WANACHAMA na wapenzi wa Simba wamejitokeza kutoa damu units 17 katika Hospitali ya Rufaa ya Songea (HOMSO) kwa ajili ya kusaidia watoto 85 wa umri wa chini ya miaka mitano wa mkoa wa Ruvuma.
Wanachama hao wamejitokeza kwa wingi Julai 30, 2024 ikiwa ni wiki ya Kilele cha Simba Day 2024 ambapo wamekuwa wakichangia damu kila mwaka.
Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Songea, Juma Ndago amesema hiyo si mara ya kwanza kwa mashabiki wa klabu hiyo kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa wenye matatizo mbalimbali wakiwemo kinamama wajawazito, wagonjwa ambao wamepata ajali na watoto wachanga.
Ndago amesema, wanachama wa Simba wamekua na desturi ya kuchangia damu na kujitolea vifaa mbalimbali vya matibabu pia wafike kwa wingi kusherehekea kilele cha tamasha la Simba Day ambayo kimkoa inafanyika wilayani Mbinga.
Zedania Mgale, kiongozi wa wanachama hao amesema kuchangia damu ni sadaka kubwa, kwani wanaenda kusaidia watu wenye shida imekuwa ni kawaida yao
utamaduni wao kujitoa kila mwaka kuchangia damu ni sadaka kwa watu wenye matatizo mbalimbali.
Kwa upande wa mwanachama, Esther Nyirenda amesema, wagonjwa wengi wana shida ya damu na wanahitaji msaada hivyo wananchi, wasiogope kutoa damu kwani ni jambo la kawaida watasaidia watu wenye shida.
Yassin Mohammed, amesema wananchi waige ambacho wanasimba wanakifanya kwani raha ya mwanasimba yeyote ni kushinda na kusaidia watu ambao wana shida mbalimbali.
Mtumishi Kitengo cha Damu Salama, Said Abdallah, amesema uhitaji wa uniti 300 za damu bado ni mkubwa, lakini uchangiaji utasaidia kupunguza vifo vya kinamama wajawazito, watoto na wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji.
Amesema, wananchi wajitokeze kuchangia damu ili kuhokoa maisha ya ndugu zetu wenye uhitaji wa damu.
Aidha, amewatoa hofu wananchi kuwa uchangiaji wa damu hauna madhara yoyote hivyo wapuuze maneno yanayotolewa mitaani.
Mwanasimba Hajika Wadari amefurahi kuchangia damu akisema anaamini itawasaidia wanawake wenye matatizo mbalimbali ya uzazi.
“Wanawake wajitahidi kujitokeza kutoa damu wasiogope,” amesema.
Mganga Mfawidhi, Magafu Majura amewashukuru wanachama na mashabiki wa simba kwa kujitolea kwenye Wiki ya Simba 2024 kwani damu waliyotoa itasaidia sana wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
Amewapongeza wachezaji waliokubali kusajiliwa na Simba pia ameomba wananchi wajitokeze kuchangia damu kwa hiari na waache kuogopa kuwa watapimwa ukimwi na homa ya ini, akisema kabla ya kutoa damu hupimwa kwanza uzito, presha kisha ndipo watatolewa damu.