Steinmeier ameomba radhi kwa madhila waliopitia Wapoland mikononi mwa watawala wa kinazi wa Ujerumani. Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amekutana na baadhi ya manusura wachache walio hai wa uasi wa Warsaw wa mwaka 1944, na kuzungumza kwenye kumbukumbu hiyo katika mji mkuu wa Poland Warsaw. Jaribio la siku 63 la vikosi vya upinzani vya Poland mwishoni mwa vita vikuu vya pili vya dunia kuwafurusha wakaliaji wa Kinazi kutoka mjini humo, ambao mwishowe ulisambaratishwa vibaya na jeshi la Ujerumani, ulianza Agosti 1, 1944.
Steinmeier amesema uasi wa Warsaw ni mmoja ya matukio yenye umuagaji mkubwa zaidi wa damu katika historia ndefu ambayo watu wa Poland na Ujerumani wanashiriki. Na ni mmoja ya matukio ya kishujaa zaidi katika historia ya Poland. Steinmeier ndiyo rais wa pili wa Ujerumani, baada ya Roman Herzog mnamo mwaka 1994, kualikwa kuzungumza katika hafla nchini Poland. Alialikwa na rais wa Poland Andrezej Duda na Meya wa Warsaw Rafal Trzaskowski.
Soma pia: Uasi wa Ghetto la Warsaw, miaka 80 baadae
Rais huyo wa Ujerumani alisema, akiwalenga hasa maveterani, ambao ni mashujaa wa uasi wa Warsaw waliokuwa wamekaa mbele yake, kwamba hakuna maneno yanayoweza kutenda haki kwa ukatili uliofanywa dhidi ya mji huo wakati wa miezi miwili ya uasi huo. “Na kwa hivyo napenda kusema sentensi moja tu, lakini ambayo inatoka moyoni kabisaa na ya dhati kabisaa. Hapa, na sasa hivi: Naomba msamaha.”
Steinmeier pia alikiri kuwa maridhiano kati ya Ujerumani na Poland yamekuwa mchakato mgumu kwa pande zote mbili, lakini hasa kwa Poland, kutokana na ukatili wa Vita vya Pili vya Dunia na mauaji ya Holocaust, ambayo 4kwa sehemu kubwa yalifanyika katika ardhi ya Poland iliyokuwa inakaliwa.
Pia aligusia kile Berlin inachotaazama kama mafanikio ya hivi karibuni juu ya mada tata ya fidia au fidia kutoka Ujerumani, ambayo ni juhudi za hivi karibuni za kufikia muafaka na serikali mpya inayoongozwa na Donald Tusk. Uhusiano kati ya Ujerumani na Poland ulishuka wakati wa utawala wa miaka kadhaa ya chama cha kihafidhina cha Sheria na Haki, PiS, ambacho kilidai fidia kubwa zaidi kutoka Ujerumani, wakati serikali ya Ujeurmani ikisistiza suala la fidia lilitatuliwa kisheria katika mikataba iliyopita.
Wakati wa ziara ya karibuni ya Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk nchini Ujerumani, serikali mbili zilipendekeza mipango ya kujenga jumba la Ujerumani na Poland mjini Berlin, na kuanzisha Jukwaa la ukumbusho wa mateso ya Poland na waathirika wa Vita vikuu vya Pili vya Dunia.