa mataji 22 iliyonayo katika Ligi Kuu Bara ikiwa nyuma ya Yanga iliyotwaa mara 30, Simba pia ina mataji mengine lukuki yanayoifanya itishe kwa klabu za Tanzania.
Katika Ligi, Simba ilibeba mataji yake 22 katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2009-10, 2011-12, 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Haya manne ya mwisho imeifanya iweke rekodi kwa miaka ya hivi karibuni kwa timu iliyotwaa mara nne mfululizo.
Katika Kombe la Kagame Simba inashikilia rekodi ya kubeba mataji mengi ikifanya hivyo mara sita ikiwa sambamba na AFC Leopards ya Kenya. Simba imetwaa taji hilo katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.
Simba pia inashikilia rekodi ya kubeba Kombe la Tusker mara nyingi zaidi kwa klabu za Afrika Mashariki ikifanya hivyo mara nne 2001, 2002, 2003 na 2005.
Katika Ligi Kuu ya Muungano pia ilimenyakua jumla ya mataji sita ikifanya hivyo 1993, 1994, 1995, 2001, 2002 na mwaka huu wa 2024 michuano hiyo iliporudishwa kinyemela, huku katika Kombe la Nyerere (sasa FA) imenyakua mara sita miaka ya 1984, 1995, 2000, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021.
Jumla ya mataji hayo ni 44 hapo hayajawekwa ya Ngao ya Jamii iliyotwaa mara 10 ikiwa ndio klabu kinara hapa nchini tangu mwaka 2001, Kombe la CCM ama lile la Kombe la Mapinduzi walilowahi kutwaa mara nne wakiwa nyuma ya Azam ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo ikibeba mara tano.
Sasa kwa rekodi hizo tamu kwa nini Simba a.k.a Wekundu wa Msimbazi wasiitwe ‘Taifa Kubwa’? Huu sasa ndio Ubaya Ubwela na hawa ni Wazee wa Kimataifa!