Straika Simba atoroka kambini | Mwanaspoti

WAKATI Simba Queens ikiwa kambini Bunju jijini Dar es Salaam kujiandaa na michuano ya Klabu Bingwa kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa wanawake inaotarajiwa kuanza katikati ya mwezi huu, straika wa timu hiyo, Aisha Mnunka hayuko na timu.

Michuano ya CECAFA kwa msimu huu itafanyika Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Agosti 17 hadi Septemba 04 ambapo Simba imepangwa Kundi B ikiwa pamoja na timu za PVP Biyenzi ya Burundi, Kawempe Muslim Ladies ya Uganda na FAD (Djibouti).

Mnunka msimu uliopita aliibuka kinara wa mabao wa Ligi Kuu (WPL) akifunga 20 katika mechi 18.

Inaelezwa tangu Simba waingie kambini inakwenda wiki sasa na bado mchezaji huyo hajafika kwenye timu na viongozi wakiwa hawana taarifa yoyote juu.

Mwanaspoti linafahamu, baada ya mchezaji huyo kurudi katika majukumu ya timu ya taifa ‘Twiga Stars’ hajaonekana kambini na simu yake haipatikani, lakini kuna ofa kubwa amepata hapa kwenye timu itakayoshiriki Ligi msimu ujao.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo alisema “Tunajua bado ana mkataba wa mwaka mmoja tutatuma ofa kwa klabu hiyo kumsajili moja kwa moja kwa sababu ni mshambuliaji mzuri na tunatamani kuwa nae.”

Juhudi za kumpata Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya na mchezaji huyo lakini simu yake haikupatikana.

Related Posts