Tanzania yaipa homa Msumbiji kufuzu Kombe la Dunia kriketi

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Kocha wa timu ya kriketi ya Msumbiji, Filipe Cossa amesema  Tanzania ni ndiyo   timu  inayoweza kumzuia katika mashindano kriketi ya kufuzu kombe la dunia, daraja la pili (Divisheni II) kwa vijana wenye umri chini ya miaka 19.

Michuano hiyo ambayo itashirikisha  jumla ya Mataifa nane, inatarajiwa kuanza kesho kwenye viwanja vya Gymkhana na Chuo Kikuu Dar es Salaam(UDSM).

Akizungumzia maandalizi yao mbele ya waandishi wa habari leo Agosti Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam kocha huyo amesema  anaihofia Tanzania kutokana na ubora wake na pia inacheza katika ardhi ya nyumbani.

“Kwa hali ilivyo Tanzania ndiyo timu  inaweza kutuzuia kufuzu kwa sababu inacheza nyumbani. Malengo yetu ni kufuzu kwenda Division I, tumejipanga kucheza kwa nidhamu na kutoa ushindani kwa wapinzani wetu,” amesema Cossa.

Naye Kocha Msaidizi wa timu kriketi ya vijana Tanzania, Salum Jumbe  amesema  wapo tayari kufuzu safari hii kutokana na maandalizi waliyofanya.

“Tunavijua viwanja vyote ambavyo tutatumia kwenye mashindano, vijana wako vizuri na safari hii hatutawaangusha Watanzania, tupo tayari kufuzu,” amesema Jumbe.

Kwa mujibu wa ratiba mechi  ufunguzi Tanzania itakutana na Nigeria kwenye viwanja vya Gymkhana, huku Msumbiji ikicheza dhidi ya viwanja UDSM.

Kwa upande wake Mratibu wa mashindano hayo, Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), Atif Salim amesema katika michuano hiyo timu zimepangwa katika makundi mawili yenye kila kundi timu nne, Tanzania ipo kundi  A na Nigeria, Msumbiji na Malawi, huku kundi B likiundwa na Ghana, Botswana, Sierra Leone na Rwanda.

Amefafanua kuwa washindi wawili wa kila kundi watacheza nusu fainali, kisha fainali  na kutafuta mshindi wa tatu.

“Watakaocheza fainali tayari wote watakuwa wamefuzu kwenda Division I, na nchi itakayokuwa mshindi wa tatu nayo itafuzu kwenda mbele Division I,” ameeleza Atif.

Related Posts