WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi akizindua rasmi huduma za usafiri wa reli ya kisasa (SGR), treni iliyokuwa imebeba wageni walioshiriki uzinduzi huo wakiwamo mabalozi na abiria kutokea mkoani Dodoma, imepata tena hitilafu karibu na Stesheni ya Morogoro kwa zaidi saa moja sasa.
Treni hiyo iliyoanza safari 2:10 jijini Dodoma, imekwama kwa zaidi ya saa 2 baada ya kukatika kwa mfumo wa umeme hali iliyosababisha kusimama ghafla huku wahudumu wa treni hiyo wakitoa tahadhari kwa abiria kutotoka nje.
Hata hivyo, baadhi ya abiria hao waliwasiliana na Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima ambaye aliahidi kufuatilia tatizo hilo kwa uongozi wa TRC, ilihali Mkurugenzi wa TRC naye alipopigiwa simu naye alidai kuna treni wanabadilisha ya treni.
Hayo yanajiri ikiwa zimepita siku mbili baada shirika hilo kuomba radhi kwa treni yake iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili kati ya stesheni ya Kilosa na Kidete mkoani Morogoro juzi tarehe 30 Julai 2024.
“Taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu za aina hiyo husababishwa na wanyama (ngedere) au ndege (bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system),” amesema.